Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango asimulia madhila uzushi wa kifo chake

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2023.

Muktasari:

  • Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amewataka Watanzania kutumia mitandao ya kijamii kuombeana mema na heri badala ya kuzushiana kifo kama ambavyo iliwahi kumtokea na kumsababishia madhila makubwa.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema uzushi kuhusu kifo ambao umekuwa ukisemwa mitandaoni mara kadhaa umeleta madhila mengi kwa watu wake wa karibu na wale wanaomtakia mema.

Amesema miongoni mwa madhila yaliyomkuta baada ya kuzushiwa kifo ni pamoja na dada yake mlezi aliyekuwa na umri wa miaka 80 kupata mshtuko na kuanguka baada ya kusikia kutoka mitandaoni kwamba amefariki dunia mwaka 2021.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumapili, Desemba 10, 2023 wakati akimkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kuhutubia wakati wa kupokea hundi ya michango kwa ajili ya maafa ya Katesh, Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara, hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino, mkoani Dodoma.

“Unajua ukisema huyu mzee amekata moto, wengine wanaweka picha yangu na mshumaa unawaka. Mheshimiwa Rais, sisi viongozi ni binadamu, tuna watoto, wajukuu, familia ndugu na jamaa na tuna wafanyakazi wenzetu, ni taharuki kubwa sana isiyo na sababu,” amesema.

“Mwaka 2021 dada yangu niliyemzika mwezi wa nane, alipoambiwa kwamba mimi mwanaye kwa sababu alinilea nimefariki, alianguka akiwa mama wa miaka 80. Kumbe si vema kuzusha, ni vizuri tujifunze kutumia mitandao ya kijamii kwa kuwatakia mema na heri Watanzania wenzetu,” amesema.

Kufuatia kauli hiyo, Rais Samia kabla ya kutoa hotuba yake amemkaribisha Dk Mpango nyumbani akisema, “Nikwambie tu kwamba ukiwa kiongozi wewe ni public figure (mashuhuri), sasa kuna wale watakaojiuliza yuko wapi mbona hatumuoni, lakini kuna wazushi watakaoamua kuzusha tu na kuleta hataruki kwenye nchi.

“Sasa sisi viongozi tuyapokee tu, karibu nyumbani kama ulivyotukuta tunashukuru karibu uungane nasi,” amesema Rais Samia.

Awali, Dk Mpango amewashukuru waliomwombea na wachache waliosema maneno mengine kwamba amewaombea msamaha kwa Mungu.

Amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kuthamini utu na haki kwa kila mtu na kwamba umoja wa nchi lazima ujengwe katika misingi iliyojengwa na waasisi kama Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume na si kutumia mitandao kwa ajili ya kueneza mabaya.

 Huku akisema ana afya njema, amesema kuwa alirejea nchini jana saa 8 na leo asubuhi akafika Dodoma na kwenda moja kwa moja kanisani.

“Nikakimbilia kwenda kuomba msaada wa Mungu na kumshukuru kwa kurejea salama, kwa hiyo Rais, najua yamesemwa mengi kweli kweli, lakini kikubwa niko salama nina siha njema kama mnavyoniona.

“Nilikuwa namtania mtu mmoja, namwambia mimi si mzuka, kila ninayemsalimia anasema ni wewe kweli au mwingine,” amesema.

Amesema kwa sasa yupo tayari kuendelea na kazi ukiacha hizo maalumu ambazo alikuwa anashughulika nazo.

Katika hatua nyingine, Dk Mpango ametoa shukrani kwa viongozi na wote waliohangaika na maisha ya Watanznaia waliopatwa na majanga huko Hanang.

“Pole sana Rais kwa maafa haya katika Taifa letu, lakini pia pole sana kwa wananchi wa Hanang na Watanzania kwa ujumla. Haya ni maafa makubwa, zaidi ya watu 80 wamepotea hii ni nguvu kazi ya Taifa, tuwaombee waliojeruhiwa, waliopoteza mali nasi tunawaombea majeruhi wote waweze kupona haraka,” amesema.

“Pamoja na kuwa nilikuwa mbali lakini nilikuona Rais ukiwatembelea, walifarijika sana, nimekuona ukibeba watoto kabisa, yaani mama hawezi kupoteza umama wake, lakini ulivyoelekeza urejeshaji wa huduma muhimu na miundombinu, nakupongeza kwa dhati.”

Dk Mpango pia amempongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuiongoza timu ya Serikali vema na msaidizi wake Waziri Jenister Mhagama na timu yote ya maafa.

“Imekuwa fahari kubwa, wakati inatokea Waziri Mkuu alikuwa Rufiji, nilipoongea naye alikimbia mara moja akimtanguliza msaidizi wake Waziri Mhagama. Mmefanya kazi iliyotukuka tunawashkuru lakini pia hili lililotuleta hapa (kupokea michango), viongozi wetu wa mashirika na taasisi za umma asanteni sana na hongereni,” amesema.