Undani sakata la vyama 19 vya wafanyakazi kuunda shirikisho jipya

Muktasari:

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) linaundwa na vyama 13 wakati vyama vingine vya wafanyakazi vilivyo nje ya Tucta vikiwa 19.

Mwanza. Wakati maandalizi ya sherehe za sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi) yakiendelea, vyama 19 vya wafanyakazi wa sekta binafsi vinakusudia kuanzisha shirikisho lao,  kwa sababu ya kile wanachodai kutengwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).

Akizungumza na Mwananchi kuhusu azma yao, mwenyekiti wa mpito wa vyama hivyo 19 vilivyo nje ya Tucta, Michael Pamaga amesema kutokana na vyama hivyo kutengwa kwenye shirikisho hilo ikiwemo kutoshirikishwa kwenye sherehe za Mei Mosi, wameamua kuanzisha shirikisho lao. Amesema hivi sasa wako katika hatua ya awali ya mchakato wa usajili.

“Sijapata mwaliko wa kushiriki Mei Mosi, mwaka huu na miaka yote huwa hatupewi, tunajaribu kuhangaika kuzungumza na watu na viongozi mbalimbali namna ya kukamilisha mchakato lakini naona kuna sintofahamu.Hatujawahi kushirikishwa officially (rasmi), huwa tu tunaenda kama tukiamua kwenda…ki kawaida huwa inatakiwa vyama vyote vialikwe kwa barua rasmi,” amesema.

Hata hivyo, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya amekanusha madai ya kutengwa kwa vyama hivyo akisema katika maadhimisho ya Mei Mosi, mwaka huu wamealika vyama vyote vilivyopo kwenye shirikisho hilo na ambavyo havipo na kuwa madai ya vyama hivyo yamelenga kuharibu sherehe hizo.

“Vyama vimealikwa vyote kuanzia kwenye maandalizi yanayohusisha michango, sasa hawajachanga na sio wao tu wapo hata wengine waliopo kwenye shirikisho tumewaalika lakini pia hawajaja,” amesema na kuongeza:



Rais waTucta, Tumaini Nyamhokya

“Hapa tunaendelea na maandalizi na kuna ambao tunashirikiana nao zaidi ya vyama sita ambao hawako kwenye shirikisho, tunashirikiana nao kuanzia mwanzo. Hao wanaolalamika tuliwaalika, tulialika vyama vyote vilivyopo kwenye shirikisho na ambao hawapo kwenye shirikisho, hao wasitumie magazeti kutaka kuharibu sherehe yetu.”

Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, hadi Agosti 2020, jumla ya vyama vya wafanyakazi vilivyosajiliwa vilikuwa 32.

Baadhi ya vyama hivyo ni Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (Tuico), Chama cha Wafanyakazi Mashambani na Kilimo Tanzania (TPAWU), Chama cha wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi (COTWU), Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyingine (Tamico), Chama cha Wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRAWU) na Chama cha Wafanyakazi wa Uvuvi na Majini (Tafimu).

Vyama vingine ni Umoja wa Mabaharia Tanzania (Tasu), Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti (Raawu), Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU),  Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahoteli, Majumbani na kazi nyinginezo (Chodawu) na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe).

Pia, kuna Umoja wa wafanyakazi wa viwandani (IGWUTA), Chama cha Wafanyakazi wa Huduma za Jamii Tanzania (Tasiwu), Chama cha Kulinda Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (Chakuhawata), Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU), Chama Cha Wafanyakazi wa Tasnia Ya Habari Tanzania (JOWUTA), Chama Cha Walimu wa Shule Binafsi Tanzania (TPTU) na Chama cha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TAREWU).

Pamaga amesema walishajaribu kuunda shirikisho lao miaka ya nyuma ikashindikana, lakini kwa sasa wamepiga hatua ikiwemo kuwa na jukwaa la muda la kuunda shirikisho la pili la vyama vya wafanyakazi.

“Sisi sio members (wanachama) kwenye Tucta sababu Tucta wana member 13 na sisi tupo 19, sasa hivi tunaendelea na mchakato wa kuanzisha shirikisho letu kwa sababu jitihada za huko nyuma hazikuzaa matunda. Tumeanzisha tena hilo vuguvugu ndio tunaendela nalo sasa hivi.

“Sasa hivi bado tunaita kama jukwaa na tumeshafanya vikao viwili bado hatujafikia mwisho maana kabla ya kufika mwisho tutasaini fomu maalumu ya makubaliano ya hivi vyama 19 maana fomu hizo huwa zinasainiwa halafu ndiyo mnapeleka kwa msajili wa vyama vya wafanyakazi. Hatujafikia hiyo hatua, kwa hiyo bado vikao vinaendelea,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule  Binafsi nchini (TPTU) ambacho ni miongoni mwa vyama 19, Julius Mabula amesema kwa uzoefu wake wa miaka sita tangu chama chao kisajiliwe, hawajawahi kushirikishwa kwenye sherehe hizo akiomba mambo hayo yakomeshwe.

“Sisi kupitia chama chetu tumeyalalamikia mno miaka yote mpaka mwaka 2022, tuliyafikisha kwa  Rais Samia Suluhu Hassan na aliyatolea maelekezo kwenye sherehe za Mei Mosi za mwaka 2022 kitaifa zilizofanyikia  Dodoma, lakini baada ya hapo wasaidizi wake hawakuchukua hatua zozote.Zaidi  tulisikia kuwa waliandaa mwongozo wa namna sherehe hizo ziwe zinafanyikaje kwa utaratibu jumuishi, mwongozo ambao hatujawahi hata kuuona wala haujawahi hata kutumika na hatujui uliko,” amesema.

Amesema baada ya vyama hivyo 19 kuonekana kutengwa kwenye matukio muhimu, vikaona njia sahihi ni kuanzisha shirikisho lao ambalo litakuwa linatetea maslahi ya wafanyakazi hususani wa sekta binafsi nchini.

“Vyama 19 vilishatengwa nje ya shirikisho hilo, kwa kuwa tu hivyo vyama vilianzishwa kutoka ndani ya vyama hivyo 13 vilivyomo ndani ya shirikisho baada ya hivi vyama kuanzishwa na ni matakwa ya kisheria, kwani sheria inaruhusu hilo jambo la kuanzisha chama kipya ama kutoka ndani ya chama fulani mkajimega au kutojimega kutoka ndani ya chama chochote, kama ilivyo kwenye vyama vya siasa. Vyama vinajimega na kuanzishwa vingine, kwa hiyo hivi vyama vilivyoanzishwa kwa kujimega kutoka kwenye vyama hivyo vilivyoko ndani ya shirikisho, vilianza kuitwa ni vyama vilivyoasi,” amesema na kuongeza.

“Vikaonekana ni vyama ambavyo havipaswi kupewa nafasi yoyote ya kuwa kwenye shirikisho la vyama vya wafanyakazi, vibaki tu huko nje ya shirikisho kwa sababu ni vyama vilivyoasi. Lengo kuu la kutengwa kwa vyama hivi ni kwamba vionekane ni vyama vya kihuni visivyoungwa mkono na shirikisho la vyama vya wafanyakazi ili wanachama wanaojiunga navyo wakose imani navyo ili vife,” amesema.

Amesema miongoni mwa masharti yaliyowekwa ya kujiunga kwenye shirikisho lililopo ni lazima chama kinachotaka kujiunga kiwe kinakata ada ya asilimia 2 kwa wanachama wake akidai sheria haisemi hivyo.

“Sheria imetoa uhuru kwa vyama kupanga ada za kutoza wanachama wake kulingana na vipato vyao na hali ya kiuchumi, sharti jingine ni lazima chama hicho kinachotaka kujiunga kwenye shirikisho hilo kisiwe chama pinzani wa chama chochote kilichopo kwenye shirikisho na hapa ndipo shida inaanzia.

“Mfano kama chama kinajihusisha na wafanyakazi walimu ndani ya shirikisho, kusiwepo na chama kingine cha wafanyakazi walimu ndipo uruhusiwe kujiunga humo, wakati sheria imeruhusu kuwa na chama zaidi ya kimoja katika sekta moja au mahala pa kazi ili kuongeza uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wanachama na kuwapa wafanyakazi uhuru wa chama kipi wajiunge nacho,” amesema.

Katibu Mkuu wa Tawuta, Boaz Nyakeke amesema hata chama chake hakijapata mwaliko akidai ndiyo sababu ya vyama hivyo 19 kubaguliwa.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambacho kipo Tucta, Leah Ulaya amesema jukumu ya kushiriki katika sikukuu hiyo ni la chama au shirikisho husika, hivyo kuwataka wafanye maandalizi vizuri ili nao washiriki kwa sababu ni haki yao.



New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Kimsingi, hakuna mtu anayebaguliwa lakini hawajataka tu kushiriki kwa sababu kama hawapo Tucta wanatarajia wapate wapi taarifa ya kushiriki? Kama wao ni shirikisho na linatambulika na Serikali, wajiandae kwa sababu kushiriki ni namna wewe ulivyojiandaa, hakuna mtu atakayekukataza,” amesema Ulaya.

Mwenyekiti wa Raawu, Jane Mihanji amedai hoja ya kwamba hawashirikishwi haina mashiko kwani maandalizi na shughuli hiyo husimamiwa na ofisi ya mkuu wa mkoa na hakuna anaye kataliwa kushiriki.

“Shughuli hii ni huru na kama kuna kikundi sio mwanachama wetu hawezi kujua nini tunapanga, lakini hii haimwondolei kushiriki kwa sababu na wao wana chama au muungano wao na isitoshe shughuli hii inasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Mkoa wa Arusha na kwenye maandalizi wote wanahusishwa sasa, kwa hiyo hoja ya kwamba hawashirikishwi haina mashiko,” amesema Mihanji.

Imeandikwa na Saada Amir, Janeth Mushi na Anania Kajuni.