Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vipaumbele vitano bajeti ya 2022/2023

Muktasari:

  • Serikali imetangaza mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023, ikiweka bayana kuwa inatarajia kutumia Sh41 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ya bajeti inayomalizika

  

Dodoma. Serikali imetangaza mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023, ikiweka bayana kuwa inatarajia kutumia Sh41 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ya bajeti inayomalizika.

Katika mwelekeo huo, baadhi ya mambo yaliyozingatiwa ni ongezeko la mishahara, ajira mpya, upandishaji wa madaraja kwa watumishi na sensa ya makazi.

Bajeti ya Serikali iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka 2021/22 ilikuwa Sh37.9 trilioni, kati ya kiasi hicho, Sh23 trilioni zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 14.9 trilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Hata hivyo, katika mkutano wa sita wa Bunge la 12, wabunge waliridhia Serikali kuongeza matumizi ya zaidi ya Sh1.3 trilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 na kuifanya bajeti hiyo kuongezeka kutoka Sh36.66 trilioni hadi kufikia Sh37.98 trilioni.

Mapendekezo hayo ya nyongeza yaliwasilishwa kwenye mkutano wa sita wa Bunge la 12 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Hamad Masauni kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Alisema Serikali ilipata mkopo usio na riba kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wenye thamani ya Sh1.3 trilioni, sawa na dola za Marekani milioni 567.3.

“Fedha hizo zilizopatikana hazikuwa sehemu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge katika mwaka 2021/22, hivyo Serikali inawajibika chini ya kifungu cha 43 cha Sheria ya Bajeti, sura 439 na Ibara ya 137 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwasilisha bungeni mapendekezo ya kuomba ridhaa ya Bunge kutumia fedha za mkopo huo,” alisema Masauni.

Alisema fedha hizo zitatumika kuwakinga Watanzania dhidi ya maambukizi ya Uviko-19 na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii zilioathirika na ugonjwa huo kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani.

Mwelekeo wa bajeti

Jana Waziri Mwigulu aliwasilisha kwa wabunge taarifa ya mapendekezo ya mfumo wa ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23, akisema jumla ya Sh41 trilioni zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.

“Mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti ya mwaka 2022/23 yamezingatia: Mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ikijumuisha ulipaji wa deni la Serikali, mapendekezo ya mahitaji ya nyongeza ya mshahara, upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma, ajira mpya, sensa ya watu na makazi na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa,” alisema Mwigulu.

Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa zaidi ya Sh28.6 trilioni, sawa na asilimia 69.9 ya bajeti yote.

Alisema kati ya mapato hayo, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 11.1 hadi Sh24.1 trilioni kutoka makadirio ya zaidi ya Sh21.7 trilioni mwaka 2021/22.

Mwigulu alisema mapato yasiyo ya kodi (wizara, idara, taasisi na mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuongezeka zaidi ya Sh4.5 trilioni mwaka 2022/23 kutoka zaidi ya Sh3.9 trilioni mwaka 2021/22.

“Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kufikia zaidi ya Sh4.1 trilioni, sawa na asilimia 10.1 ya bajeti yote,” alisema.

Alisema Serikali inatarajia kukopa zaidi ya Sh5.3 trilioni kutoka soko la ndani ambapo zaidi ya Sh3.3 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Sh2 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

“Serikali inatarajia kukopa Sh2.8 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu,” alisema.

Mishahara kuongezwa

Pia, Mwigulu alisema katika bajeti ijayo zimetengwa fedha kwa ajili ya mishahara, ikiwamo nyongeza ya mishahara, upandishaji madaraka na ajira mpya.

“Kati ya fedha hizo, Sh25.5 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni asilimia 62.2 ya bajeti yote, ikijumuisha Sh11.3 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu na Sh9.7 trilioni kwa ajili ya mishahara, ikiwemo nyongeza ya mshahara, upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya,” alisema Mwigulu.

Maeneo ya vipaumbele

Mwigulu alisema mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti ya mwaka 2022/23 yatakuwa ni ya pili katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”.

Aliyataja maeneo ya vipaumbele yatakayozingatiwa ni kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23.

Mwigulu alisema utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 utajumuisha ugharamiaji wa miradi ya kielelezo inayoendelea.

“Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, deni la Serikali, mishahara ya watumishi na huduma za kijamii, ikiwemo afya, elimu na maji na pia kuweka mazingira wezeshi ili kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi,” alisema.

Alisema miradi itakayotekelezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 ni miradi katika maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa ambayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji.

“Kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu. Aidha, msisitizo umewekwa katika miradi ya kielelezo ambayo ni ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere – MW 2,115, bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga eneo la Chongoleani na ufufuaji wa Shirika la Ndege Tanzania.

Mapendekezo

Alisema Serikali katika mwaka ujao wa fedha imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.2 mwaka 2022 kutoka matarajio ya ukuaji wa asilimia 5.0 mwaka 2021.

Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0 katika muda wa kati.

Alisema Serikali imedhamiria kuongeza mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya halmashauri) kufikia asilimia 16.3 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23, mapato ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23 kutoka matarajio ya asilimia 13.3 mwaka 2021/22.

Pia, alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Ajira TRA

Aidha, Dk Mwigulu aliwaambia wabunge kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ajira mpya 2,100 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Alisema pia TRA inatakiwa kuendelea kufanya utafiti wenye lengo la kupanua wigo wa kodi hasa katika maeneo ya biashara mtandao na wachimbaji wadogo wa madini.

Mwigulu alisema kipindi cha Julai 2021 hadi Januari 2022, mapato yaliyokusanywa na TRA (ya kodi na yasiyo ya kodi) yalikuwa zaidi ya Sh12 trilioni, sawa na asilimia 92.8 ya makadirio ya kipindi hicho.

Alisema kati ya mapato hayo, mapato ya kodi yalikuwa Sh11.5 trilioni na mapato yasiyo ya kodi ni Sh 514.8 bilioni.