Wadaiwa kuzika juu ya makaburi yaliyojaa
Muktasari:
- Wakazi wa Kata ya Nyakato Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wanadaiwa kuwazika wapendwa wao kwenye makaburi ya Nyakato Sokoni ambayo yamefungwa baada ya kujaa.
Mwanza. Wakazi wa Kata ya Nyakato jijini Mwanza wanadaiwa kuzika miili ya wapendwa wao juu ya makaburi ya watu wengine katika makaburi ya Nyakato Sokoni yanayodaiwa kujaa kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Februari mosi, 2024 na Diwani wa kata hiyo, Jonathan Mkumba wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani humo, akidai watu wengi wanang’ang’ania kuzika eneo hilo wakidai baadhi ya wapendwa wao walizikwa hapo miaka iliyopita.
“Siku za karibuni baadhi ya wananchi wanakwenda kuzika kwenye makaburi ya Nyakato Sokoni ambayo yamefungwa zaidi ya miaka 10 iliyopita,, ukiwauliza wanasema mama yangu amezikwa hapa na mimi lazima mtoto wangu azikwe hapa,” amesema Mkumba.
Amesema baada ya kubaini changamoto hiyo ameitisha kikao na uongozi wa Serikali ya mtaa akiutaka kuweka matangazo yanayoonyesha kusitishwa shughuli za maziko katika eneo hilo, agizo ambalo anadai wananchi wanalikaidi na kuendelea kuzika.
“Nimemuomba mkurugenzi wa halmashauri kwenye bajeti iliyotengwa itengwe fedha kidogo kwa ajili ya kujenga uzio na ofisi katika makaburi yale ili kukomesha vitendo hivyo.
“Nimekuwa nikishuhudia wakizika pale, kulikuwa na msiba umetokea katika mtaa wangu pale mtaa wa Ihangilo, nilienda kuwatangazia hairuhusiwi kuzika eneo hilo kwa sababu limejaa wakasitisha, tukiweka uzio naamini kero hiyo itakwisha,” amesema diwani huyo.
Akijibu hoja katika kikao cha baraza hilo lililokuwa linajadili rasimu ya bajeti ya mapato na matumizi ya mwaka 2024/25, kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Herbert Bilia amekiri kutambua uwepo wa changamoto hiyo na kusema tayari manispaa imetenga fedha zaidi ya Sh70 milioni.
“Tumekubaliana katika vikao vya baraza la madiwani kwamba maeneo ya maziko yanahitajika kuwa na uzio na ofisi. Kwenye bajeti hii tumetenga fedha kwa ajili kujenga ofisi na uzio, ili maeneo yale yasiharibiwe na kwa kuanzia tutaweka uzio wa nyaya,” amesema Bilia.
Bila kutaja ukubwa wa eneo la makaburi hayo, Bilia amewataka wananchi watakaofiwa na ndugu zao kwenda kuwazika eneo la Kangae wilayani humo, ili kuepusha uharibifu wa makaburi yaliyopo eneo la Nyakato Sokoni ambayo huduma hiyo imesitishwa.
Mkazi wa Kata ya Nyakato katika manispaa hiyo, Happiness Juma amesema wakati mwingine wakazi wa eneo hilo hulazimika kwenda kuzika eneo la Nyakato Sokoni kutokana kuogopa kutenganishwa na wapendwa wao waliozikwa eneo hilo.
“Kwa mfano mimi mama yangu amezikwa pale, hata mimi na familia yangu natamani tukifariki tukazikwe pale karibu na wazazi wetu. Kama Serikali hawataki iwe hivyo basi wajenge uzio, ili watu tusiendelee kuzika eneo hilo,” amesema Happiness.
Kupitia kikao hicho, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Baraza la Halmashauri ya Ilemela limeidhinisha makisio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Sh81 bilioni na baadhi ya fedha hizo zitatumika kama ruzuku kwa ajili ya miradi ya maendeleo (Sh10 bilioni), mishahara (Sh55 bilioni) na matumizi ya kawaida Sh1 bilioni.