Waamini Katoliki wataka mjadala wa wazi mkataba wa bandari

Muktasari:
- Baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kutoa tamko la kutokuunga mkono mkataba wa bandari juzi, leo limesomwa katika makanisa yote ya Kikatoliki nchini huku baadhi ya waumini wakitaka mjadala wa wazi kuhusu mkataba huo na wengine wakitoa maoni kuwa TEC imefanya haraka kuja na waraka huo.
Mikoani. Waumini wa Kanisa Katoliki nchini wameunga mkono tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), huku wakisema kuna haja ya kuwapo kwa mjadala wa wazi utakaojadili Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai (IGA) kabla ya kuridhiwa utekelezaji wake.
Wakati wengine wakisema hayo, baadhi ya waamini hao pia wamesema TEC imefanya haraka kutoa waraka huo unaopinga wakidai tayari suala hilo linaendelea kujadiliwa hivyo wangesubiri msimamo wa Serikali.
Waumini hao wametoa maoni yao leo Agosti 20, 2023 katika mahojiano na waandishi wa Mwananchi baada ya kumalizika kwa Misa za Jumapili katika makanisa mbalimbali ya Kikatoliki nchini.
Parokia ya Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi ni miongoni mwa ulikosomwa waraka huo katika Misa ya Jumapili iliyoongozwa na Paroko wa parokia hiyo, Evans Mavumilio.
Akizungumza na Mwananchi baada ya misa ya kwanza kanisani hapo, Agripina Swai Mkazi wa Majengo kwa Mtei, ameiomba Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo yaliyotolewa kwenye waraka huo.
“Tunaomba Serikali isikilize maoni ya wananchi, wao wanaelewa kuwa madhara yatakayokuwepo baadaye ni nini lakini pia iwasikilize Maaskofu, wakae pamoja wafikie maridhiano, maana baadaye kunaweza kuja kuwa na madhara makubwa ya mvutano wa huku na huku na kukishakuwa na mvutano amani itatoweka,” alisema Swai.
Muumini mwingine mkazi wa Rau, Sabini Kilawe, amesema anaungana na Maaskofu kupinga mkataba huo na kwamba, tangu miaka zaidi ya 60 ya uhuru imepita nchi inao uwezo wa kujitegemea yenyewe.
Waumini wa Kanisa la Mtakatifu Agustino Mkolani lililopo jijini Mwanza wao wameiomba Serikali kuupitia na kuangalia upya mkataba huo kwa kuzingatia maoni ya watu mbalimbali kwa mustakabali wa taifa.
“Kwa hapa tulipofikia, tunapaswa kuangalia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla, lazima wananchi washirikishwe kwenye kila hatua ya maendeleo yanayofanywa na serikali ikiwa ni pamoja nah ii mikataba kwa kuzingatia maoni yao kabla ya kufanyika uamuzi," amesema John Madama mkazi wa kata ya Buhongwa na muumini katika parokia hiyo.
Waumini wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jijini Dodoma wameunga mkono waraka huo baada ya Padri Michael Msamila aliyeongoza misa ya kwanza kuwasomea waraka huo.
Muumini Mariam Petro amesema TEC haiwezi kutoa tamko bila kujiridhisha na sintofahamu zilizoko kwenye mkataba huo, ndiyo maana wamekuja na waraka huo..
"Baada ya waraka huu kusomwa mbele yetu, hata mimi siwezi kuunga mkono ubinafsishwaji wa bandari yetu kwa sababu mkataba huo umejaa vipengele vya kuwanyonya wananchi na kupora mapato yetu badala ya kutupatia mapato zaidi," amesema Mariam.
Romanus Rutagwa amesema tamko hilo limekuja wakati mwafaka kwa sababu Baraza hilo limeeleza jinsi lilivyousoma kipengele kwa kipengele na kubaini kasoro zilizowafanya maaskofu kutouunga mkono.
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Birika Maria Malkia wa Rozali Takatifu mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Padri Aristarki Tarimo amesoma tamko hilo na waumini wameliunga mkono kwa isahara ya makofi na vigelegele.
Mmoja wa waamini wa kanisa hilo kutokea mkoani Manyara, Gift Thadey amesema tamko hilo linawajengea uwezo zaidi Watanzania wa kuwa na uelewa mpana juu ya mkataba huo wa bandari.
"Kila mmoja wetu ana maslahi na rasilimali za nchi ikiwemo bandari, hivyo TEC wamefanya jambo sahihi kutoa tamko kwa lengo la kuwajengea uelewa zaidi Watanzania juu ya mkataba huo," amesema Thadey.
Baada ya misa kunalizika katika Kanisa la Mtakatifu Patrick Vwawa wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe iliyoongozwa na Padri Frank Msungwe, baadhi ya waumini waliozungumza na Mwananchi wameiomba Serikali kuupitia upya na kufanya marekebisha kwenye mkataba mkataba huo.
Rosemary Msyete amesema inaonyesha maaskofu wamebaini kasoro nyingi ndiyo maana wamekuja na waraka huo.
"Suala la uwekezaji ni zuri lakini yawezekana kuna baadhi ya vifungu kwenye mkataba huo vina athari kwa Taifa basi viondolewe kisha uwekezaji uendelee," amesema.
Watoa angalizo
Elisha Haonga amesema katika suala hilo Kanisa limefanya haraka kujiingiza na kuchukua hatua iliyochukua.
"Licha ya kuwa Kanisa kama taasisi isingekaa kimya, lakini TEC inayo nafasi ya kumuona Rais moja kwa moja kuliko mkanganyiko huu ambao binafsi naona kama tunataka kuingia,” amesema Elisha.
Nako mkoani Tanga, Mwananchi lilizungumza na baadhi ya waumini wa Parokia ya Mtakatifu Petro iliyoko eneo la Saruji Pongwe.
Akizungumzia hilo, Mosses Alex anayeishi Chumbageni jijini humo amesema kabla ya kuutoa kwa waumini waraka huo, viongozi hao wa dini walistahili kuomba kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kushauriana naye ili kuepuka kuligawa Taifa.
Alisema anahofu kama hiki kilichofanyika ni sahihi; “Sisi ni wakatoliki, sijui wenzetu nao watasema nini. Lakini hata hii njia iliyotumika kuusoma makanisani si dhani kama ni nzuri nahisi kama inakwenda kutugawa.”
Naye Spelansia Komba amesema; "Tumeusikia kwa makini waraka wa maaskofu wetu uliosomwa hapa kanisani, tumeuelewa na tunauunga mkono, naiomba Serikali iufanyie kazi.”
Bernard Swai amesema ni vyema Serikali ikasikiliza ushauri uliotolewa katika waraka huo kwa sababu madhehebu ya dini yanasikilizwa na huo ndiyo msimamo wa wakatoliki nchini.
Imeandikwa na Anania Kajuni (Mwanza) Joseph Lyimo (Mirerani) Rachel Chibwete (Dodoma) Janeth Joseph (Moshi) Stephano Simbeye (Songwe) Burhan Yakub (Tanga).