Wadau wataka kuongezwa muda mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo

Muktasari:

Baadhi ya mawakili wamependekeza kuongezwa muda wa kusoma Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) ili kukabiliana na changamoto ya matokeo mabovu kwa wanafunzi.  


Dar es Salaam. Baadhi ya mawakili wamependekeza kuongezwa muda wa kusoma Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) ili kukabiliana na changamoto ya matokeo mabovu kwa wanafunzi.  

Kando ya hilo, wamependeza kufanyika tathmini ya wanafunzi wanaojiunga na taasisi hiyo kwa madai baadhi ya wanaojiungani kwa kuwa wana uwezo wa kulipa ada na kuchukulia taaluma ya sheria kama suala rahisi.

Wameeleza hayo jana Jumatano Oktoba 12, 2022 katika mjadala wa ‘Space’ uliokuwa ukiendeshwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kuhusu nini kifanyike kufeli kwa wanafunzi wa shule ya sheria.

Mawakili hao waliowaonya wanafunzi wanaosoma sheria wakisema sheria ni tofauti na masomo mengine na inahitajika jitahada za kusoma kwa vitendo na sio nadharia.

Hayo yamejiri kutokana na matokeo ya mtihani wa uwakili yaliyotangazwa na LST mapema mwezi huu kuonyesha kuwa kati ya wanafunzi 633, waliofaulu ni 26 pekee, sawa na asilimia 4.1.

Katika matokeo hayo yaliyoripotiwa na gazeti la Mwananchi na kuzua gumzo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, wanafunzi 265 wamefeli na kuondolewa masomoni (Discontinue) na wengine 342 wametakiwa kurudia mtihani (Supplementary).

Katika maelezo yao, wakili Fulgence Masawe amesema sababu ya wanafunzi wengi kuanguka katika shule ya sheria inatokana na fani hiyo kurahishwa zaidi ambapo kila mtu sasa anataka kuwa mwanasheria.

Ameshauri kuangaliwa zaidi sifa za wanaojiunga, ‘’pia muda wa kusoma shule ya sheria ni mfupi sana, uongezwe ili wanafunzi wapikwe zaidi, halafu wanaokwenda shule ya sheria wawe wamepitia mafunzo kwa vitendo kwanza ndipo wajiunge.’’

Wakili mwingine, Jebra Kambole amesema fani ya sheria ni ngumu na si rahisi kama watu wanavyofikiria huku akieleza changamoto kubwa kwenye shule hiyo ni wanafunzi wengi wasio na ubora.

Changamoto nyingine aliyoitaja Kambole ni muda mfupi wa kusoma  huku  matokeo ya mitihani yakiwa hayatolewi kwa wakati.

“Mitihani unafanya hupewi majibu,unaenda mafunzo kwa vitendo unarudi unafanya majaribio hujui matokeo,  unafanya mtihani wa mwisho  baadaye unamwagiwa majibu, hivyo nashauri muda uongezwe wa kusoma pale,”amesema.


Wakili Sweetbert Nkuba amesema, ‘’mimi ni wakili wa mwanzo mwanzo sana kusoma pale shule ya sheria…, lakini mtaala wake ni tofauti na ule wa chuo kikuu. Mtu akimaliza pale na kuwa wakili anapata cheti cha shahada ya juu ya elimu kwa vitendo.’’

‘’Katika masomo ya juu ya chuo tunafundishwa zaidi vitendo, hasa kuandika nyaraka. Sasa kilichopo shule ya sheria wale wote wanafaulu lazima waelewe dhana ya mafunzo kwa vitendo…, mshangao ni wanafunzi wengi kuamini kwamba msuli walitumia vyuo vikuu wanahamishia kwenye shule ya sheria, badala ya kujifunza kutatua matatizo ya kisheria yaani namna mteja anavyokufuata ofisini na kumsaidia.’’

“Ukifaulu unathibitisha kwamba umefaulu ya kwamba umetatua matatizo ya kisheria. Wakati mimi nasoma kilikuwa na utararibu wa mitahani ya aina ya tatu, ikiwemo mmoja kutokuwa na kazi za darasani. Sasa ukiwa shule ya sheria  hakuna utaratibu huu.’’

Mmoja wa wananchi waliochangia mjadala huo, Boss Kissa mkazi wa Arusha amesema  ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofanya vizuri waanza kwanza kufanya mafunzo kwa vitendo.

Anania Mwasote yeye amesema, ‘’Serikali iunde kamati maalumu kuchunguza kilichotokea Shule ya Sheria, lina mantiki. Kwa sababu Kamati hii itafanya utafiti na kuchimba mizizi kujua kilichotokea katika matokeo ya wanafunzi wa shule ya sheria.’’

‘’Kwa hali ya kawaida wanafunzi 600 kati yao 26 wamefaulu, nadhani kuna shida mahali. Serikali kuunda kamati ni suala sahihi, watajua tatizo liko wapi wanafunzi au walimu.’’