Wadau waja na mbinu kudumisha mila Kilimanjaro

Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali , kilimanjaro Cultural Festival (KCF)Ansi Mmasi katikati  akizungumza na waandishi habari Leo Disemba  3,2023,  hawapo pichani. Picha na Fina Lyimo

Muktasari:

  • Wadau wa maendeleo Mkoa wa Kilimanjaro wameanza kupambana kurejesha mila na tamaduni zinazoanza kupotea Mkoani kilimanjaro.

Moshi. Wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Mkoa wa kilimanjaro, wameanza kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa kukutanisha viongozi wa koo za makabila mbalimbali ya mkoa huo ili wawe chachu ya kurejesha mila na desturi ambazo zimeanza kupotea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 3, 2023 mjini Moshi, Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya Kilimanjaro Culture  Festival (KCF) Ansi Mmasi  amesema taasisi hiyo itatumika kufundisha mila na tamaduni za Kilimanjaro, kwa kutumia viongozi wa koo.

Amesema pia taasisi hiyo inalenga kutoa  elimu  ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana pamoja na kutoa fursa za kiuchumi,  utalii, kwa jamiii  na koo za makabila ya  wanakilimanjaro

Mwenyekiti huyo, amesema taasisi hiyo Itazindua tamasha la utamaduni litakalo husisha wakazi wa  Kilimanjaro  waishio katika Mataifa mbalimbali duniani.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Desemba 27 na 28 mwaka huu, litaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki.

Kwa mujibu wa Mmasi washiriki wa tamasha hilo watapata fursa ya kutembelea vivutio vya kitalii vya utalii vilivyopo mkoani humo pamoja na mapishi ya vyakula vya asili.

"Tunategemea watu zaidi ya 1,000 wa koo mbalimbali za Mkoa wa kilimanjaro ambao wataonyesha tamaduni husika kwa lengo la kuelimisha jamii ya mkoa huu ambayo imetoka kwenye uasili wake na kuiga  tamaduni za magharibi" amesema Mmasi

Amesema washiriki watapata fursa za kiuchumi na utalii ambapo watatembelea mapango ya Marangu, Mapango ya Nubi na Maporomoko ya maji maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Akiunga mkono juhudi hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema ili kurejesha utamaduni wa Kilimanjaro, makanisa na misikiti, amesema wanaona mwanga katika utashi huo, kwa kuwa  utafundisha jamii na viongozi wa koo mbalimbali.

Amesema kuwepo kwa taasisi hiyo itasaidia kutoa elimu ya kiuchumi na kuhamasisha jamii kutembelea vivutio vya kitalii, hasa  mwezi Disemba, ambao wakazi wa Kilimanjaro huzuru mkoa huo kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka.

Amesema kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili kuna haja ya kurejesha mila na desturi ambazo ziko mbioni kupotea.

"Viongozi wa koo na viongozi wa dini wakitumika vizuri mila na desturi za makabila zitarejea ili kuondokana  vizazi vya sasa ambao hawatambui mila zao na kupelekwa kuiga tamaduni za Magharibi"