Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabuni teknolojia za kupunguza matumizi ya viyoyozi, gharama za ujenzi

Mwanasayansi wa maabara, Jason Kaijage, akizungumza na kwa niaba ya timu ya watafiti leo Jumatano, Julai Mosi, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Muktasari:

  • Matumizi ya teknolojia ya lami baridi yanaweza kupunguza gharama za ujenzi wa barabara kwa kati ya asilimia 20 hadi 25, huku yakipunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira na kuruhusu barabara kufunguliwa kwa matumizi ndani ya saa mbili hadi tatu baada ya kazi kukamilika.

Dar es Salaam. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamebuni teknolojia mpya za ujenzi zitakazosaidia kupunguza matumizi ya viyoyozi na majokofu, kushusha gharama za ujenzi wa barabara, na kuongeza uwezo wa miundombinu pamoja na majengo kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Teknolojia hizo za ndani, zinazolenga pia kupunguza utoaji wa hewa ukaa na kuongeza matumizi ya nishati safi, zimezinduliwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya timu ya watafiti leo Jumatano, Julai Mosi, 2026, mwanasayansi wa maabara, Jason Kaijage, amesema ubunifu huo umetokana na utafiti uliofanyika kwa zaidi ya miaka minne ukilenga kupata mbadala wa bidhaa na teknolojia zinazochangia uharibifu wa mazingira.

“Lengo letu lilikuwa kubaini bidhaa zinazochangia uharibifu wa mazingira na kubuni suluhisho litakalosaidia kulinda mazingira huku likitoa bidhaa bora na nafuu zaidi,” amesema Kaijage.

Miongoni mwa teknolojia hizo ni Duracem, teknolojia ya lami baridi inayotumika kujenga na kukarabati barabara bila kuhitaji kupashwa moto kama ilivyo kwa lami ya kawaida.

Kaijage amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kupunguza gharama za ujenzi wa barabara kwa asilimia 20 hadi 25, huku yakipunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira na kuruhusu barabara kufunguliwa kwa matumizi ndani ya saa mbili hadi tatu baada ya kazi kukamilika.

“Lami ya kawaida hulazimika kupashwa moto, jambo linaloongeza gharama za ujenzi na kutoa gesi hatari kwa mazingira. Hii ya kwetu ni nafuu zaidi, ni rafiki kwa mazingira na inaruhusu magari kuanza kutumia barabara ndani ya muda mfupi,” amesema.

Katika sekta ya ujenzi wa majengo, watafiti hao wameunda matofali na paneli maalumu za kuta zenye uwezo wa kuhifadhi hali ya joto inayofaa ndani ya jengo, hivyo kupunguza matumizi ya viyoyozi, majokofu na gharama za umeme.

“Tunaelekea katika kipindi ambacho mahitaji ya umeme yataendelea kuongezeka kwa sababu watu watahitaji viyoyozi kwa ajili ya kupunguza joto ndani ya nyumba na majokofu kwa ajili ya kupooza maji. Hali hiyo itaongeza matumizi ya umeme, ndiyo maana tunatafuta njia za kukabiliana nayo.”

“Ndiyo maana tumebuni vifaa vya ujenzi vitakavyopunguza utegemezi wa mifumo ya kupooza majengo. Kwa kutumia matofali yetu, hata kama nje kutakuwa na joto kali, ndani ya nyumba kutabaki na ubaridi, hivyo haitakuwa lazima kutumia kiyoyozi kwa sababu matofali hayo yatazuia joto kuingia,” amesema.

Mbali na teknolojia hiyo, watafiti hao pia wamebuni kemikali maalumu ya kuimarisha udongo inayowekwa chini ya tabaka la barabara katika maeneo yenye maji mengi chini ya ardhi au chumvi nyingi, hali inayosaidia kuongeza uimara na maisha ya barabara.

Pia wamebuni Nova Cement, aina mpya ya saruji inayostahimili unyevunyevu na kiwango kikubwa cha chumvi katika maeneo ambayo saruji za kawaida huharibika kwa haraka.

Amesema saruji hiyo inaweza kutumika kutengeneza matofali na paving blocks zenye uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, huku zikiendelea kuhifadhi ubora wake bila kuathiriwa na unyevunyevu au ukungu.

Kwa upande wa nishati safi, timu hiyo pia imebuni teknolojia ya kusafisha gesi ya bayogesi inayozalishwa kutokana na taka za kikaboni na samadi ili iweze kuhifadhiwa kwenye mitungi na kutumika kama gesi ya kawaida ya kupikia.

“Ikishasafishwa, gesi hiyo inaweza kujazwa kwenye mitungi na kutumika kama gesi nyingine za kupikia. Hii itasaidia kaya zinazozalisha bayogesi kutumia nishati hiyo kwa urahisi zaidi bila kutegemea gesi za kibiashara,” amesema.

Kaijage amesema teknolojia zote zimekamilisha hatua za majaribio ya maabara, huku baadhi yake ikiwemo lami baridi tayari ikiwa imefanyiwa majaribio kwa kushirikiana na kampuni moja ya ndani inayojihusisha na ujenzi wa barabara.

Amesema pia mazungumzo yanaendelea na mamlaka zinazohusika na ujenzi wa barabara ili teknolojia hizo zianze kutumika kwa kiwango kikubwa nchini.

“Utafiti umekamilika. Changamoto iliyopo sasa ni kuhamia katika uzalishaji wa kibiashara ili wananchi wengi zaidi waanze kunufaika na teknolojia hizi,” amesema.

Akizungumzia matofali yenye uwezo wa kupunguza joto ndani ya nyumba, Mkurugenzi Mkuu wa Cam Constructions, Castor Mahundi, amesema katika nchi zilizoendelea tayari matofali ya aina hiyo yanatumika.

“Matofali haya kwa kawaida huwa na uwazi katikati. Hali hiyo husababisha joto linalopiga ukuta kubaki katika uwazi huo, hivyo kuhifadhi ubaridi ndani ya jengo. Tanzania yapo baadhi ya maeneo yanayotumia teknolojia hii, lakini si kwa kiwango kikubwa kwa sababu wengi bado wanajenga kwa mazoea,” amesema.