Wachambuzi wanavyozungumzia uteuzi wa Rais Samia

Wachambuzi wanavyozungumzia uteuzi wa Rais Samia

Muktasari:

  • Baadhi ya wasomi waliozungumza na Mwananchi akiwemo, Dk Paul Luisulie wa Chuo kikuu cha Dodoma (Udom), alisema mabadiliko haya ni muendelezo wa Rais Samia kujiweka sawa kwa kupanga safu yake.

Rais Samia Suluhu Hassan ameanza kupanga upya safu yake akifanya uteuzi wa viongozi wa Serikali ikiwa pamoja na kulipangua Baraza la Mawaziri, ambapo ametengua  uteuzi wa mawaziri watatu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Profesa Adelardus Kilangi na kuteua mawaziri wapya watatu.

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa  na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,  Jaffar Haniu jana Septemba  12, 2021,  kiongozi huyo amehamisha idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na kuipeleka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Walioteuliwa kuwa mawaziri ni Dk Stergomena Tax kuwa  Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akichukua  nafasi ya  Elias Kwandikwa (marehemu).

Mbunge wa Bumbuli,  January Makamba ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati  huku Dk Ashatu Kijaji akiteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Mwingine ni Profesa Makame Mbarawa  aliyeteuliwa kuwa  Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Dk Eliezer Feleshi ameteuliwa  kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Dk  Kilangi aliyeteuliwa kuwa balozi.

Mawaziri wateule pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameapishwa leo Septemba 13  Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Baadhi ya wasomi waliozungumza na Mwananchi akiwemo, Dk Paul Luisulie wa Chuo kikuu cha Dodoma (Udom), alisema mabadiliko yaliyofanyika ni muendelezo wa Rais Samia kujiweka sawa kwa kupanga safu yake.

“Hii ni kwa sababu alirithi ile safu iliyokiwa imeachwa na Dk Magufuli, yeye alifanya kuisuka kidogo ila ulikuwa ni mwanzo kuangalia anaweza kufanya kazi na nani. Kila kiongozi ana namna yake ambayo anapenda anachofanya kwa Watanzania kifanikiwe na kiwe na matokeo chanya,” alisema Dk Luisulie

“Nafasi ya Kwandikwa imerahisisha haja ya kusuka baraza lake na katika uteuzi huu utaona kuna watu ambao wameingia, ila huko nyuma walikuwa mawaziri na sasa wamerudi tena akiwemo Makamba,” alisema Dk Luisulie.

“Huenda mama anaamini hawa anaweza kufanya kazi vizuri zaidi kuliko waliokuwepo awali, kila mtu ni mzuri kulingana na aina na maono ya kiongozi wa juu aliyepo madarakani,” alisema.

Lakini, alitumia nafasi hiyo kutoa mtazamo kuhusu uteuzi wa Dk Tax kuwa mbunge na kupewa uwaziri kuwa unaleta picha yenye maswali mengi.

Alisema hilo linaibua maswali kuhusu ubora wa wabunge zaidi ya 300 waliopo bungeni kwa sasa kama hawakuwa wakitosha kuziba nafasi hiyo au vinginevyo.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kuikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Faraja Kristomus alisema uteuzi huo ulitarajiwa siku nyingi ingawa unaweza kuibua hisia tofauti kwa jamii.

Alisema ilitarajiwa kuwa Dk (Tax) Stargomena angeteuliwa kuwa waziri lakini, hakufikiriwa kama angepewa Wizara ya Ulinzi.

“Na kwa upande wa waliotenguliwa, nadhani wakati wao ulifika ukomo ingawa hisia za wananchi zinaweza kuwa kali kwa kuachwa mawaziri ambao wao walidhani hawajafanya vizuri,” alisema Dk Kristomus.

Hata hivyo, alisema kuwa masikio ya wengi yalitegwa kusubiri hatima ya baadhi ya mawaziri akiwemo wa afya na fedha kutokana na masuala mbalimbali yanayoendelea kwa sasa kuhusu sekta zao.

Akiwa na mtazamo kama huo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Andrew Bomani alisema mabadiliko hayo yalitarajiwa kwa sababu Rais Samia hakuteua mawaziri wapya baada ya kuchukua madaraka zaidi ya kuwahamisha waliokuwepo.

“Nilitarajia atafanya mabadiliko, ni jambo la kawaida kiongozi kuteua watu ambao anadhani watamsaidia kazi,” alisema Bomani.