Uchambuzi wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/22

Muktasari:

  • Bajeti za Wizara ya Madini (MoM) kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2020/21, pamoja na mambo mengine, zina sifa zifuatazo; kiasi kidogo cha fedha zinazotolewa kulinganisha na kiasi kilichotengwa, upungufu wa uwezo (ufanisi) wa kisera au kitaasisi katika kuhimiza na kuwezesha mazingira ya uwazi na uwajibikaji, ulegevu na uhusiano dhaifu wa; sera, sheria, miongozo na maelekezo yasiyotabirika unaathiri utekelezaji wa vipaumbele vya wizara.

Utangulizi

Bajeti za Wizara ya Madini (MoM) kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2020/21, pamoja na mambo mengine, zina sifa zifuatazo; kiasi kidogo cha fedha zinazotolewa kulinganisha na kiasi kilichotengwa, upungufu wa uwezo (ufanisi) wa kisera au kitaasisi katika kuhimiza na kuwezesha mazingira ya uwazi na uwajibikaji, ulegevu na uhusiano dhaifu wa; sera, sheria, miongozo na maelekezo yasiyotabirika unaathiri utekelezaji wa vipaumbele vya wizara.

Ni kutokana na changamoto hizo zilizotajwa, jumuiko la asasi za kiraia, HakiRasilimali imekuwa na utamaduni wa kuchambua bajeti za wizara hii kwa lengo la kufuatilia, kubaini undani, uhalisia na mwenendo wake ili kujifunza na kuibua masuala yanayoweza kujadiliwa ili hatimae nchi iwe na bajeti yenye vipaumbele vinavyotekelezeka, mgawanyo mzuri wa fedha hasa kwa miradi ya maendeleo, ushiriki na uimarishaji wa uwezo.

Uchambuzi wa bajeti ya mwaka 2021/2022 umejikita zaidi katika maeneo machache ya kisera, ikiwemo; ukusanyaji wa mapato na mchango wa sekta kwenye pato la Taifa (GDP), Urasimishaji wa Wachimbaji wadogo, Mazingira ya Uwekezaji, Ushiriki na Uwezeshaji wa Wazawa, Jinsia na Ukuaji Shirikishi.

Mwenendo wa bajeti ya sekta ya uziduaji: Makusanyo ya mapato, utengwaji wa fedha na matumizia)

Kiasi kilichotengwa, kilichopatikana na kilivyotumika: Katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali ya Tanzania ilitenga kiasi cha shilingi 12.8 trilioni, sawa na asilimia 37 ya bajeti kuu ya serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wizara zake mbalimbali.

Katika fedha hizo, shilingi 4.7 trilioni, sawa na asilimia 36.7, zilitoka katika vyanzo mbalimabli kwa mchanganuo ufuatao; shilingi 3.4 trilioni kuto-ka vyanzo vya ndani na shilingi 1.3 trilioni kutoka vyanzo vya nje.

Katika utekelezaji wake, bajeti ya Wizara ya Madini ilitumia fedha hizo za miradi ya maendeleo katika; Uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini na mradi wa uchenjuaji uliopo jiji la Mwanza, Maboresho na marekebisho ya sheria ili kuvutia wawekezaji (kuzaliwa kwa Twiga, Tembo na masoko 39) na Kuendeleza mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma-Liganga.

b) Ukusanyaji wa mapato ya Wizara ya Madini, kiwango kinachotengwa na kiwango kinachotolewa:

Mwaka wa fedha, 2020/21, wizara ilikadiria kukusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo mrabaha na tozo yanayofikia shilingi 547,735,863,567. Kufikia Februari 2021, jumla ya shilingi 399, 352, 335,099 (sawa na asilimia 113.73) zilikuwa zimekusanya na kuwasilishwa Hazina. Katika mwaka wa fedha 2021/22, kiasi cha shilingi 696,441,872,667 kinakadiri wa kukusanywa sawa na ongezeko la shilingi bilioni 148,706,009,070 kulinganisha na mapato ya mwaka 2020/2021.

Mwaka huo wa 2020/21 Bunge letu liliidhinisha kiasi cha shilingi 62,781,586,000 (bilioni 62.8) kwa ajili ya wizara ya madini, ambapo asilimia 13.54 (sawa na shilingi bilioni 8.) zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na asilimia 86.64 (sawa na shilingi bilioni 54.3) zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Hata hivyo, kufikia Februari mwaka 2021, ni asilimia 21.5 tu (sawa na shilingi bilioni 1.22) ya fedha za miradi ya maendeleo ndiyo ilikuwa imetolewa kwa ajili ya matumizi kupitia mradi wa “Sustainable Management of Mineral Resources Project (SMMRP)”.

Katika mwaka wa fedha wa 2021/22, wizara imepanga kutumia bajeti ya shilingi 68,541,467,000 (shilingi bilioni 68.5) ambapo shilingi bilioni 51.8 zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida (ikiwamo mishahara) huku shilingi bilioni 16.7 ambayo ni sawa na asilimia 24.40 ikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayohusiana na STAMICO, GST, Kamisheni ya Madini, Wizara (shilingi bilioni 15 kutoka vyanzo vya nje) na TEITI (shilingi 1,725,000,000 kutoka vyan-zo vya nje).Matokeo ya Uchambuzia) HakiRasilimali inaipongeza wizara kwa kazi kubwa iliyofanya mwaka 2020/21 na pia kwa kuongeza fedha (kwenye bajeti yake) kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2021/22. Hata hivyo, HakiRasilimali imebaini changamoto kwenye; mwenendo wa makusanyo, utengwaji wa mafungu na matumizi ya mapato kulinganisha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kama ifuatavyo;

b) Kuna kiasi kidogo kinachotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kulinganisha na kiasi kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Wakati mapato ya wizara yamekuwa yakiongezeka kila mwaka, kwa miaka mitano mfululizo, fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zimekuwa kidogo kulinganisha na ongezeko la mapato. Ilitarajiwa ongezeko la pato liongeze kiasi cha fedha kwenye miradi ya maendeleo.

c) Utekelezwaji wa miradi Isiyo vipaumbele vya wizara: Katika mwaka wa fedha 2020/21, (Julai mpaka Februari), wizara imetekeleza miradi ambayo haiendani na vipaumbele vilivyowekwa na wizara katika mwaka huu. Wizara kupitia mradi wa SMMRP ilikuwa imepanga kununua magari kwa ajili ya kazi za utafiti na utafutaji madini, ujenzi wa kituo cha ubobezi wa masuala ya madini, kituo cha msaada kwa wachimbaji wadogo wa madini, uendelezaji wa mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira na mambo mengine.

Hata hivyo, wizara ilitekeleza miradi kama vile ujenzi wa barabara, ununuzi wa vifaa vya tehama kwa ajili ya ulinzi wa mgodi wa Mererani na ujenzi wa vituo ubobezi (centers of exellency) wa madini katika Wilaya za Songea, Chunya na Mpanda.

Miradi hii ilitekelezwa bila kuwepo kwenye bajeti na hivyo haikuwa kwenye orodha ya vipaumbele vya wizara. Bajeti haisemi chochote kuhusu miradi ambayo ilikuwa imepangwa lakini haikutelezwa.

d) HakiRasilimali imebaini kwamba miradi iliyotekelezwa ilikuwa imepangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 na hivyo ina maana utekelezaji wake ulisogezwa mbele. Hata hivyo, jambo hili halijawekwa bayana na wizara na hivyo kuleta changamoto za kihasibu kuhusu utekelezwaji wake.

Mapendekezo:

a) Ili kutekeleza ipasavyo miradi ya maendeleo katika wizara, kunahitajika uwepo wa chanzo cha kimkakati cha mapato ili kuweza kusaidia kwa uhakika utekelezwaji wa miradi hiyo kama ilivyopangwa na wizara.

b) Tunaiomba wizara kuhakikisha kwamba kunakuwa na taratibu za kihasibu kuonyesha utekelezaji wa miradi iliyobebwa kutoka mwaka uliopita wa fedha ili kurahisisha ubaini wa miradi halisi iliyotekelezwa na bajeti ya wizara kwenye mwaka husika wa fedha. Hii itasaidia pia taasisi zingine za umma kuona utekelezaji kwa uwazi na hivyo kushauri kirahisi zaidi.

2: Ukuaji na mchango wa sekta ya madini nchini Tanzania

Vitabu vya bajeti vya wizara kwa mwaka wa fedha 2021/22 vinaonyesha kwamba sekta ilikua kwa asilimia 17.7 mwaka 2019. Pia, vitabu hivyo vinaonyesha kwamba mchango wa sekta kwenye GDP umeongezeka kutoka asilimia 4.8 mwaka 2017 hadi asilimia 5.2 mwaka 2019. Hata hivyo, uchambuzi wetu unaonyesha kwamba mchango wa sekta kwenye GDP bado ni mdogo ukikua kwa wastani wa asilimia moja tu pamoja na ongezeko hilo la makusanyo na ukuaji wa sekta.

Changamoto:

  1. Mchango wa sekta kwenye GDP (lengo ni asilimia 10):

Mpaka sasa mchango wa sekta ya madini ni asilimia tano. Kiwango hiki kimefikiwa kukiwa na ongezeko kubwa la mapato na ukuaji wa jumla wa sekta. Wizara inahitaji jitihada maradufu ili kufikia lengo la Dira ya Taifa (Vision 2025, ambayo inalenga kuona mchango wa sekta hii ukifikia asilimia 10 kwenye zao la Taifa (GDP), imebaki miaka minne kutoka sasa ili kufikia lengo hili.

b) COVID 19 kwenye sekta ya madini:

Mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID 19) na athari zake kwenye sekta ya madini (bei na mapato yatokanayo na uzalishaji wa dhahabu na vito)umeathiri utekelezaji wa bajeti za mwaka 2019/2020, 200/21, hivyo ni mjadala katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022. Duniani kote, mwenendo wa uzalishaji wa madini uliathiriwa na COVID19 na Tanzania ilishuhudia kupungua kwa uzalishaji kwa kiwango cha wastani wa asilimia 27.3 kati ya mwishoni mwa mwaka 2019 mpaka mwaka 2020.

Kwa mfano, ripoti za Serikali zinaonyesha kwamba uzalishaji wa dhahabu kati ya mwaka 2019 na 2020 haukuwa tulivu dhahabu ikizalishwa kwa kiwango cha juu Oktoba mwaka 2019 kwa kiwan-go cha gramu milioni 1.5, mwezi Juni 2020 ikifikia kiasi cha gramu milioni 1.3 huku mwezi Juni mwaka 2019 uzalishaji ukiwa wa chini kabisa kufikia gramu 447,861.8.

Ingawa Tanzania haikufunga mipaka yake wala kuzuia watu kutembea wakati wa janga la COV-ID19, wachimbaji wadogo wa madini waliathiriwa sana na janga hilo kutokana na vikwazo vya kusafiri vilivyowekwa kimataifa na uhitaji mdogo wa madi-ni katika nyakati hizo.

Hali hiyo ilisababishwa na ugumu wa wauzaji wa kimataifa kusafiri kwenda kuuza biashara zao nje na wale walio nje kushindwa kusafiri ili kuja nchini Tanzania.

Mapendekezo:

1. Juhudi zielekezwe katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (FYDP III 2021-2025) ili ili kuvutia wawekezaji ikiwamo kufanya mabadiliko ya kimkakati katika utekelezaji wa sera na sheria za madini. Tanzania tunaweza kujifunza kutoka Ghana ambayo mchango wa sekta yao ya madini katika GDP sasa imefikia asilimia 8.1. pamoja na kua Ghana kuna uzoefu wa muda mrefu katika sekta hii.

2. Maendeleo ya taifa na mipango ya bajeti: mitazamo na fursa katika utekelezaji wa sera za kuwawezesha wazawa katika sekta ya uziduaji

Dhana ya uwezeshaji wazawa na ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati ya uwekezaji imekuwa ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Uchumi ya mwaka 2004. Tamko la sera hii ni Kujenga uchumi wa viwanda na kufikia Uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Ripoti za bajeti za wizara na zile za Baraza la Uwezeshaji Uchumi za mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/2021 zinaonyesha kwamba suala la uwezeshaji wazawa limeanza kupata nguvu miongoni mwa taasisi za serikali, kampuni na asasi za kiraia. Hata hivyo, ripoti za kibajeti za mwaka wa fedha 2020/2021 ziko kimya kuhusu hali ya utekelezaji wa dhana yenyewe ya uwezeshaji wa wazawa.

Katika mwaka wa fedha wa 2021/22, Wizara imepanga kutekeleza sheria inayotaka kampuni kubwa za uchimbaji madini nchini kuajiri na kununua huduma na bidhaa kutoka kwa wazawa ili kutimiza matakwa ya sheria ya kuwezesha wazawa (Local Content Act).

Pamoja na hayo, suala la uwezeshaji wa wazawa limeendelea kukumbwa na changamoto zifuatazo;

3.1 Muktadha wa uwezeshaji wazawa sekta ya madini:

Ingawa Tanzania imekuwa na sheria ya masuala ya uwezeshaji wazawa tangu mwaka 2004, hadi sasa hakuna mkakati kamili wa kushajiisha utekelezaji wake. Hakuna uelewa wa pamoja wa nini hasa maana ya uwezeshaji wazawa katika sekta mtambuka za uchumi.

Matokeo yake, kila sekta sasa inatekeleza jambo hilo kwa mujibu wa muktadha au matakwa ya sekta yake. Kwa mfano, katika sekta ya madini, suala hilo limefafanuliwa katika Kanuni ya Madini (Uwezeshaji Wazawa ya mwaka 2018, kama ilivyofanyiwa marekebisho, inayoeleza suala hilo kuwa ni asilimia ya kiasi kilichozalishwa nchini, wafanyakazi walioajiriwa, huduma na bidhaa zilizotolewa katika mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya madini na ambavyo vinavyoweza kupimwa kwa thamani halisi ya fedha.

Maana hii ya uwezeshaji wazawa imeacha kueleza kinagaubaga maana ya mzawa na hivyo imesababisha matarajio yasiyo halisi ya ushiriki wa Watanzania katika sekta.

3.2 Kanuni za sheria ya uwezeshaji uchumi:

Tanzania ilipitisha Sheria ya Uwezeshaji Uchumi tangu mwaka 2004 lakini, hadi sasa, hakuna kanuni zilizotengenezwa kukazia utekelezaji wa sheria hiyo kwa ufanisi na uthabiti ili kufikia malengo.

3.3 Utaratibu wa mrejesho wa taarifa kuhusu dhana ya uwezeshaji wazawa:

Wizara haijatoa taarifa rasmi kuhusu vipaumbele vyake kwenye uwezeshaji wazawa. NEEC na TEITI zinatoa taarifa kuhusu masuala ya ajira, manunuzi ya huduma na bidhaa, misaada kwa jamii, mafunzo na uhaulishaji wa teknolojia.

Hata hivyo, taarifa za namna hazitoshelezi kwa sababu hakuna mkakati unganishi wa utoaji wa taarifa, Ufuatiliaji, Kubaini na Kutathmini utekelezaji wa shughuli zinazolenga Kuwezesha wazawa.

Mapendekezo:

1.Mwelekeo mpya uwezeshaji wazawa: Kuna haja ya kutoa mwelekeo mpya wa suala hili la uwezeshaji wazawa katika muktadha wa uwezo wa nchi kufaidika na sekta za kiuchumi kama uziduaji kwa maana ya upatikanaji wa ajira, uendelezaji utaalamu na ununuzi wa bidhaa na huduma.

2. Uwezeshaji ni eneo muhimu sana katika dhana nzima ya uwezeshaji wazawa. Kwa kutambua hilo na kwa lengo la kutengeneza sheria unganishi ya jambo hilo, HakiRasilimali inapendekeza kufanyiwa kwa mapitio ya Sera na Sheria ya Uwezeshaji ili iwe ndiyo sheria mama ya masuala ya uwezeshaji wazawa nchini Tanzania.

3. Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC) lililoanzishwa kwenye Sheria ya Uwezeshaji linapaswa kufanyiwa marekebisho na kuundwa kama Mamlaka au Kamisheni ili kulipa nguvu zaidi. Kwa namna lilivyo sasa, baraza hili linaonekana kama chombo cha ushauri na si taasisi yenye dhima ya kusukuma mbele na kusimamia kwa utahbiti dhana hii ya uwezeshaji wazawa.

Tanzania inaweza kuiga mfano wa Sierra Leone ambako kuna Wakala kamili anayehusika na utekelezaji wa suala la uwezeshaji wazawa ambalo limefanikiwa sana katika uendelezaji wafanyakazi katika sekta ya uziduaji na kuongeza nguvu ya ushiriki wa wazawa wa taifa katika kufaidika na utajiri wa rasimali zao kwa mujibu wa mipango ya maendeleo iliyowekwa na taifa lao.

4. Kupitia Kamisheni ya Madini na NEEC, Tanzania inatakiwa kuwekeza katika utafiti utakaokuwa na lengo la kubaini ubora na kiasi cha bidhaa na huduma ambazo nchi ina uwezo wa kuilisha sekta ya uziduaji hapa nchini. Majibu ya utafiti huo yatakuwa kama kielelezo cha wingi na ubora wa huduma na bidhaa ambazo Tanzania inaweza kuilisha sekta hiyo katika mnyororo wake mzima wa thamani.

5. Ili kufikia lengo lake la kuwa taifa la uchumi wa viwanda vinavyotokana na madini, Tanzania inahitaji kujenga mazingira wezeshi ya fungamanisho na sekta nyingine zinazoilisha. Hii ni kama vile kuchagiza ukuaji na ongezeko la uwezo wa taasisi kama vyuo vikuu, vyuo vya ufundi, sekta binafsi NEEC n.k. Taasisi hizi hujenga uti wa mgongo wa kijamii na kiuchumi ambao husaidia kuifanya sekta iwe imara.

6. Kuanzisha utaratibu wa kujiandikisha kwa njia ya mtandao kwa watoa huduma wa ndani kwa lengo la kupunguza urasimu na pia kujua na kutathmini uwezo wa ndani wa watoa huduma. Utaratibu huo pia utakuwa kiunganishi kwa watoa huduma wa ndani kuona fursa zilizopo kwao katika soko la madini la ndani.

3.4 Ushiriki wa ndani (DSE, ajira, manunuzi ya bidhaa na huduma):

I) Ajira

Kwa mujibu wa ripoti za MoM, NEEC na TEITI, katika sekta ya madini, idadi ya wazawa walioajiriwa ni 7,967 huku wageni wakiwa ni 158. Ripoti hizi ni katika kipindi cha kati ya mwaka 2019 hadi 2020. Kwa takwimu za mwaka 2018, kiwango kilikuwa ni wazawa 6,623 dhidi ya wageni 140.

Hata hivyo, taarifa za namna hii si toshelezi kwa sababu hazisemi hasa hizo ni ajira za moja kwa moja, vibarua au nyinginezo. Zaidi, taarifa kama hizi hazisemi kitu pia ni aina gani ya kazi zinafanywa na waliotajwa kwa maana ya zile za kitaalamu, za utaalamu wa kazi au zile zisizohitaji ujuzi.

2) Manunuzi ya huduma na bidhaa:

Ripoti za wizara na NEEC kwa miaka ya 2020/21 na 2021/22, hazisemi kitu kuhusu ni aina gani ya bidhaa au huduma ambazo zimenunuliwa au zinatarajiwa kununuliwa kutoka masoko ya ndani katika sekta ya madini. Ni muhimu kuelewa kwamba manunuzi kutoka ndani ni miongoni mwa misingi mikuu ya fungamanisho la uchumi kati ya sekta ya madini na nyingine katika kufikia lengo la uchumi wa viwanda unaochagizwa na madini kama ilivyoaisnishwa kupitia Mpango wa 2025. Miongoni mwa huduma hizo ni kama vile huduma za kisheria, kifedha na chakula.

Inahusu pia matumizi ya bidhaa zinazotumika katika migodi na vifaa vingine kama vile viatu, sare za kazi n.k. Wizara haina kanzidata ya mtandaoni yenye taarifa kuhusu watoa huduma katika sekta ya madini. Kanzidata itaongeza uwezo wa kuonana na utambuzi katika mnyororo mzima wa thamani kwenye sekta.

Manunuzi ya bidhaa na huduma katika sekta ya uziduaji yamezidi kukumbwa na changamoto kadhaa zikiwamo; kushindwa kuwezesha wafanyabiashara wadogo kuwekeza, kiwango cha chini cha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kutokuwapo kwa taarifa za kutosha kuhusu uwezo hasa wa Watanzania kuzalisha huduma na bidhaa zinazohitajika katika migodi (kampuni za madini).

3.4 Kujiandikisha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) –Aina za kampuni za madini zinatakiwa kujiandikisha.

a) Katika utafiti huu, HakiRasilimali imebaini kwamba taarifa za wizara hazisemi kitu kuhusu hali za kampuni za madini ambazo zimejiandikisha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

b) Kifungu cha 126 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 (CAP 123 Revised Edition 2018) kinazitaka kampuni za madini zinazofanya kazi nchini Tanzania kujiandikisha katika soko la hisa (DSE) kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Masoko ya Hisa (Section 109) ili Watanzania waweze kununua hisa na kuwa wamiliki wa kampuni hizo.

Hata hivyo, utaratibu uliotumika katika makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni za Barrick na Kabanga Nickel kwenye kuunda kampuni za TWIGA na TEMBO mtawalia, inaonekana hali ni tofauti. Kampuni hizo mbili zimepewa leseni maalumu za uchimbaji na kwa mujibu wa kanuni mpya za Sheria ya Madini za mwaka 2020, hazilazimiki kujiandikisha katika soko la hisa.

Hii maana yake ni kwamba kampuni hizo na nyingine zitakazokuja baadae kupitia utaratibu huo wa leseni maalumu hazitalazimishwa kuuza hisa zake DSE. Jambo hili linafungua uwezekano mkubwa wa rushwa na mambo mengine kama ukwepaji kodi na utoroshaji nje wa fedha za kigeni.

c) Asili ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini Tanzania haiendani na masharti ya kujiandikisha katika soko la hisa. Ili kampuni ya madini iruhusiwe kuuza hisa zake DSE, inatakiwa iwe imefanya biashara na kupata faida kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Uzoefu wa Tanzania umeonyesha kwamba kampuni zote kubwa zinazofanya kazi nchini zimekuwa zikitangaza kupata hasara hapa lakini faida nchini kwao. Hii ni changamoto kubwa kwa DSE.

Mapendekezo:

1. Zaidi ya kupata asilimia 16 za umiliki za hisa za moja kwa moja kwenye kampuni za madini, Tanzania inaweza pia kuazima maarifa kutoka katika nchi kama Botswana ambayo, ili kufaidika zaidi na utajiri wa maliasilia yake, iliamua kununua hisa zaidi za umiliki katika masoko ya hisa.

Hivyo, Tanzania inaweza kunufaika zaidi kwa kununua hisa nyingi za kampuni za wawekezaji kama Barrick katika Soko la Hisa la Uingereza na mengineyo.

2. Serikali pia inatakiwa kuonyesha mfano kwa kufuata sheria zilizopo ikiwamo sheria zinazotaka kampuni za madini zilizo nchini ziandikishwe katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

3. Kuongeza ushirikiano baina ya kampuni za udalali wa hisa za ndani na za kimataifa kwenye kutoa elimu, hii itachagizwa na Serikali, ni muhimu kuwe na vivutio vya kodi kama vile gharama ndogo za kodi ya zuio. Kwa kufanya hivyo, wananchi wanaweza kushawishika kuanza kuweka akiba zao katika mfumo wa hisa badala ya fedha taslimu.

4. Kuchukua hatua mahususi za kuoanisha taarifa zinazohusiana na ukuaji uchumi na zile zinazohusu ukuaji wa maendeleo ya watu ili kuwa na picha halisi ya ushiriki wa wananchi katika uchumi wao.

5. Kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa kiha-sibu na kikaguzi utakaobaini ni kwa vipi kampuni za madini zinapata hasara hapa nchini lakini wakati huo huo taarifa zao kwa wanahisa wao zinaonesha kuwa zinapata faida.

4. Kuboresha uwezo wa kitaasisi kwa zile zilizo chini ya Wizara ya Madini (STAMICO na TEITI) ili kuongeza ufanisi na uthabiti kwenye kutimiza majukumu yao

Ili kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa miradi ya maendeleo, wizara kupitia katika bajeti zake za mwaka 2020/21 na 2021/22, imelekeza nguvu na umuhimu katika kuongeza uwezo wa taasisi zake kama vile TEITI na STAMICO ili zitimize majukumu yake ipasavyo.

4.1. The Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative (TEITI):a) Kiasi kidogo kinachoteng wa kwa ajili ya miradi ya maendeleo:

Pamoja na nia njema ya wizara katika kuongeza uwezo wa taasisi zake kama TEITI kwa ajili ya kuongeza uwazi na uwajibikaji, imeonekana wazi kwamba kuna ukosefu wa utashi wa kisiasa kwenye kutoa fedha kwa ajili shughuli za TEITI. Katika kipindi cha miaka mitatu; 2018/19, 2019/2020 na 2020/21 TEITI haikutengewa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya miradi yake ya maendeleo.

Jambo hili limesababisha kuchelewa kukamilika kwa wakati kwa taarifa za mapato ya madini. Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/22, wizara imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.75 ambazo zitatolewa na Benki ya Dunia kupitia mradi wake wa Extractive Global Programmatic Support (EGPS). Pamoja na mambo mengine, mradi huo una lengo la kusaidia sekta kufuata vigezo vya EITI, kujenga uwezo wa wadau kufikia malengo, kufanikisha mazungumzo baina ya Serikali na sekta binafsi kuhusu mchango wa sekta ya uziduaji nchini na uanzishwaji wa mfumo wa kielektroniki wa kuweka taarifa za malipo.

b) Uwekwaji wazi wa mapato kupitia TEITI: TEITI imetoa taarifa kumi (10) za mapato kwa umma mpaka sasa zilizohakikiwa (2009 hadi 2019), zinazoonyesha malipo yaliyofanywa na kampuni za madini kwenda serikali ya Tanzania na kulinganisha risiti za malipo hayo kama yalivyopokewa na Serikali. Hata hivyo, katika wakati huohuo, kumebainika kiasi cha shilingi 90 bilioni na dola 328,000 zimekosa maelezo/viele-lezo kuonesha zilipo.

Ukaguzi maalumu tayari umefanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hasa katika ripoti za saba na nane za TEITI ingawa hadi sasa bado matokeo ya ukaguzi huo hayajawekwa hadharani kwa ajili ya kujadiliwa na wadau kama ilivyo katika ripoti za kawaida za TEITI. Katika kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika jambo hilo, TEITI imeeleza kuwapo jambo hili la fedha zilizolipwa lakini hazionekani katika risiti (stakabadhi za malipo). Kwa upande mwingine, kama ambavyo inatarajiwa na wadau kama HAKIRASILIMALI, Bunge linahitaji kutimiza wajibu wake, hakuna taarifa kuwa limeomba au kuagiza ripoti za TEITI ziwasilishwe bungeni.

c) Ukosefu wa sheria inayomruhusu CAG kufanya ukaguzi kwenye miradi ya uziduaji ambayo serikali ina maslahi: Kwa sababu ya namna mikataba ya madini ilivyosainiwa, wajibu wa CAG kwenye sekta ya uziduaji unakuwa kama wa mtazamaji tu na kumnyima fursa ya kufanya ukaguzi wa miradi hiyo. Ni katika mazingira maalumu tu ndipo TEITI inaweza kumuita CAG kwa ajili ya kufanya ukaguzi. Kwa ujumla, “kunyimwa” huku kwa CAG kukagua mikataba hiyo ni kinyume na Katiba ya Tanzania Ibara ya 143 kuhusu kupata taarifa na kifungu cha 5 na 15 cha Sheria ya Ukaguzi ya mwaka 2008.

d) Ukimya kuhusu mikataba na kufahamika wamiliki: Vitabu vya bajeti ya wizara tangu mwaka 2016/17 hadi sasa havitoi taarifa yoyote kuhusu kuweka wazi kwa mikataba au uanzishwaji wa masjala ya kuhifadhi kumbukumbu za wamiliki wa kampuni. Wakati wa uchambuzi, ilibainika kwamba mchakato wa kuanzisha vitu hivyo unapunguzwa kasi na mamlaka husika kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi bado. Kwa mfano, Aprili mwaka huu, Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara (BRELA) iliongeza muda wa kuwasilisha taifa za wamiliki kwa muda wa miezi 12 zaidi kuanzia Januari 1, 2021 kwa kampuni zilizosajiliwa kabla ya Julai 1, 2020.

Azma iliyotangazwa awali na Serikali ni kwa wamiliki na wanufaikaji wa kampuni za uziduaji kuweka wazi taarifa zao yakiwamo mawasiliano yao na namna ya kuwafikia, ifikapo mwaka 2021 kwa kufuata viwango vya EITI na TEITI.e) Mapungufu ya kitaasisi katika Uratibu:

Sheria na Kanuni kuhusu Uwazi na Uwajibikaji pamoja na taasisi za sekta kama vile TEITI, BRELA na CAG hazishirikiani kikamilifu katika kuhimiza Uwazi na Uwajibikaji.

Mapendekezo.

1. Wizara ielekeze rasilimali fedha kwa taasisi kama TEITI ilikuongeza uwazi na uwajibikaji, ni muhimu kwa sababu hilo litapunguza vitendo vya kifisadi katika sekta.

2. Kuna haja ya kuweka ukomo wa kiasi kinachoruhusiwa “kupotea bila maelezo ya kutosha” kwa sababu upotevu wa kiasi kikubwa cha mapato unasababisha Taifa kushindwa kufikia malengo yake ya kiuchumi na kusaidia miradi mikubwa. Fedha zinazopotea bila maelezo ni mtaji wa kuanzisha mradi kama vile uanzishwaji wa Mfuko wa Madini, Mfuko wa Kuwezesha Wachimbaji Wadogo.

3. Kuna uhitaji wa kuboresha sheria na kanuni, ili Bunge liweze kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha mapato ya nchi hayapotei, Bunge lipokee na kujadili ripoti za TEITI.

4.2. Shirika la Taifa la Madini (STAMICO)

Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara haikutoa taarifa kuhusu ni kiasi gani cha fedha kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara kilitumika kwa ajili ya STAMICO. Ifahamike kwamba katika kiwango kilichoombwa kwa ajili ya maendeleo, ni shilingi 1.2 bilioni tu, sawa na asilimia 21.55, ndiyo kiasi kilichotolewa na Hazina kwa jukumu hilo.Pamoja na kujulikana kiasi kilitolewa na Hazina, hakuna taarifa kuhusu kiasi kilipelekwa STAMICO kati ya hizo.

Katika mwaka wa fedha wa 2021/22, STAMICO imetengewa kiasi cha shilingi bilioni tatu ambayo ni sawa na asilimia 20.13 ya kiasi cha shilingi bilioni 15 kutoka katika makusanyo ya ndani kilichotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.Wakati tukiipongeza wizara kwa jitihada zake za kuiongezea nguvu STAMICO, tafiti mbalimbali zilizowahi kufanywa na HakiRasilimali zimeonyesha kwamba STAMICO imekuwa haifanyi vizuri katika utendaji wake na imeshindwa kujitafutia vyanzo vyake vya mapato kwa ajili ya kuendesha miradi yake.

Katika kipindi hicho cha utafiti, STAMICO imeshindwa kuishawishi Serikali kuwa inaweza kuwa kampuni inayobeba hisa za umma kwa niaba ya Serikali kwenye kampuni za madini na kuratibu shughuli zote za sekta ya madini hapa nchini.

Tunaipongeza pia ofisi ya CAG na TEITI kwa taarifa zao za kila mwaka ambazo zimekuwa zikiele-za matatizo ya mitaji na madeni yanayosababisha STAMICO kufanya kazi zake kwa hasara. STAMICO ina madeni yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 82.3 huku yenyewe ikiwa na mtaji wa shilingi bilioni 12. Kampuni dada ya STAMICO, STAMIGOLD nayo sasa ina deni la shilingi bilioni 66 wakati ina mtaji wa shilingi bilioni 17.

Pia, kushindwa kwa wizara kupitia STAMICO kushindwa kufanya mazungumzo na Wizara ya Nishati kwa lengo la kupatiwa umeme kutoka katika gridi ya taifa nao umekuwa na madhara makubwa kwani STAMIGOLD inatumia zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya petroli kwenye kuendesha shughuli zake.

Jambo hili limeongeza sana gharama za uendeshaji wa kampuni na hivyo kuinyima Serikali mapato ambayo yangetumika kufanyia shughuli nyingine

Mapendekezo

1. Kuongeza mtaji:

Tarehe 14, Oktoba mwaka 2020, iliripotiwa kwamba Serikali kupitia Wizara ilipokea kiasi cha shilingi 1.1 bilioni kutoka STAMICO kama gawio kutokana na faida iliyopata kutoka katika shughuli zake. Hata hivyo, tunaamini kwamba badala ya kutoa gawio kwa Serikali, STAMICO ingeweza kutumia fedha hizo kujiongezea mtaji na kufanya mazungmzo na Wizara ya Nishati yatakayoiwezesha kuweza kuingizwa katika gridi ya taifa ya TANESCO ili ipunguze gharama za uendeshaji.

2. STAMICO kuwa kampuni hodhi:

Serikali inatakiwa kuchukua hatua za makusudi na kuonyesha utashi wa kisiasa kwa kuiwezesha STAMICO kisera na kitaasisi, kubadilika na kuwa chombo imara (kampuni hodhi) kinachoweza kushikilia hisa za Serikali katika sekta ya madini na kwa ujumla kusimamia sekta nzima. Jambo hili litaisaidia STAMICO siyo tu kuongeza mtaji wake si tu kwa kuingia katika mikataba ya kimkakati ya ubia na wawekezaji wakubwa lakini pia uwezekano wa kukopesheka na kushawishi wadau kuingiza mitaji yao katika shughuli zake. Kwa kufanya hivyo, katika muda mfupi, STAMICO itaweza kujitengenezea mtaji wake kwa haraka.

3. Wajibu wa CAG:

Jitihada za kuibadilisha STAMICO ni muhimu, kwa kuiwezesha kuwa kampuni hodhi, pia itakuwa rahisi kwa CAG kufanya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za uziduaji kwa kuwa itakuwa na msingi wa kisheria kufanya hivyo tofauti na hali ya sasa ambapo haiwezi kufanya hivyo.

Kuibadilisha STAMICO kutaipa nguvu ya kuchukua, kwa niaba ya Serikali, asilimia 16 ya hisa katika kampuni za uziduaji, kama ambavyo kanuni mpya za kisheria zimeruhusu kwa kufuata mfano wa namna Shirika la Taifa la Petroli (TPDC) kwenye sekta ndogo ya gesi na mafuta.

5 Rasimishaji wa wachimbaji madogo wa madini Katika kipindi cha muda mrefu sasa, sekta ya wachimba madini wadogo imeanza kukua na mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali umeanza kuonekana. Hili ni jambo ambalo linastahili pongezi kwa Serikali. Hii kwa kiasi kikubwa imetokana na maamuzi kuhusu mazingira wezeshi ya ukuaji; vivutio vya kikodi, kuanzisha masoko ya uuzaji madini na njia nyingine za udhibiti zilizolenga kuhakikisha nchi inafaidika kutokana na sekta hii ndogo ya madini. Pamoja na mafanikio hayo, uchambuzi wa taarifa mbalimbali umebaini kwamba changamoto zinazosababishwa na ukosefu wa sera ya kitaifa kwa ajili ya kuongoza mchakato wa kurasimisha sekta ya wachimbaji madini wadogo ili iendane na Malengo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2025 bado zingalipo.

Baadhi ya changamoto hizo ni; ukosefu wa leseni zinazolindwa kisheria kama zile za wachimbaji wakubwa, ukosefu wa uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu muhimu, ukosefu wa uhakika wa mikopo, teknolojia isiyo ya kisasa, ukosefu wa taarifa za kitafiti kuhusu miamba na madini, kutozwa kodi za mrabaha zaidi ya mara moja, ukosefu wa kupata taarifa sahihi za masoko kiasi cha kuwafanya wachimbaji wadogo kubaki kufanya shughuli hizo kwa kiwango cha kujikimu tu.

Mapendekezo:

1. Sera na sheria:

Kujifunza kwa kutumia mifano ya nchi kama Sierra Leone na Peru ambazo zilichukua hatua mahususi na mabadiliko ya kisheria ikiwamo kutengeneza Sera ya Taifa ya Madini na Sera ya Wachimba Madini Wadogo. Kuwa na Sera, Sheria na Taratibu pamoja na ujenzi wa taasisi zenye uwezo wa kufungamanisha sekta ya wachimbaji wadogo na mkakati wa maendeleo ya vijijini kwa kuhusisha taasisi husika za serikali kama vile wizara, taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo, vyombo vya dola na asasi za kiraia ni jambo la muhimu.

Sheria pia zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili zichochee kampuni kubwa kuwa na utaratibu wa kutoa kazi kwa wachimbaji wadogo pamoja na kuwa na programu za kuongeza uwezo na weledi kwa wachimbaji wadogo. Kwa namna hii, pande zote mbili zitanufaika.

2. Mafunzo na ujengaji uwezo:

Programu za mafunzo yakiwamo ya ufundi stadi katika maeneo kuliko na uchimbaji kwa lengo la kuwafundisha wachimbaji wadogo watakaokuwa wakitumika katika sekta hiyo ni muhimu kwenye kukabiliana na changamoto kama vile taarifa za masoko, uongezaji thamani wa madini, uhifadhi wa taarifa, teknolojia pamoja na mambo mengine. Pia, mafunzo haya yanaweza kutumika kufundisha mbinu mpya za uchimbaji zinazolinda mazingira na hivyo kuchochea shughuli kama za ukaguzi wa mazingira na miradi ya kulinda mazingira. Kwa kufanya hivyo, sekta hii itapunguza athari hasi za kimazingira kwa sekta nyingine muhimu kama vile ufugaji, kilimo na misitu.

3. Uanzishwaji wa mfuko wa kusaidia wachim-baji wadogo:

Ili kufikia lengo la kuwa na sekta ya madini inayochangia asilimia 10 ya pato la Taifa (GDP), uanzishwaji wa Mfuko wa Kusaidia Wachimbaji ni wazo la kimkakati. Mfuko huu unaweza kupata fedha kwa wizara kutenga kiasi fulani cha fedha zinazopatikana katika mauzo ya madini kwa ajili ya jambo hili.

Fedha za mfuko huu zitatumika kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali ikiwemo: Utafiti, Mafunzo na Utafutaji wa madini.

4. Kuanzisha kanzidata ya wachimbaji wadogo wa madini ili kufahamu idadi ya wahusika na pia kwenye masuala ya utoaji wa vyeti.

5. Serikali kuwa makini katika kuhakikisha utekelezaji wa sheria zinazotoa nafuu ya kikodi kwa wachimbaji wadogo na pia kuweka mfumo thabiti wa kuzuia biashara za magendo za madini zinazoinyima mapato inayostahili na pia kukomesha ulipaji kodi zaidi ya mara moja unaotokea kwa wachimbaji wadogo hususani kwenye madini kama rubi.

6. Ufuatiliaji na uchunguzi wa migodi inayofanya kazi (uchambuzi wa mazingira)

Katika mwaka wa fedha wa 2020/21, wizara imetoa taarifa ya kufanya ukaguzi wa usalama wa afya na mazingira katika maeneo ya kazi kwenye kampuni za madini zilizoonyesha kufuata maelekezo ya kufanya maboresho katika mwaka uliotangulia wa fedha.

Mojawapo ya changamoto kubwa zilizojitokeza ni kutokuwapo kwa mipango ya kuhakikisha kwamba kampuni hizi zitaacha mazingira katika hali nzuri wakati zitakapokuwa zimemaliza shughuli za uchimbaji.

Pia, kuna migodi ambayo haina mfumo mzuri wa kuhifadhi taka zikiwamo za sumu kwa kufuata kanuni zilizowekwa kama kuweka mabwawa ya kuhifadhi taka hizo.Matumizi ya zebaki katika kusafisha madini bado yanaendelea miongoni mwa wachimbaji wadogo na hadi sasa Serikali imechukua hatua kidogo sana katika kuondokana na hali hii.

Tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kwamba uchimbaji mdogo wa madini unaotegemea matumizi ya zebaki ndiyo chanzo namba moja cha uchafuzi wa mazingira. Kwa muda sasa, jamii zilizo jirani na migodi zimekuwa zikiathirika sana na hali hii kwa sababu uchafuzi huo umeingia katika maji wanayotumia na udongo wanaotumia na zipo ripoti za vyakula kama samaki ambavyo vimekutwa vimeathiriwa na hali hiyo.

Athari za sumu hizi kwa watoto ni kubwa na zinaweza kuji-tokeza au kuonekana kwenye mwili au kiakili. Kwa sasa, mipango mbalimbali ya kupambana na matumizi ya zebaki kwenye migodi imekuwa haifanikiwi kwa sababu bado watu hawajapewa elimu ya kutosha.

Changamoto

1. Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi unatarajiwa kufungwa ifikapo Juni mwaka 2021, lakini hadi sasa taarifa tulizonazo ni kwamba hakuna tathmini iliyofanywa na Kamati ya Kitaifa ya Kufunga Migodi kuangalia endapo kiasi kilichotolewa na kampuni hiyo kama fidia kwa uharibifu wa mazingira iliyoufanya unaendana na uharibifu wenyewe.

2. Ukosefu wa mpango timilifu wa uhifadhi wa taka na matope yenye sumu ni changamoto inayojirudia katika kampuni nyingi za madini, ikiwemo North Mara Gold Mining.

Mapendekezo

1. Serikali kupitia Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), inahitaji kufanya mapitio ya mipango ya kutunza mazingira kabla ya kufungwa kwa migodi ili kuona kama inafuatwa wakati migodi ikikaribia kufungwa.

2. STAMICO iweke jitihada zaidi katika tafiti hasa kwenye mbadala wa matumizi ya zebaki (mercury)

3. Kuna haja ya kupitia upya Sera ya Mazingira na Sheria yake ili kujumuisha pia uchimbaji wa madini ya makaa. Tukilenga uwekezaji kwenye vyanzo rafiki vya nishati.

4. Kuna haja ya kuchagiza uwepo wa kanuni zitakazotumika kwa ajili ya ufungaji wa migodi na bima za fidia za mazingira, hapa kanuni ya “aliechafua alipe” (polluter must pay) itiliwe mkazo.

7. Masuala ya kutafakari

7.1. Ushiriki wa Serikali katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye Sekta ya Madini

Utafiti kutokana na vitabu vya bajeti ya miaka ya fedha 2016/17, 2018/19, 2019/2020, 2020/21 na 2021/22 unaonyesha dhamira ya serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini pasipo kuathiri maendeleo na matarajio yanayotokana na tasnia hiyo.

Hili linaweza kuendelea kufanya tafiti za kimkakati katika madini yanayotumika viwandani na yale ya chuma. Hata hivyo, utafiti wa HakiRasilimali katika jambo hilo unaonyesha kwamba Serikali inaweza kufaidika zaidi na sekta hiyo endapo itafanya mabadiliko ya ziada kisera kwenye sekta hiyo ili kuifanya imara, yenye uwazi na inayotabirika.

7.2. Mwelekeo mpya wa mikataba ya madini Vs TWIGA, TEMBO na Helium:

Tunapongeza jitihada zilizofanyika kuhakikisha serikali inajipatia umiliki wa hisa za asilimia 16 kwenye kampuni za uziduaji na pia kupata mgawanyo wa asilimia 50/50 wa faida za kiuchumi baada ya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold yaliyoelezwa kuwa ya kimapinduzi.

Mazungumzo hayo ndiyo sasa yanatumika kama rejea kwenye mazungumzo yoyote na wawekezaji wapya wanaotaka kuingia katika sekta ya madini na uziduaji kwa ujumla. Hata hivyo, kuna mambo kadhaa ambayo hadi sasa wadau wengi hawayafahamu vizuri kuhusu makubaliano hayo ikiwemo;

1) Makubaliano ya mwisho kati ya Serikali na Barrick yaliyofanyika mwaka 2020, pia makubaliano kuhusu mkataba wa uchimbaji wa Nickel kwa kampuni ya TEMBO pia hayako wazi.

2) Ukosefu wa taarifa na uwazi kwenye mikataba na mazungumzo haya ni kinyume kabisa na kifungu cha 16 cha Sheria ya TEITA ya mwaka 2015, na pia ukosefu wa kushirikishwa kwa Bunge kwa nafasi yake ya uangalizi kama ilivyobainishwa katika kifungu cha 12 cha Sheria ya Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act 2017 and kifungu cha 4 cha Sheria ya Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Renegotiation of the Unconscionable terms) Act, 2017.

Majadiliano na makubaliano yalifanyika katika mazingira ya usiri mkubwa kiasi cha kuunyima umma fursa ya kujadili kupitia Bunge. Athari za usiri wa kiwango hiki unajulikana.

7.3. Ushiriki wa Serikali kwenye miradi ya Gesi ya Helium:

Tanzania inaelezwa kuwa na hazina ya gesi ya Helium yenye ujazo wa 138Bcf iliyopo mkoani Rukwa. Hata hivyo, suala la ushiriki wa Serikali katika uendelezaji wa miradi hiyo kupitia kampuni za Gogota (Tz) Limited na Stahamili (Tz) bado halijajadiliwa kwa kina.

Machi 22, 2021 kampuni ya kimataifa ya Heliumone Global Limited iliitangaza kuipa kampuni ya Mitchell Drilling Limited kandarasi ya kuchimba visima vyake vitatu vya gesi pamoja na kazi ya kutafuta gesi katika kisima chake cha nne. Kampuni hiyo ya uchimbaji ilitangazwa kwamba malipo yake yatakuwa ni kwa kupewa umiliki wa hisa katika visima hivyo vilivyoko Tanzania.

Zingatio:

a) Kuhakikisha uwajibikaji, kama yalivyo matakwa ya kisheria, uhamishaji wowote wa hisa kutoka kampuni moja kwenda nyingine unahitaji kupata kibali cha Serikali kwa ajili ya udhibiti na pia Serikali inapata kodi zake inazostahili. Pili, taarifa hiyo kwa umma inakosa taarifa muhimu ikiwamo thamani ya mradi wenyewe na hivyo thamani ya hisa haijulikani. Kukwepa ukwepaji kodi na upotevu mwingine wa mapato, ni muhimu kufahamu thamani halisi ya mradi na hisa zake kwa kufanya ukaguzi wa hesabu za gharama ya hisa na mradi kama mauziano hayo ya hisa kati ya Helium One na Mitchell Drilling hayajakamilika.

b) Helium iko katika kundi la gesi adimu na hivyo uchimbwaji wake ni tofauti na mwingine tuliozoea kufanya hapa nchini. Kwa sababu hiyo, sheria zilizopo za madini na za kodi zina mapungufu katika namna ya kufaidika na maliasilia ya namna hii kwa maana ya kodi na mapato mengine kama mrabaha.

Ni muhimu kwa Serikali kufanya marekebisho ya sheria ili iweze pia kufaidika na uchimbaji wa maliasilia kama Helium ambayo ina faida kubwa.

8 Jinsia Mjadala na tafakuri ya bajeti na suala la jinsia.

Kwa ujumla mapato na matumizi ya fedha za umma vinaongozwa na sheria za fedha ikiwemo; Sheria ya fedha ya mwaka 2001, ambayo inaelekeza mapato yote yanayotokana na uziduaji yaingie katika mfuko maalumu ujulikanao kama Consolidated Fund (CF). Wakati hii ni dhana nzuri, hatari yake ni kuwa ni vigumu kuona matumizi yake kwa makundi mbalimbali kwa jamii moja kwa moja.

Hasa kwa sababu mfuko huu unaweza kuelekezwa kwenye miradi mikubwa ya Nishati, Kilimo, Viwanda na Huduma za jamii. Hata hivyo, tuna uhakika kuwa uwekezaji wa fungu hili kwenye Kilimo na Afya utagusa moja kwa moja maisha ya wanawake, wasichana, wazee na vijana.

Takwimu za Taifa zinaonyesha kuwa Kilimo kinaajiri takriban asilimia 54 ya wanawake. Kwenye afya pia tunaambiwa kua asilimia kubwa ya wanawake ndio waathirika wakubwa katika maeneo ambayo kuna huduma haba za afya, husan huduma za afya ya uzazi.

Pendekezo

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, suala la jinsia siyo moja ya vipaumbele katika bajeti ya wizara ya mwaka 2020/21 na 2021/22. HakiRasilimali tunapendekeza kuwa Wizara ishughulikie masuala ya jinsia katika sekta katika maeneo makuu yafuatayo; uharibifu mazingira, uwakilishi wa wanawake katika taasisi mbalimbali, miradi yote ya maendeleo katika sekta na katika dhana ya Uwezeshaji wa umma (local content).