Wachimbaji madini watatu wafariki kwa kuangukiwa na kifusi

Monday May 03 2021
machimbo pc
By Mussa Juma

Arusha. Wachimbaji wa madini watatu wamefariki dunia kwa kuangukiwa na kifusi wakati wakichimba madini ya changarawe.

Tukio hilo limetokea leo saa mbili asubuhi wakati wachimbaji hao wakifanya shughuli zao katika mgodi wa madini hayo uliopo Kisongo mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Justine Maseju alithibitisha kutokea vifo na majeruhi katika mgodi huo baada ya kuangukiwa na kifusi.

Kamanda Maseju amewataja waliofariki  katika ajali hiyo ni Nurdin Rajabu(29) Idd Hussein (26) na  Bonkila Martine(27) wote wakazi wa eneo la Ngorbobo lililopo jirani na machimbo hayo.

Waliojeruhiwa ni.Evarist Martin(25) Haruna Mbasa (32) na Eliasi Kigeso wote wakazi wa kijiji cha  Ngorbobo ambao walikimbizwa hospitali kupatiwa matibabu na wameruhusiwa.

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Iddi Kimanta ametembelea eneo la ajali hiyo na kuagiza maofisa wa madini kufanya uchunguzi kama migodi hiyo ni salama.

Advertisement

Kimanta amesema ajali hiyo ingeweza kuepukika kama wachimbaji hao wangeweza kuchukua tahadhari mapema.

Advertisement