Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wakemea kuzushiana vifo, kushabikia matatizo ya viongozi

Askofu William Mwamalanga akifurahia na watoto katika Kongamano lililofanyika jijini Dar es SalaamJumapili, Desemba 14, 2025.

Muktasari:

  • Katika siku za hivi karibuni, katika mitandao ya kijamii imeshamiri tabia ya watu kuombeana mabaya na kufurahia wengine wanapopata matatizo, hali inayodhoofisha maadili ya kiroho na mshikamano wa kijamii.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya amani ya kitaifa ya pamoja ya maaskofu na mashekhe, Askofu William Mwamalanga, ametoa wito kwa viongozi na jamii kwa kuachana na tabia ya kuzushiana vifo na kushabikia matatizo ya wengine.

Rai hiyo ameitoa jana Jumapili, Desemba 14, 2025, katika kongamano maalumu la kujenga misuli ya haki, amani na upendo lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Askofu Mwamalanga, akizungumza mbele ya waumini na vijana waliokusanyika katika Kanisa la Injili ya Ufalme wa Mungu, ameeleza kuwa kumekuwa na mwenendo hatari wa kijamii ambapo watu wanatabiria wengine vifo kwa chuki na kufurahia pale viongozi wanapopata matatizo ya kiafya au kisiasa.

Akizungumzia tafsiri ya tabia hiyo na agizo la Mungu, Askofu amesema tabia hiyo si ya kiroho bali ni ya kiburi na inaharibu mshikamano wa kijamii, akitoa wito kwa jamii kumrudia Mungu ili kujitenga na maisha yanayojenga chuki katika jamii.

"Njooni ninyi nyote mnaolemewa na mzigo ya dhambi, naye atawatua mizigo yenu ya dhambi," amesema, akinukuu maandiko ya Biblia (Matayo 11:28) kuhimiza viongozi na wananchi kumrudia Mungu badala ya kushabikia maovu. 

Katika hotuba yake, Askofu Mwamalanga pia, ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, akimtaja kama askari mchapakazi.

Sambamba na hilo, amekemea kauli zinazotofautiana kutoka kwa viongozi kuhusu hali ya marehemu kabla ya kifo chake, akisema zinadhihirisha ukosefu wa mshikamano na upendo miongoni mwao. 

"Waziri mmoja anasema marehemu alikuwa anaanguka anguka, mwingine anasema hajawahi kuumwa, mwingine tena anasema tulikuwa naye jana akiwa mzima, mimi kama kiongozi wa kiroho nawaonya mrudieni Mungu haraka," amesema.

Askofu ameongeza kuwa viongozi wanapoteza sifa ya uongozi wanaposhabikia matukio ya uongo na kushindwa kuonyesha mshikamano wa kweli, akiwataka wakiri matatizo yaliyopo na kutubu ili Mungu aweze kuwarehemu. 

Askofu Mwamalanga alikemea pia tabia ya baadhi ya viongozi wa dini na wananchi kuwakejeli wanasiasa wanapopoteza nafasi zao za uongozi.

Ameonya kuwa kejeli hizo ni dalili ya ufinyu wa maarifa na kupoteza maadili ya kiroho. 

"Kumkejeli mtu ambaye amepoteza uwaziri, ubunge au urais ni ufinyu wa maarifa, acheni kuiga lugha za kejeli, mnapoteza maadili na heshima zenu mbele ya jamii," ameonya.

Aidha amesisitiza kuwa nafasi za uongozi ni siri ya Mungu na si jukumu la binadamu kuhukumu.

Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na vijana zaidi ya 3,400, Askofu Mwamalanga pia amezungumza na vijana, akiwataka kujitenga na ujinga na uongo unaoenea mitandaoni.

Amesema kushinda mitandaoni bila kujenga imani sahihi ya kumcha Mungu kunaharibu maadili ya kizazi kipya. 

"Vijana ni vema mkajilinda na kukaa mbali na tabia za uongo na kuzua taharuki katika jamii kwa vitu vya uongo uongo. Jitengeni navyo," amekemea.

Katika kongamano hilo, amejibu maswali mbalimbali ya vijana sambamba na kutoa ubatizo kwa vijana.

Askofu Mwamalanga ameonya kuwa mtindo wa kutabiria vifo kwa chuki umeanza kuwa kawaida na ni tabia ya kiburi.

 Amesema badala ya viongozi wa dini kushabikia maovu, wanapaswa kuwa manabii wa kuwaokoa watu ili wamche Mungu. 

 "Toeni nabii za kuwaokoa watu ili wache Mungu, msichukue nafasi ya kuhukumu," amesema.

Ameongeza kuwa kuzusha vifo ni uongo unaosababisha taharuki na kupoteza imani ya jamii kwa viongozi wa kiroho na kisiasa. 

Askofu Mwamalanga amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka viongozi wa dini na kisiasa kuacha kushabikia maovu na badala yake kujikita katika kujenga mshikamano wa kijamii.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi wa kiroho kuwaombea na kuwasaidia wale wanaopata matatizo badala ya kuwakejeli. 

 "Ni dhahiri mnapoteza sifa ya uongozi kama mna matatizo njooni tuwasaidie, ni wajibu wetu kuwaombea.

 Lakini mtubu na mseme shida yenu ili yamkini Mungu apate kuwarehemu," amesema akihimiza maadili ya kiroho, na kuonya vijana dhidi ya tabia zisizoendana na maadili mema.

Msimamo huo, unaungwa mkono na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, ambaye alipozungumza na Mwananchi leo, Jumatatu Desemba 15, 2025 ameitaka jamii kuachana na tabia ya kushabikia matatizo ya wengine.

"Katika hali ya ubinadamu hatupaswi kushabikia shida za wenzetu, kwani binadamu ana hadhi yake.

"Lakini pia, tofauti za kisiasa zisitumike kutugawa kama jamii hadi tukashindwa kusalimiana na kusaidiana kwani hiyo si ishara njema kwa jamii," amesisitiza.

Sheikh Ponda amesema ipo haja pia jamii kuangalia malezi ya vijana hasa katika eneo la kisiasa akitaja kuwa watu kufikia hatua ya kushabikia matatizo ya wenzao ni mpasuko ambao unaondoa umoja na mshikamano katika jamii.

Kwa upande wake, Mtetezi wa haki za binadamu, Ananilea Nkya, ametoa wito kwa jamii kutenda haki na kusimama na watu wakati wanapopata matatizo badala ya kuwaacha peke yao ili kuondoa hali hiyo.

"Mimi ninachokiona ni wajibu kwa jamii ndilo jambo la msingi,  watu wote ambao wana wajibu kwa jamii, mfano viongozi, waandishi wa habari, watumishi hata wasanii wajue kuwa katika kazi yao wanapaswa kusimama na watu.

"Hizi ni zama za teknolojia, watu wanarekodi kila unachofanya, kama utawaacha wakati wa matatizo ukumbuke kuwa siku na wewe yakikupata watakukumbusha ulivyowahi kuwatendea ndipo unaona watu wanafurahia matatizo ya mwingine," amesisitiza Nkya.

Amefafanua kuwa kutenda wema kunafanya watu wasimame waguswe pale mtu huyo anapata tatizo, badala yake kutawafanya watu walipize ubaya kwa kufurahia matatizo ya wanayemuona hakuwa pamoja nao wakati akiwa hana shida.