Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waandishi wa tanzu za Kiswahili watwaa Tuzo ya Safal ya Fasihi ya Afrika

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma akikabidhi mfano wa hundi kwa mshindi wa kwanza katika kipengele cha Riwaya cha Tuzo ya Safal ya Kiswahili ya Fasihi Afrika 2025 Salim Hussein Ng’azi huku wageni wengine pamoja na viongozi wa Safal Group wakishuhudia katika hafla iliyofanyika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).

Muktasari:

  • Tuzo hizo zilizofanyika kwa mara ya 10 tangu kuanzishwa kwake, zimewakutanisha waandishi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika

Dar es Salaam. Waandishi wa Kiswahili wameendelea kupata jukwaa la kutambuliwa na kukuza kazi zao baada ya washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kutangazwa katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, huku wadau wakisisitiza nafasi ya lugha hiyo katika kuimarisha fasihi na utamaduni wa Afrika.

Tuzo hizo zilizofanyika kwa mara ya 10 tangu kuanzishwa kwake, zimewakutanisha waandishi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, huku jumla ya miswada 230 kutoka nchi saba ikiwasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo za mwaka huu.

Akizungumza katika hafla hiyo hivi karibuni, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar,  Riziki Pembe Juma  ameipongeza Kampuni ya Safal Group kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills ya Kenya na Alaf Limited Tanzania, kwa kudhamini  tuzo hizo kwa miaka 10, akisema zimechangia kukuza Kiswahili na kuibua vipaji vya waandishi wa Afrika.

Riziki akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema: “Hii ni namna bora ya kukuza lugha ya Kiswahili hapa Tanzania na nchi za nje kama tunavyofahamu, Kiswahili kwa sasa kinazungumzwa kote duniani ikiwamo nchi za ng’ambo ambako baadhi ya Watanzania wameajiriwa ili wafundishe lugha hii.”

Amesema Serikali itaendelea kutangaza Kiswahili na kuhakikisha kinatumika huku akiandaa matukio mbalimbali yanayolenga matumizi ya lugha hiyo.

 “Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na taasisi zingine zinazohimiza matumizi ya lugha hii ya Kiswahili,” amesema.

Pia, amewapongeza washindi wa mwaka huu na kuwahimiza kutumia vipaji vyao vya uandishi kujiendeleza na kuhakikisha pia wanajiingizia kipato kwa kuuza machapisho yao duniani kote.

Washindi kwa mwaka huu wametangazwa katika vipengele vitatu vya uandishi, huku waandishi kutoka Tanzania na Kenya wakitwaa tuzo hizo.

Katika kipengele cha riwaya, mshindi wa kwanza ni Salim Hussein Ng’azi kutoka Tanzania kwa kazi yake ya ‘Mwanamkasi ndio basi,’ aliyepokea zawadi ya Dola 5,000 za Marekani (Sh13 milioni) huku Dickson Damas Mtalaze akishika nafasi ya pili kwa riwaya yake  ya ‘Shamba la mawe’ na kujinyakulia Dola 2,500 za Marekani (Sh6.5 milioni).

Kwa upande wa ushairi, Ali Hilal Ali kutoka Tanzania ameibuka mshindi wa kwanza kwa kazi yake ‘Diwani ya vizikwa ya kale’ na kupata Dola 5,000 za Marekani wakati Leonard Barnaba Mtesigwa akishika nafasi ya pili kupitia ‘Rima la miiko la balaa,’ akipokea Dola 2,500 za Marekani.

Katika kipengele cha hadithi fupi, Dominic Maina Oigo kutoka Kenya ameibuka mshindi kwa kazi yake ya ‘Mbunge mtarajiwa na hadithi nyingine’ na kutunukiwa Dola 2,500 za Marekani.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Alaf Limited, Bibhu Nanda amesema kampuni hiyo imeendelea kudhamini tuzo hiyo kwa miaka 10 kutokana na umuhimu wa Kiswahili katika kuunganisha jamii mbalimbali, si tu Afrika Mashariki bali pia watu kutoka sehemu tofauti duniani.

“Tukiwa tunaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa tuzo hii, tunapenda kuwashukuru wabia wetu wote ambao wamesimama na sisi katika kipindi hiki chote kwa lengo la kukuza na kutangaza lugha ya Kiswahili,” amesema Nanda.

Tuzo hiyo  ilianzishwa mwaka 2014 na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma wa Ngugi  ili kutambua kazi za uandishi katika lugha za Kiafrika na kuhamasisha kazi za utafsiri kwa lugha adhimu za asili ya Kiafrika.

Akizungumzia tuzo hizo, Dk Attree amesema miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ni hatua kubwa.

"Tayari tumeshatoa zaidi ya Dola 150,000 kwa waandishi zaidi ya 40 mchango ambao umewawezesha kuchapisha zaidi ya vitabu 20. Ni matumaini yetu kuwa lugha za Kiafrika zitaendelea kutambuliwa kwa njia hii na kwamba kazi hii inaendelea kuikuza fasihi ya Kiswahili duniani."

Dk Mukoma wa Ngugi ameelezea kuhusu mfumo wa uchapishaji unaohusiana na fasihi ya Kiswahili kwa kipindi cha mwongo mmoja, akisema umewaunganisha waandishi walioshinda tuzo mbalimbali moja kwa moja na wachapishaji wakiwamo Mkuki na Nyota na Mfuko wa Vitabu vya Ushairi wa Kiafrika (APBF).

"Tunashukuru uongozi wa Kampuni ya Safal, ambayo imetoa mchango mkubwa unaokuza tamaduni za Kiafrika. Tunatoa wito kwa Serikali mbalimbali barani Afrika, kupitia wizara zao za utamaduni kuunda mfumo ikolojia utakaohusisha lugha zote za Kiafrika."

Mwenyekiti wa jopo la majaji wa tuzo hizo, Profesa Rayya Timammy kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya   amesema ushindani wa tuzo hizo ulikuwa mkubwa.

Amesema hali hiyo imesababishwa na idadi kubwa ya mawasilisho yaliyopokewa kuwa na vipaji vya hali ya juu na kipekee vilivyooneshwa na waandishi waliowasilisha kazi zao.

"Jopo la majaji lilikabiliwa na changamoto kubwa katika kuchagua washindi kwa sababu ya ubora wa kazi zilizowasilishwa. Bila shaka hii inaonesha kwamba, vipaji vya fasihi vinaendelea kukua na kushamiri kwa kasi ya ajabu," amesema Profesa Timammy.

Mkurugenzi wa tuzo hizo, Munyao Kilolo amesema ukuaji huo umeendelea kukua kwa kipindi chote cha miaka 10 iliyopita.

 "Mwanzoni tulikuwa tukipokea mawasilisho chini ya 50 kwa mwaka, sasa hivi tunapokea mamia ya mawasilisho kila mwaka," amesema.

Kilolo amesema ukuaji huo umeenda sambamba na kukua kwa  jumuiya ya waandishi ambao mbali na kupata zawadi, wanashirikiana katika kukuza fasihi ya Kiswahili.

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya tuzo hiyo, Abdilatif Abdalla amesema: “Ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 2015, bado tuzo hii inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia, kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, na kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”