Wabunge wataka deni la TPDC lilipwe

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula akiwasilisha bungeni maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jijini Dodoma leo Jumatatu Mei 31, 2023. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Kukukuwa kwa deni la mauzo ya gesi limeiibua Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na kushauri Serikali lilipwe ili kutozorotesha shughuli za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Serikali kulipa deni la Sh720 bilioni mauzo ya gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwenda Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo linaendelea kukuwa.

 Hayo yamesemwa leo Mei 31, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula wakati akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo kuhusu bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/24.

Amesema deni hilo limeongezeka kutoka Sh526 bilioni mwaka 2022/23 na kufikia Sh720 bilioni.

“Kwa kuwa licha ya ushauri wa mara kwa mara wa Kamati wa deni hili kulipwa hali inayozoretesha utendaji kazi wa TPDC, Kamati inashauri mwaka huu wa fedha 2023/2024 deni hili lote lilipwe,”amesema.

Aidha, amesema kumekuwa na utaratibu usiofaa wa baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa ankara za umeme hali ambayo imepelekea deni kufikia Sh334.8 bilioni.

 “Kwa mara nyingine Kamati inashauri hatua za makusudi zichukuliwe ili deni hili lilipwe kabla ya mwaka ujao wa Fedha 2023/2024 kuisha,” amesema.

Kuhusu nishati mbadala, Kitandula amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na wizara na Serikali katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia, Serikali katika mipango yake iwezeshe matumizi ya majiko ya umeme yenye presha (pressure cookers) zinazotumia umeme kidogo.

Pia iwezeshe mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe (Rafiki Coal Briquette) ambao umethibitishwa kutokuwa na hewa/kemikali zinazosababisha uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya za watumiaji.

“Serikali ione namna ya kupunguza kodi za uingizwaji wa majiko ya umeme yenye presha,”amesema.