Wachimbaji wadogo wapewa vifaa vya Sh20 milioni

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya kuendeleza wachimbaji wadogo (Fadev), Theonestina Mwasha akikabidhi vifaa vya usalama na afya kazini kwa wachimbaji wa mgodi wa Nsangano uliopo kata ya Nyarugusu wilayani Geita. Taasisi hiyo imetoa vifaa vyenye thamani ya Sh20 milioni.

Muktasari:

Taasisi ya kuendeleza Uchimbaji mdogo (Fadev) imetoa vifaa vya usalama na afya kazini kwa vikundi vitano vya wachimbaji wadogo katika kata za Mgusu, Rwamgasa na Nyarugusu Wilayani Geita vyenye thamani ya Sh20 milioni lengo likiwa kuwasaidia wafanye kazi kwenye mazingira salama na kulinda afya zao.

Geita. Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo (Fadev) imetoa vifaa vya usalama na afya kazini kwa vikundi vitano vya wachimbaji wadogo katika kata tatu wilayani Geita vyenye thamani ya Sh20 milioni.

Hatua hiyo inalenga kuwasaidia wafanye kazi kwa kuwa na mazingira salama na kulinda afya zao katika Kata za Mgusu, Rwamgasa na Nyarugusu.

Akikabidhi vifaa hivyo Agosti 9, 2023, Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo, Theonestina Mwasha  amesema tabia, desturi na mazoea ndio vinavyowafanya wachimbaji wadogo kutovaa vifaa kinga na kusababisha madhara kiafya na yasipozuiliwa mapema husababisha kifo.

Mwasha amesema wachimbaji wadogo wanafanya kazi kwenye mazingira hatarishi yenye vumbi inayoathiri mapafu, kukaa kwenye maji muda mrefu, matumizi mabaya ya kemikali ya zebaki pamoja na hatari ya kuangukiwa na vitu vizito kama mawe ambayo yanaweza kudondoka na kuwasababishia majeraha au vifo.

“Tumeona ili uchimbaji mdogo uwe salama na endelevu tuwape vifaa wafanye kazi wapate pesa lakini maisha yao yawe bora na salama tumegundua wanaishi kwa mazoea wamekuta wazee wao hawatumii vifaa na wao wameendeleza bila kujali madhara ya kiafya,” amesema Mwasha

Mbali na vifaa hivyo, taasisi hiyo imetoa mafunzo ya matumizi sahihi ya fedha na kuwafundisha kuweka akiba pamoja na kuwapa mbinu za kuwekeza kwenye shughuli mbadala ili dhahabu itakapoisha au watakapozeeka wawe na sehemu ya kupata kipato.

Mwenyekiti wa wanawake wachimbaji Mgusu, Bernadeta Petro amesema uchimbaji usiozingatia usalama na afya kazini umesababisha baadhi ya wachimbaji kupata majeraha ya kudumu huku wengine wakiugua kifua kikuu kutokana na vumbi kali la mgodini.

Amesema vifaa walivyopewa vitawasaidia kuingia kwenye mashimo wakiwa salama na kuepuka kupondwa mawe, lakini pia wataondokana na vumbi na kelele hivyo kufanya kazi kwenye mazingira salama na rafiki.

Masabire Modest kutoka chama cha wachimbaji wadogo Mgusu amesema wachimbaji katika maeneo hayo hupata madhara yanayoonekana kwa haraka na yale yasiyo onekana na kusema vifaa walivyopewa endapo watavitumia kama inavyotakiwa vitanusuru afya zao.

Amesema kutovaa vifaa kunasababisha wapate madhara ya kiafya ikiwemo kuugua kifua kikuu kutokana na vumbi linaloathiri mapafu, kupata madhara ya usikivu kutokana na kelele.

Takwimu za kifua kikuu kwa Mkoa wa Geita zinaonyesha kwa mwaka hupata wagonjwa 4,000 na asilimia 18 ya wagonjwa hao wanatoka maeneo ya uchimbaji huku sababu kubwa zikitajwa kuwa ni vumbi linaloathiri mapafu pamoja na nyumba wanazoishi kutokuwa na madirisha.