Wadau wakoshwa Rais Samia kuvunja bodi TRC

Rais Samia afanya uteuzi

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan jana alivunja Bodi ya Shirika la Reli la Tanzania (TRC),na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mhandishi John Nzulule ikiwa ni wiki moja baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Dar es Salaam. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi wameleza kukoshwa na hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuvunja bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali, John Nzulule.

 Wadau hao wanaona hatua hiyo itasaidia itapunguza ubadhirifu, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka yanayoisababishia hasara Serikali inayoongozwa na Rais Samia.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumatatu Aprili 10, 2023, wamesema wanaamini ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwa mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita kama itafanyiwa kazi kikamilifu itakomesha ubadhirifu, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka.

Wanaounga mkono hatua ya Rais Samia wamesema wanaamini Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka atatekeleza agizo la kuhakikisha makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi kupitia taarifa ya CAG na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zinazogusa maeneo yao na watakaobainika kuhusiska na ubadhirifu wachukuliwe hatua.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Charles Matekela amesema Rais Samia, ameonyesha kwa vitendo umuhimu wa uwajibikaji kwa kuanza kutengua uteuzi wa baadhi ya viongozi waliohusika na kuisababishia Serikali hasara.

Amesema hatua ya kuwaagiza makatibu wakuu kufanyia kazi hoja za CAG, ni jambo la msingi lakini changamoto bado iko palepale bila kusimamia na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani hoja za CAG zitaendelea kujirudia mwaka baada ya mwaka.

“Kila taasisi lliyokaguliwa huwa inapewa barua ya kosoro zote zilizoibuliwa na CAG, ombi langu kila ofisa masuhuli achukue hatua stahiki, ikiwemo adhabu kali kwa wale wote waliotajwa.

“Pia bodi za wakurugenzi na kamati za ukaguzi ziwajibishwe kwa kasoro zilizotajwa.Vyombo hivi vina wajibu mkubwa katika utendaji wa taasisi za Serikali na mamlaka ya Serikali za mitaa na mashirika ya umma,”amesema Matekela.

Mchambuzi mwingine, Dk Faraja Kristomus amesema ni jambo la muhimu kwa Katibu Mkuu Kiongozi kulifanyia kazi jambo hilo, kwa sababu ndiye anayehusika na mapendekezo ya wajumbe wanaohusika katika bodi na watendaji wa mashirika ya umma

“Katibu Kiongozi yeye ndiye anayehusika na ajira zao, kuna tofauti kidogo kati ya ofisi ya Rais (Utumishi) na ofisi ya Rais inayosimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi anayesimamia makatibu wakuu na watendaji wa mashirika ya umma wanawajibika kwake.

Naye Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kinapendeza kuundwa kwa kamati teule ya Bunge ili watendaji wa TRC wakijieleza ndani ya kamati hiyo kutokana na uzito wa hoja iliyoigusa taasisi hiyo.

“Ukiangalia hoja zote ni kubwa lakini hii ya TRC ni kubwa, ndio maana tumependekeza tusisubiri mchakato wa kawaida wa PAC. Hili suala la ndege za Serikali, Rais amechukua hatua moja kwa moja hatuwezi kuliingilia na halikuwa kwenye hoja za CAG,”amesema Zitto.

Mdau mwingie kutoka mtandao wa Twitter aliyetambulika kwa jina la Kidanga Swahibu amepongeza uamuzi wa Rais na kumtaka awe mkali zaidi kwa kuwa kila Mtanzania anamuangalia yeye.

“Hongera sana rais wetu tunakuomba uwe mkali zaidi kwani kila mtu amekuangalia wewe mana wewe ni kila kitu.” Aliandika Swahibu.