Vyuo vikuu vyaunga mkono ujenzi elimu ya kidijitali Tanzania
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimeunga mkono wizara ya elimu kuimarisha safari ya elimu ya kidijitali nchini Tanzania kwa kukabidhi jumla ya kompyuta 55 kwa shule tano za msingi zilizopo jirani na chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Shughuli hiyo iliyofanyika tarehe 23 Agosti 2025, ilitekelezwa kupitia mradi wa VLIR-UOS kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Hasselt cha Ubelgiji, ikiwa ni hatua ya hivi karibuni kutoka taasisi za elimu ya juu kusaidia jitihada za serikali za kuingiza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ngazi zote za elimu.
Shule zilizonufaika ni; Makongo, Mugabe, Msewe, Mapambano na Shule ya Msingi ya Buguruni ya Viziwi, ambazo sasa zitakuwa na vifaa vya kompyuta kwa ajili ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Mpango wa taifa wa elimu ya kidijitali
Mchango huu unakuja wakati ambapo serikali imekuwa ikitekeleza mpango maalumu wa kupunguza pengo la kidijitali katika elimu.
Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesambaza maelfu ya kompyuta katika shule za sekondari kote nchini, kwa lengo la kufanya TEHAMA kuwa sehemu ya lazima katika mtaala wa masomo.
Hii ni sehemu ya mpango mpana wa ‘Digital Tanzania’ unaolenga kuimarisha upatikanaji wa miundombinu ya kidijitali, ujuzi na huduma kwa wananchi wote.
Mpango huu wa kidijitali umesisitiza umuhimu wa ushirikiano. Vyuo vikuu, wadau binafsi na mashirika ya kimataifa wanahitajika zaidi kutoa msaada wa kitaalamu, mafunzo na miundombinu ili kukamilisha jitihada za serikali.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika kampasi ya ARU jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Evaristo Liwa, amesisitiza dhamira ya chuo kufanya TEHAMA kuwa nyenzo ya mageuzi katika elimu.
“Jitihada hizi ni za kuwaandaa vijana wa baadaye,” amesema Profesa Liwa.
“Tunataka walimu na wanafunzi waweze kutumia TEHAMA kwa kujiamini kama chachu ya mabadiliko katika sekta ya elimu.”
Ameongeza: “Zaidi ya walimu wakuu 80 na wasaidizi wao tayari wamepatiwa mafunzo na ARU juu ya matumizi ya kompyuta na vifaa vinavyohusiana.
Utaratibu huu utaleta mabadiliko makubwa katika jamii kwa kuwa kizazi cha sasa lazima kiwe na uwezo wa kutatua changamoto za kesho kupitia TEHAMA.”
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya ARU, UHasselt na Serikali ya Ubelgiji sio tu kuhusu kukabidhi vifaa, bali pia kujenga suluhu za muda mrefu kwa maendeleo endelevu.
Kwa Shule ya Msingi ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikio -Buguruni, iliyopokea kompyuta 15, msaada huo umefika kwa wakati muafaka.
Shule hiyo inahudumia watoto wenye ulemavu wa kusikia, ambapo ufundishaji umekuwa ukitegemea zaidi mbinu za kuona.
“Kompyuta hizi zitatupa urahisi mkubwa katika kufundisha,” alisema Naibu Mwalimu Mkuu, Mwalimu Chris Kweka. “Wanafunzi wetu hujifunza haraka wanapoona taarifa. Kompyuta hizi zitaokoa muda na kutuwezesha kutumia maudhui ya kielektroniki yanayokidhi mahitaji yao. Hii italeta mageuzi makubwa katika namna tunavyofundisha.”
Walimu kutoka shule nyingine pia wametoa maoni chanya. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makongo, Magdalena Nachunga, amesema msaada huo ni wa wakati muafaka huku shule zikianza kutekeleza mtaala mpya unaosisitiza ujuzi wa TEHAMA.
“Vifaa hivi vitatusaidia katika shughuli za kila siku kama vile kutunza kumbukumbu na pia kufanya masomo yawe ya kuvutia zaidi kwa wanafunzi wetu,” amesema.
Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika, bado inakabiliwa na changamoto ya kufuta pengo la kidijitali.
Wakati shule za mijini zikinufaika na miundombinu bora ikiwemo vifaa vya TEHAMA, shule nyingi za vijijini bado hazina rasilimali hizo muhimu.
Wataalamu wanasema ushirikiano kama huu wa ARU na washirika wake ni muhimu kuhakikisha usawa katika elimu.
Mshauri huru wa TEHAMA katika elimu, Dkt. Amana Mwalimu, alisema vyuo vikuu vina nafasi ya kipekee katika mabadiliko haya.
“Taasisi za elimu ya juu ndizo vituo vya utafiti, ubunifu na mafunzo. Ushiriki wao katika kupeleka TEHAMA mashuleni unamaanisha suluhu zitakuwa na ushahidi wa kitaalamu na endelevu,
Ushirikiano huu kati ya serikali, vyuo vikuu na washirika wa kimataifa ndio hasa unaohitajika kuharakisha ajenda ya elimu ya kidijitali Tanzania inafanikiwa,” amesema.
Mbali na kugawa kompyuta, ARU pia inawekeza katika kuwajengea walimu uwezo wa kutumia TEHAMA kwa ufanisi. Chuo hicho kinasema kuwa vifaa bila mafunzo huenda visitumike ipasavyo.
Kwa kuwafundisha walimu wakuu na wasaidizi wao, ARU inalenga kuanzisha mnyororo wa mabadiliko utakaosaidia TEHAMA kuingia moja kwa moja katika madarasa na kunufaisha wananfunzi.
Mradi wa VLIR-UOS pia unalenga kuzalisha tafiti na kuendeleza zana za ubunifu kwa maendeleo jumuishi na endelevu katika maeneo ya mijini nchini Tanzania, hivyo kuunga mkono dhamira ya serikali ya kutumia Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Ubunifu (STEM) kuchochea maendeleo ya taifa.
Prof Liwa amebaini kuwa: “Hatuwezi kuzungumza kuhusu elimu bora katika karne ya 21 bila TEHAMA. Kuwaandaa wanafunzi wetu kwa dunia ya kidijitali si chaguo-ni wajibu.”