Samia afyeka mawaziri watatu, ateua wapya watatu

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,   Samia Suluhu Hassanamefanya mabadiliko madogo  katika baraza  la mawaziri  kwa kutengua  uteuzi wa mawaziri watatu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Profesa Adelardus Kilangi na kuteua mawaziri wapya watatu.

Ambao uteuzi wao umetenguliwa  ni aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani; Ujenzi na Uchukuzi,   Leonard Chamuriho na  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Dk Faustine Ndugulile.

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa  na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,  Jaffar Haniu leo usiku Septemba  12, 2021,  kiongozi huyo amehamisha idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na kuipeleka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Walioteuliwa kuwa mawaziri ni Dk Stergomena Tax kuwa  Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akichukua  nafasi ya  Elias Kwandikwa (marehemu).

Mbunge wa Bumbuli,  January Makamba ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati  huku Dk Ashatu Kijaji akiteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.


Mwingine ni Profesa Makame Mbarawa  aliyeteuliwa kuwa  Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Dk Eliezer Feleshi ameteuliwa  kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Dk  Kilangi aliyeteuliwa kuwa balozi.

Mawaziri wateule pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wataapisha kesho Septemba 13,  2021  Ikulu Chamwino Dodoma.

Haya ni mabadiliko ya kwanza kufanywa na Rais Samia tangu aapishwe kushika nafasi hiyo Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha hayati  John Magufuli na ya kwanza tangu alipotangaza baraza la mawaziri  Machi 31, 2021.