Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge wahoji maiti kuzuiwa hospitali mpaka ndugu walipe fedha, Serikali yajibu

Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Janeth Masaburi akiwashangaa wabunge waliokuwa wakipinga  ufafanuzi wa Waziri Ummy Mwalimu kuhusu utaratibu wa kulipia gharama za matibabu kabla ya kuchukua maiti, wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Utaratibu wa kulipia gharama za matibabu kabla ya ndugu kuchukua maiti leo Ijumaa Septemba 6 2019 umehojiwa na wabunge katika kipindi cha maswali na majibu bungeni mjini Dodoma.


Dodoma. Utaratibu wa kulipia gharama za matibabu kabla ya ndugu kuchukua maiti leo Ijumaa Septemba 6 2019 umehojiwa na wabunge katika kipindi cha maswali na majibu bungeni mjini Dodoma.

Swali kuhusu jambo hilo lilianza kuulizwa na mbunge wa Viti Maalum (Chadema),  Susan Lyimo.

Lyimo amesema Serikali ina utaratibu wa kutoza gharama miili iliyohifadhiwa hospitali jambo alilodai kusababisha simanzi kwa familia zisizokuwa na uwezo wa kulipa.

“Lini Serikali itaacha kutoza gharama miili ya wanaofia hospitali na kuhifadhiwa ili kupunguza simanzi kwa wafiwa,” amesema Lyimo.

Akijibu swali hiyo, naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile amesema miili ya wanaofia hospitali husika au kuletwa kutoka maeneo mbalimbali inatakiwa kuwekwa kwenye majokofu yenye ubaridi na wakati mwingine kuwekwa dawa za kusaidia isiharibike.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2017 wananchi wanapaswa kuchangia gharama za afya ikiwa ni pamoja na matibabu na hata huduma za uhifadhi wa maiti.

“Panapotokea changamoto au mwananchi kushindwa kumudu gharama za afya ikiwa ni pamoja na matibabu na hata huduma za uhifadhi wa maiti, mwananchi huyu anapaswa kutoa taarifa kwenye uongozi wa hospitali husika ili kupata maelekezo ya namna ya kutatua changamoto hiyo,” amesema.

Ili kuondokana na changamoto hizo amewahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa lengo la kupunguza gharama za matibabu toka mfukoni.

Lyimo aliuliza swali la nyongeza, safari hii akitaka kujua utaratibu unaotumika kukabidhi maiti kwa wenye dhida zaidi pamoja na kutaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha asilimia 66 ya wananchi wanajiunga na bima ya afya.

Akijibu swali hilo, Dk Ndungulile amesema hakuna maiti imezuiwa moja kwa moja kwa ndugu kushindwa kulipia gharama za matibabu.

Amesema changamoto hiyo inajitokeza kwenye hospitali mbalimbali hasa  Mloganzila na Muhimbili na kuwataka wanaoshindwa kulipa fidia kufika ofisi ya ustawi wa jamii  kuna utaratibu wataelekezwa wa kufanya ikiwemo kupewa utaratibu wa kulipa kidogo kidogo.Amesema kati ya Juni na Augosti katika Hospitali ya Temeke walitoa msamaha wa  Sh500 milioni.

Hata hivyo, amesema hiyo haiondoi jukumu la ndugu kulipia gharama.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM),  Faida Bakari amesema ni bora ungebadilishwa utaratibu  ili kutoa heshima kwa maiti.

Amesema gharama za kuhifadhi maiti zimekuwa zikiongezeka kila siku na kuhoji maiti za wananchi wanaoshindwa kulipia gharama zinapelekwa wapi. 

Akijibu swali hilo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema watu hawalipii maiti ila wanalipia gharama za matibabu.

Ametoa mfano mgonjwa anapohudumiwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) gharama zake kwa siku ni Sh500,000 na  hospitali binafsi ni Sh2.5 milioni.

Amewataka wabunge badala kulalamika suala hilo wawahimize wananchi wakate huduma za afya.

Majibu hayo yaliwaibua wabunge wengi huku wengine wakinong’ona jambo lililomfanya mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kusema wanaotaka ufafanuzi wamuone Ummy.