Wadau wapendekeza suluhisho wanafunzi, vijana kuacha kujinyonga

Muktasari:

  • Elimu ya afya ya akili shuleni yatajwa kuwa moja kati ya mwarobaini wa kupunguza matukio ya watoto na vijana kujiua katika jamii.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa za watoto na vijana kujiua nchini, imeshauriwa semina kuhusu elimu ya afya ya akili iwe inatolewa mara kwa mara mashuleni na hata kuwekwa   kwenye mitalaa.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 700,000 hupoteza maisha kwa mwaka kutokana na kujiua.

Akizungumza katika hitimisho la semina ya siku tano kwa walimu na siku mbili kwa wanafunzi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mashujaa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Rustika Tembele amesema elimu hiyo itawasaidia walimu na wanafunzi katika kutambua dalili za awali kwa mtu mwenye changamoto ya afya ya akili.

Mradi huo unaotekelezwa na shirika hilo una lengo la kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi kuhusu afya ya akili na huduma za unasihi.
Tembele amesema baadhi ya dalili hizo ni pamoja na mfadhaiko, kupenda kujitenga, kuwa na hasira za haraka, kupoteza kumbukumbu na nyinginezo.

"Elimu hii itawasadia walimu na wanafunzi hao kutambua dalili za awali za wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto ya afya ya akili na namna gani wanaweza kuwasaidia kukabiliana nayo.

Amesema shule ni sehemu muhimu kwa elimu ya afya ya akili ili kuwanusuru watoto na vijana hivyo elimu hiyo itawasaidia walimu kubaini watoto walio na changamoto na kukaa nao kuwaweka sawa kiakili.

“Tumeanza na Sekondari ya Mashujaa, walimu watafundishwa kuhusu afya ya akili ili waweze kuwatambua kwa haraka watoto wenye matatizo ya afya ya akili,” alisema Tembele.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa shule hiyo, Sadick Siza amesema pamoja elimu waliopatiwa wanafunzi hao itawasaidia kuwabaini wenzao ambao wanapitia changamoto hiyo na kuwasaidia kwani hao ndio hupata muda zaidi wa pamoja na huwa wanashirikishana katika mambo mbalimbali.

Msaikolojia tiba, Isack Lema amesema kuna umuhimu wa elimu ya afya ya akili kuingizwa rasmi katika mtaala wa elimu ya msingi, sekondari na hata vyuo vya ualimu.
Amesema katika kipindi cha kuanzia miaka 14 baadhi ya vijana hukabiliwa na changamoto hiyo inayosababishwa na mabadiliko mbalimbali anayopitia ikiwemo yale ya kibaiolojia.

"Hivyo katika kipindi hiki elimu hiyo inahitajika zaidi ili kumuweka sawa katika kipindi ambacho anapitia mabadiliko hayo," amesema.

Pia amesema yapo mazingira tofauti yanayoweza kumsababishia mtoto kuwa na tatizo la afya ya akili na yanaweza kuchangiwa pia na mzazi ikiwemo ukali kupitiliza unaweza kumsababishia mtoto kupata ugonjwa wa wasiwasi uliopitiliza.

Kumekuwa na matukio mbalimbali ambayo yameripotiwa ya watoto kujiua ikiwemo lile lilitokea Machi 3 ambapo mtoto wa miaka 10, Dotto mkazi wa Kijiji cha Chalinze Mzee wilayani Chalinze alikutwa amejinyonga baada ya mama yake kumkataza asiende kwenye kigodoro.

Februari 27 mkoani Mbeya mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Lyoto jijini Mbeya, Ibrahim Edson (12 ) alifariki dunia baada ya kijinyonga ndani ya chumba alichokuwa akilala kwa kutumia kamba ya katani.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Benjamin Kuzaga amesema mwanafunzi huyo alifikia hatua ya kujitoa uhai baada ya kufokewa na wazazi wake kwa kuchezea simu ya mama yake hadi kumaliza chaji.

Februari 26, huko Mtwara mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kiromba, Azana Dadi (13), mkazi wa eneo la Muungano Kata ya Kiromba alikutwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia mtandio wake.

Februari 10, mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Kambarage, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Tatu John (10) alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba chumbani kwake.