Viongozi watakiwa kufanya kazi kwa weledi

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa Askofu mstaafu Dk. Elinaza Sendoro akimkabidhi Tuzo ya mchango uliotukuka aliotoa kwa chuo hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikari (NaCONGO) Lilian Badi wakati wa mahafali ya 24 ya chuo hicho, mjini Iringa .
Muktasari:
Mwenyekiti Baraza la Taasisi zisizo za kiserikali nchini, Lilian Badi ametoa wito kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya Serikali kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili mchango wao uwe na tija kwa jamii wanayoiongoza.
Iringa. Mwenyekiti Baraza la Taasisi zisizo za kiserikali nchini, Lilian Badi ametoa wito kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya Serikali kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili mchango wao uwe na tija kwa jamii wanayoiongoza.
Wito huo umetolewa katika mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) baada ya kukabidhiwa tuzo ya Kiongozi mwenye mchango wa maendeleo ya chuo hicho yaani Iringa University Deveroper Award.
Lilian amesema tuzo hiyo inamchango mkubwa katika kuhamasisha viongozi kuwajibika katika nafasi walizopewa ili kuwatumikia wananchi.
Tuzo hiyo hutolewa kwa viongozi wa juu serikalini ambao wametoa mchango wamkubwa kwa chuo hicho au tasnia ya elimu kwa ujumla.
Akishukuru kwa tuzo hiyo alikipongeza chuo hicho kwa kuendelea kushirikiana na serikali kuboresha sekta ya elimu na mazingira yake ya mafunzo kulingana na mahitaji.
"Chuo hiki ni mfano wa kuigwa nchini kina sifa ya kutoa wahitimu wengi wanaotumia maarifa yao kwa manufaa ya Taifa"
Miongoni mwa waliotunukiwa Tuzo hizo za heshima ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Azam Media Tido Muhando,Mkuu wa Usalama wa Taifa Nchini Diwani Athumani na Aliyekuwa Mkuu wilaya ya Iringa Richard kasesela.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ndelilio Urio amesema Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa amepata tuzo hiyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika chuo hicho wakati akiwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Profesa Urio amesema akiwa Takukuru alisaidia kuendesha uchunguzi katika chuo hicho uliosaidia kudhibiti vitendo vya rushwa vilivyokitikisa chuo hicho.
Amewasihi wahitimu zaidi ya 1400 katika mahafali hayo ya 24 wakiwemo wa shahada ya uzamili, stashahada ya uzamili, shahada ya kwanza, stashahada na astashahada katika fani mbalimbali kuitumia elimu waliyoipata kujiletea naendeleo na kuepuka vitendo vya rushwa.
"Mkaitumie elimu mliyopata kukabiliana na changamoto mbalimbali mtakazokutana nazo huko mnakokwenda ili mjiletee maendeleo, kuondoa umasikini na kuboresha maisha yenu mkaepuke rushwa ya aina yeyote ile"
Alimtaka kila mmoja bila woga kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa, dhuluma, ukatili wa kijinsia na mambo mengine yanayoweza kuathiri maendeleo yao na ya Taifa.
Pamoja na tuzo hiyo ya Mlima Kilimanjaro, chuo hicho pia kimemtunuku Mkurugenzi wa Azam Media, Tido Mhando tuzo ya heshima ya kuchochea maendeleo kutokana na kutambua na kuthamini mchango wa Azam Media katika kulea na kukuza wahitimu wa chuo hicho na sekta ya habari nchini.
Wengine waliowahi kupewa tuzo hiyo ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brig. Jen. John Mbungo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Salvatory Venance Mabeyo.
Mwisho.