Wabunge Mbeya wabainisha mafanikio miaka miwili ya Rais Samia

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi, Meryprisca Mahundi akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye siku ya kumpongeza Rais Samia Suluhu kutimiza miaka miwili ya uongozi wake. Picha na Hawa Mathias

Mbeya. Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Meryprisca Mahundi amesema wanawake ndani ya chama wamejipanga kuhakikisha uchaguzi Mkuu 2025 wanavunja rekodi za kumpigia kura za kishindo Rais Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Mahundi amesema leo Jumamosi, Machi 18, 2023 katika siku maalumu ya kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili ya uongozi wake.

Mhandisi Mahundi ambaye ni mbunge viti maalumu Mkoa wa Mbeya amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi ikiwepo kumtua mama ndoo kichwani kwa kuboresha huduma za maji mijini na vjjijini.

“Tumeona mambo mengi yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita ikiwepo kuboresha kwa miradi mikubwa ya maji ikiwa ni juhudi za kumtua mama ndoo kichwani hivyo kama wanawake wanalojukumu la kumlipa mwaka 2025,”amesema.

Ameongeza kuwa licha ya miradi ya maji pia Serikali imeboresha upatikanaji wa huduma mbali mbali ikiwepo afya, elimu na miundombinu ya barabara jambo ambalo limerahisisha shughuli za kiuchumi kwa jamii.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini na Mwenyekiti wa wabunge, Oran Njeza amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza katika shughuli mbalimbali ikiwepo uboreshwaji wa sekta ya kilimo, miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami na kusaidia wakulima kusafirisha mazao kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Amesema kuwa Serikali imetoa Sh11 bilioni kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji katika maeneo ya vijijini ikiwepo Sh35 bilioni kwa ajili ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA).

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega amesema kwa  kipindi cha miaka miwili Serikali imefanya mambo mengi ikiwepo uchimbaji wa mabwawa sita ya kilimo cha umwagiliaji.

Stahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema wamepokea Sh420 milioni kuboresha miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Roleza.