Waandishi wa habari waaswa kufanya kazi kwa weledi

  • Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu(THRDC),Onesmo Ole Ngurumwa akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii mjini Morogoro leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini(THRDC) umesema wakati wadau mbalimbali wakiendelea kupigania mabadiliko ya sheria zinazokandamiza uhuru wa kujieleza kwa njia ya mitandao, waandishi wa habari wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.

Morogoro. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini(THRDC) umesema wakati wadau mbalimbali wakiendelea kupigania mabadiliko ya sheria zinazokandamiza uhuru wa kujieleza kwanjia ya mitandao,waandishi wa habari wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.


Mratibu wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa amesema hayo leo jumatatu Mei 10, 2021 wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wanaoendesha  mitandao ya kijamii  umuhimu wa kuzifahamu sheria zinazosimamia uendeshaji wa mitandao hiyo na kuandika habari zinazohusu haki za binadamu.

Amesema uhuru wa kijieleza kupitia vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii  unaelezwa kwenye sheria  na unapaswa kutetewa na kulindwa licha ya changamoto zinazoikabili kwa kutungiwa sheria na kanuni kugandamiza uhuru huo.


“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo waendeshaji wa vyombo vya habari vya kwenye mitandao ili kuzifahamu sheria na kanuni zake ili kuepuka kuingia kwenye utata na vyombo vya sheria  wakati tukipigania mabadiliko ya sheria zinazominya uhuru wa kujieleza,” amesema Ole ngurumwa.


Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT), Kajubi Mukajanga amesema mabadiliko ya sheria ndio utakua msingi wa haki kupatikana na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) iliiagiza serikali ya Tanzania kubadilisha sheria zinazokinzana na haki za kujieleza.


“Hivi karibuni tulimsikia Rais Samia Suluhu Hassan akiagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe na elimu zaidi itolewe kwa waendeshaji wa mitandao ya kijamii kuwa haitoshi bila kubadilisha sheria na kanuni kandamizi,”amesema Mukajanga.


Amesema matumizi ya utoaji habari kwanjia ya mtandao yanapaswa kuzingatia weledi na kusimamiwa vizuri wanataaluma wenyewe kwasababu zinafikia wananchi wengi kwa muda mfupi .