Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau waitwa kuwekeza sekta ya mifugo Tanzania

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (wa tatu kutoka kushoto), akiwa na watendaji wa wizara hiyo, pamoja na wadau kutoka Benki ya Dunia (WB) wakionyesha kitabu cha taarifa cha hali ya uchumi kuhusu sekta ya mifugo nchini.

Muktasari:

  • Watakiwa kuwekeza katika sekta za malisho, chanjo, maji ya mifugo na majosho, wizara yasema bado kuna fursa katika maeneo hayo ili kukuza sekta mifugo nchini.

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewaita wadau kuwekeza katika sekta za malisho, chanjo na  maji ya  mifugo  ili kuleta matokeo chanya katika sekta hiyo.

Ulega ametoa wito huo leo Jumatatu Juni 24, 2024 katika uzinduzi wa taarifa ya 21 ya uchumi wa Tanzania iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB), yenye kichwa cha habari ‘Kutumia fursa ya kuwa na sekta ya ufugaji inayokabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na yenye ushindani Tanzania.’

Amesema taarifa ya benki hiyo imeeleza kwa undani kupitia utafiti uliofanyika, ikionyesha kuna fursa kubwa katika sekta ya mifugo, licha kuwepo kwa changamoto mbalimbali.

Mbali na hilo, amesema kunahitaji uwekezaji zaidi wa pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, ili sekta ya mifugo izidi kusonga mbele.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Benki ya Dunia imetaja maeneo yanayotakiwa kuboreshwa, ili kuleta matokeo bora katika sekta ya mifugo ambayo ni udhibiti wa magonjwa, huku Serikali ikijipanga kwa kutenga bajeti ya Sh28 bilioni.

“Jambo jingine ni sekta ya maji ambayo tunashirikiana na Wizara ya Maji, lakini pia suala la malisho limeonekana linahitaji uwekezaji zaidi kutoka kwa wadau, ili mifugo kupata nyasi za uhakika zitakazonenepesha mifugo yao kwa wakati.

“Pia kunahitajika mbegu za mifugo zenyewe, ili tuwe na mifugo bora ikilinganishwa na hiki tulicho sasa,” amesema Ulega.

Kwa upande wa chanjo, amesema kuna kazi kubwa ya kufanya, akisema Serikali imeingia katika mkakati utakaohakikisha mifugo yote inapata chanjo, ili kuzuia maradhi yanayoenea kwa mifugo.

Waziri Ulega amewaomba wadau wa mifugo, kuendelea kutoa ushirikiano katika sekta hiyo, akisema suala la mifugo ni la kila mtu na Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wote, wakiwamo wafugaji na wawekezaji.

“Upande wa Serikali tumeshafanya ndani ya miaka mitatu, tumetoka katika kiwango cha Sh31 bilioni hadi Sh112 bilioni, mafanikio mazuri yanayonyesha mwanga mkubwa mbele ya safari katika sekta ya mifugo, lakini tunahimiza sekta binafsi kufanya uwekezaji zaidi,” amesema.

Hata hivyo, taarifa ya Benki ya Dunia imeonyesha uwekezaji katika sekta ya mifugo bado mdogo ukilinganisha na fursa zilizopo katika sekta hiyo. Licha ya kuipongeza Serikali kwa jitihada zinazochukuliwa za kukuza sekta ya mifugo, imesema kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Nathan Beleta amesema Tanzania ni Taifa lenye idadi ya mifugo inayokua kwa kasi katika bara la Afrika na duniani.

Amesema kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na ng'ombe milioni 36.6 na kuifanya kuwa ya pili kwa idadi kubwa barani Afrika, baada ya Ethiopia.

Hata hivyo, Belete amesema  kulingana na ripoti zilizopo, sekta ya ufugaji na malisho, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kunyesha kwa mvua na joto kali.

“Magonjwa ya mifugo yanayoenea yanaathiri afya ya wanyama, tija na upatikanaji wa soko,” amesema Belete.

Kwa mujibu wa taarifa ya ripoti ya WB inaeleza bado sekta ya mifugo inakabiliwa na changamoto kubwa mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mvua zisizo na uhakika na joto kuwa  juu zaidi

Changamoto hizi zinazotokana na hali ya hewa husababisha kubadilika-badilika kwa upatikanaji wa maji na malisho na kuimarisha ushindani wa rasilimali na uharibifu wa ardhi, hasa katika mikoa yenye ukame.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa changamoto hiyo inasababisha vikwazo vya kijamii hasa katika maeneo ya vijijini kupunguza upatikanaji wa rasilimali muhimu kama ardhi, maji na lishe.Pia husabababisha pia magonjwa ya mifugo yanazidi kuwasumbua kuathiri afya ya wanyama, kukosekana na tija na kushindwa kuyafikia masoko.

Hali kadhalika ripoti hiyo imebainisha kuwa sekta ya mifugo ya Tanzania ni pana na umuhimu mkubwa katika kaya nyingi, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya mifugo, lakini mchango wa pato la Taifa unaotokana na sekta hiyo bado mdogo.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika kuongeza kipato, hasa kwa kaya maskini zaidi, zinazochangia kwa kiasi kikubwa ajira, usalama wa chakula, lishe, na wanawake na ushirikishwaji wa vijana.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa katika kipindi cha miaka 10  iliyopita, Tanzania imekuwa ukuaji wa   katika uzalishaji wa mifugo, kuzidi kasi ya uzalishaji wa mazao, ingawa hasa kupitia idadi ya mifugo badala ya mavuno.