Virusi vya corona vilivyotibua biashara Kariakoo

Dar es Salaam. Wafanyabiashara katika soko la Kariakoo jijini hapa wameelezea namna ambavyo virusi vipya vya corona vinavyozidi kuathiri biashara zao.

Wakati mlipuko huo ukigusa eneo hilo muhimu la kibiashara, ripoti ya utafiti ya taasisi ya Lancet imeonyesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo hatari ya kuingia kwa virusi hivyo ni ya wastani na kushauri hatua kadhaa zichukuliwe kujiandaa kukabiliana na tatizo hilo endapo maambukizi yatabainika.

Taarifa ya Lancet imesema hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa mapema ni kutenga rasilimali za kuwezesha kukabiliana na virusi hivyo, kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa watendaji na kuimarisha ufuatiliaji.

Soko la Kariakoo ambalo ni la kimataifa ni kitovu cha biashara nchini na huhusisha bidhaa kutoka China na mataifa mengine na hivyo kuvutia wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kuzifuata.

Lakini mlipuko wa virusi vya corona, ambao tayari umeshaua takriban watu 3,000 na kuambukiza wengine zaidi ya 80,000 umefanya safari kadhaa za ndege kwenda na kutoka China zisimamishwe, huku maeneo kadhaa yakiwekewa karantini.

“Asilimia kubwa ya wafanyabiashara wanaofuata mzigo China walikuwa wanatumia bandari kama lango kuu la kuingizia bidhaa zao,” alisema Abdallah Mwinyi, katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT).

Mwinyi alisema athari za mlipuko huo wa virusi hivyo vya corona hazitaonekana kwa wafanyabiashara pekee.

“Sasa kama hali itaendelea kuwa hivi, Serikali itakosa kodi waliyokuwa wakiilipa,” alisema Mwinyi.

Mbali na wafanyabishara wa ndani, soko hilo pia hutumiwa na wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji, Malawi, Zambia na Zimbabwe ambao hununua bidhaa kama nguo, vyombo vya ndani na vifaa vya kielektroniki.

Kufungwa kwa shughuli za biashara na huduma nyingine nchini China ni hatua iliyochukuliwa na uongozi wa nchi hiyo, kuepuka maambukizi zaidi ya virusi hivyo. Takwimu kutoka ubalozi wa China nchini zinaonyesha kuwa kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2017, biashara kati ya Tanzania na China imekuwa ikikua kwa kasi.

April mwaka jana, balozi wa China nchini, Wang Ke alisema biashara kati nchi hizo imekuwa hadi kufikia Sh9.1 trilioni na kwamba kwa sasa Tanzania ni mshirika mkubwa wa China kibiashara.

Wasemavyo wafanyabiashara

Mlipuko wa virusi hivyo sasa umeanza kuathiri upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko hilo maarufu Afrika Mashariki.

“Kila baada ya wiki mbili nilikuwa naingiza dukani mzigo kutoka China, lakini hali imekuwa tofauti kwa zaidi ya mwezi,” alisema Bertha Mushi, mfanyabiashara wa Kariakoo, alipozungumza na Mwananchi jana.

“Sipati mzigo mpya, biashara imekuwa ngumu. Sasa hivi duka langu lipo tupu kama unavyoona. Hatupati bidhaa na mzigo ambao nilipokea kwa mara ya mwisho ni ule uliokuwa njiani kabla ya virusi hivyo kusambaa.”

Alisema alikuwa akimtumia wakala kupata mzigo kutoka China, lakini mtu huyo aliyekuwa ameweka makazi kati nchi hiyo, alilazimika kurudi Tanzania ili kuepuka maambukizi.

Kwa Zainabu Katala hali ni tofauti ambaye mbali ya China, huagiza mizigo nchi nyingine.

“Hata nchi nyingine nimeshindwa kwenda kufuata mzigo kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona,” alisema Katala.

“Kuna Uturuki na Thailand sehemu ambazo pia nilikuwa nafuata mzigo, lakini hizi taarifa za ugonjwa huo kuingia nchi tofauti kila kunapokucha zinaleta shida.”

Alisema kwa sababu wanashindwa kupata mzigo mpya wamejikuta wakitumia hadi fedha za mitaji katika mambo mengine.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara walionyesha hofu yao kuwa huenda biashara zikaanza kufungwa kutokana na kukosa bidhaa.

“Mtu ukikaa miezi mitatu hujapata mzigo mpya mzunguko wa fedha unatoka wapi?” alihoji mfanyabiashara mwingine, Yusuph Maduhu.

“Kodi ya pango la biashara inatoka wapi? Mikopo italipika vipi? Ni suala lisilowezekana, mwisho wa siku si ndiyo biashara zitafungwa sasa?

“Tuombe Mungu atusaidie tiba ipatikane nchi ya China iwe salama ili watu tupate bidhaa kwa sababu nchi nyingi tunategemea soko hilo.”

Mmoja wa wafanyabiashara kutoka DRC aliiambia Azam Tv juzi jinsi wafanyabiashara kutoka nje walivyoathirika. “Biashara inakuwa ngumu. Hata sisi wanunuzi kutoka Congo tunapata shida kwa sababu tumekuwa tukinunua kitu kilekile,” alisema.

Athari za ugonjwa huo katika soko la China hazijaonekana kwa wafanyabiashara wakubwa tu bali hata wamachinga wameguswa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wamachinga Kariakoo, Steven Lusinde alisema hali hiyo imeonyesha mabadiliko ya bei hata kwao kwa kuwa wamekuwa wakitegemea wafanyabiashara wakubwa wanaokwenda China.