Wachimbaji wadogo kukopeshwa mitambo

Mkuu wa mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule(katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mpango wa kampuni ya GF kuwapatia mitambo  ya migodini na Magari ya mizigo  chama cha wachimbaji wadogo mkoani Geita

Muktasari:

  • Wachimbaji wadogo wwa madini mkoani Geita wameingia kataba  wa ushirikiano kibiashara  na kampuni ya uuzaji wa mitambo  ya kuchimbia madini na magari ya mizigo ya GF Trucks & Equipment’s Ltd


Geita. Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita wameingia mkataba  wa ushirikiano kibiashara  na kampuni ya uuzaji wa mitambo  ya kuchimbia madini na magari ya mizigo ya GF Trucks & Equipment’s Ltd

kampuni ya Gf  inayouza mitambo ya migodini na magari ya mizigo ya FAW imeingia makubaliano ya kufanya kazi na Umoja wa wachimbaji madini wadogo wadogo mkoani Geita (GEREMA.)

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano  hayo Mkurugenzi wa Kampuni ya Gf, Salman Karmal amesema Kutokana na kampuni hiyo kujikita katika uuzaji wa mitambo ya migodini na wadau wakuu ni wachimbaji wadogo na wakati kampuni ikaona kuna haja ya kuingia mkataba wa kindugu baina na GF na GEREMA

Karmal amesema kupitia mkataba huo utamwezesha mwanachama wa Umoja wa wachimbaji kuingia katika familia ya  ya GF na kupata mkopo wa mitambo na maroli bila kuwa na masharti magumu wala riba.

“Tunajua wachimbaji wadogo hawana uwezo wa kununua mitambo ya kuchimbia  ili kukidhi mahitaji kwa kulitambua hilo kuanzia leo wachimbaji hao wadogo wanaweza kukopeshwa mitambo, magari kwa vigezo vidogo ambavyo hapo awali walikuwa hawana uwezo huo”.

Naye Katibu wa chama cha wachimbaji wadogo mkoani Geita Golden Hainga amesema mpango huo utaleta manufaa na tija kwa wachimbaji ambao hawana mitaji hivyo kufanya kazi kwenye mazingira magumu yasiyo na tija na wakati mwingine kupata hasara.

“Utaratibu huu wa GF Truck ni mkombozi kwa mchimbaji mdogo maana hawa wataweka dhamana na benki itatoa fedha ,wachimbaji wamekuwa na kilio cha miaka mingi wakiomba kukopeshwa vifaa au fedha ujio wa hawa wadau utasaidia hata benki kuwa na imani na wachimbaji”amesema Hainga.

Mkuu wa mkoa wa Geita Rosemary Senyamule akizungumza wakati wa makubaliano hayo  amesema lengo la maonyesho ya madini ni kuwakutanisha wachimbaji na wadau ambao kwa njia moja ama nyingine watajenga ushirikiano baina yao na wachimbaji .

Aliwataka wachimbaji wanaopatiwa mkopo kurudisha kwa wakati ili kujenga imani kwenye taasisi  za fedha ambazo hadi sasa haziwaamini wachimbaji wadogo na kuwapatia mkopo.