Wadau wapaza sauti ada LST ikiongezeka

Muktasari:
- Wakati Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) ikianza kutekeleza mapendekezo ya kamati ya Dk Harrison Mwakyembe, ongezeko la ada ya mafunzo katika taasisi hiyo limewaibua wadau wa sheria wakisema linaminya haki kwa masikini kuwa mawakili.
Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) ikianza kutekeleza mapendekezo ya kamati ya Dk Harrison Mwakyembe, ongezeko la ada ya mafunzo katika taasisi hiyo limewaibua wadau wa sheria wakisema linaminya haki kwa masikini kuwa mawakili.
Taarifa kutoka Gazeti la Serikali (NG) lililochapishwa Novemba 25, mwaka huu inaonyesha pamoja na utekelezwaji wa mapendekezo mengine ya kamati ya Dk Mwakyembe, ada ya mafunzo imeongezeka karibu mara mbili ya ilivyokuwa awali.
Awali ada ilikuwa Sh1.57 milioni, lakini kwa atakayejiunga katika muhula mpya LST mwakani itakuwa Sh2.95 milioni, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 88.
Ongezeko hilo la ada linakuja ikiwa ni wiki moja tangu kamati iliyoundwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kutathmini mafunzo yanayotolewa na LST ikabidhi ripoti yake.
Ingawa ongezeko la ada si sehemu ya mapendekezo hayo, wadau wanasema uamuzi huo utapunguza mawakili kwa upande mmoja, utaifanya taaluma hiyo kusomwa na matajiri pekee.
Akizungumzia na Mwananchi jana, Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Chris Maina alisema pamoja na ongezeko hilo kuwaathiri wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni, umefika wakati Serikali itoe mikopo kwa mafunzo hayo.
“Kama imemuamini mwanafunzi ikamkopesha shahada ya kwanza inashindwaje kumuwezesha amalizie masomo yake, ukizingatia idadi yao kule LST sio kubwa,” alisema.
Mtazamo wa Profesa Maina hautofautiani na Wakili Jebra Kambole aliyesema ni vigumu kwa watoto wa masikini kuupata uwakili kulingana na ada hiyo.
“Kama mimi ningeongezewa ada wakati nasoma nisingeweza, kwa sababu nilichangiwa na ilikuwa Sh1.6 milioni kwa sababu wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunisomesha,” alisema.
Wakili Kambole aliwataja waliomchangia wakati wa masomo hayo ni Abdallah Gonzi Mhadhiri UDSM, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Engela Kileo na Profesa Senzota wote walikuwa rafiki zake alipokuwa chuoni hapo.
Alieleza gharama hiyo ni kubwa na hailingani na huduma inayotolewa, kwani LST mwanafunzi hutumia miezi sita kujifunza si sawa kutozwa Sh2 milioni.
“Pale hakuna ada pekee kuna mambo mengine, kuna steshenari, kulala, kula na mambo mengine kwa hiyo hii itaathiri taaluma ya uwakili. Wenye hela pekee ndiyo watakaobaki kusoma hiyo taaluma,” alieleza.
Emmanuela Shirima ni muhitimu wa shahada ya sheria, alisema baada ya kuona tangazo hilo la ada amesitisha mpango wake wa kwenda kusoma mwakani.
“Nilijiandaa kwa Sh1.57 milioni ndiyo ada ya awali, lakini leo (juzi) naona tangazo la ada imeongezeka karibu mara mbili, hiyo hela niliyoandaa nitafanyia mambo mengine, kusoma nitaenda baadaye,” alisema.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkuu wa Baraza la Elimu ya Sheria, ambaye pia ni Jaji Kiongozi, Mustafa Siyani alisema si jukumu la CLE kupanga kiwango cha ada inayopaswa kulipwa na mwanafunzi chuoni, bali jukumu lake ni kusimamia ubora wa elimu ya sheria.
“Pengine hiyo ndiyo njia ya kuongeza ubora mimi sijui, waulize wenyewe LST watakwambia. Baraza lina yake ya kufanya halihusiani na kuongeza ada au kupunguza,” alisema Jaji Siyani.