Profesa Shivji asema tatizo ni mfumo ufaulu mtihani Uanasheria

Muktasari:

  • Profesa nguli wa sheria, Issa Shivji ameungana na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kuhusu sababu ya kufeli kwa kiwango kikubwa kwa wasomi wa sheria wanaofanya mtihani wa uwakili.


Dar es Salaam. Profesa nguli wa sheria, Issa Shivji ameungana na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kuhusu sababu ya kufeli kwa kiwango kikubwa kwa wasomi wa sheria wanaofanya mtihani wa uwakili.

Kauli ya Profesa huyo imelandana na ile iliyotolewa na LST kuwa tatizo ni maandalizi ya wanafunzi wa sheria katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Hata hivyo, baadhi ya vyuo hivyo vimekana madai, vikitoa sababu kadhaa na baadhi kuhitaji utafiti zaidi ufanyike.

Hayo yametokana na matokeo ya mtihani wa uwakili yaliyotangazwa na LST mapema mwezi huu yakionyesha kuwa kati ya wanafunzi 633, waliofaulu ni 26 pekee, sawa na asilimia 4.1.

Katika matokeo hayo yaliyoripotiwa na gazeti hili na kuzua gumzo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, wanafunzi 265 wamefeli na kuondolewa masomoni (Discontinue) na wengine 342 wametakiwa kurudia mtihani (Supplementary).

Kufuatia matokeo hayo, Naibu Mkuu wa LST, Profesa Zakayo Lukumay aliiambia Mwananchi kuwa hali hiyo imetokana na wanafunzi kutoandaliwa vema wakiwa vyuoni, suala ambalo limeungwa mkono na Profesa Shivji, mwanataaluma mstaafu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Tatizo ni kwenye mfumo

Mjadala wa suala hilo ukiwa umepamba moto, jana Profesa Shivji alitia mguu akisema tatizo hilo linaanzia kwenye mfumo uliosababisha kushuka viwango vya elimu katika vyuo vikuu.

Mbobezi huyo wa sheria aliyehusika kwenye kamati mbalimbali za kisheria, alisema ni vigumu kumnyooshea kidole mwalimu au mwanafunzi kwa sababu mfumo wenyewe wa elimu umezima mijadala na ubunifu.

“Pasipo mijadala au ubunifu huwezi kuendeleza fikra, na hii inakwenda moja kwa moja kuathiri usomaji na ufundishaji,” alisema.

Profesa Shivji, aliyesoma shahada yake ya kwanza ya sheria mwaka 1970, alisema utatuzi wa changamoto hiyo uanzie kwenye mapitio ya mfumo wa elimu katika taasisi za elimu ya juu.

Kauli ya Shivji haiko mbali sana na ya Dk Neema Mwita, mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) Mwanza, aliyesema mtalaa wa taaluma ya sheria ndilo tatizo katika vyuo vikuu.

Dk Mwita alisema mitalaa haikidhi mahitaji ya taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo, hivyo mwanafunzi anapotoka chuoni na akienda LST anakutana na utofauti mkubwa.

“Mitalaa ni tatizo, haimuandai mwanafunzi kukidhi mahitaji ya LST, kwa hiyo akienda kule anajikuta anakutana na vitu vipya kabisa. Tatizo lipo hapa, tuwe na mtalaa mmoja unaokidhi mahitaji hayo, watafanya vizuri,” alisema.

Mbali na hayo, hitaji la kufanyika utafiti linapata nguvu kutoka kwa Profesa wa Sheria Leonard Shaidi wa UDSM, ambaye pia alisema hakuna anayepaswa kunyooshewa kidole, badala yake kitafutwe chanzo cha tatizo kupitia utafiti.

“Kusema tatizo liko wapi (hapa), sio kweli, unahitajika uchunguzi wa kina, kisha kuja na namna ya kuboresha,” alisema Profesa Shaidi.

LST yapingwa

Profesa Costa Mahalu, makamu mkuu wa Chuo Kikuu Saut alisema mbali na aibu kwa taasisi hiyo kutokana na matokeo hayo, pia inapaswa ijitafakari.


“Haiwezekani wanaofeli mtihani wa uwakili pale LST hawana ujuzi na maarifa katika masomo yao kutoka vyuo walivyosoma. Hapana! Kuna tatizo na lazima utafutwe ufumbuzi,” alisema Profesa Mahalu, aliyewahi kuhudumu kama mkuu wa kitivo cha sheria UDSM na aliyewahi kuwa makamu mkuu wa kilichokuwa Chuo Kikuu cha Bagamoyo.

Profesa Mahalu alisema matokeo mabaya yanasababishwa na makundi matatu ya walimu wanaowafundisha wanafunzi hao wa uwakili.

Moja ya matatizo ni uwezo, pili wanaopenda kuogopwa na wanafunzi na tatu ni wale wasiotaka mafanikio ya wengine, alilolitaja kuwa hatari zaidi.

“Hata hapa Saut niliwakuta walimu wa aina hiyo. Tumefanya kazi kubwa kumaliza tatizo hilo,” alisema profesa huyo.

Alishauri kulindwa msingi wa kuanzishwa kwa LST ambao ni kutoa elimu kwa vitendo kutoka kwa majaji, mahakimu na mawakili wanaoshughulika na mashauri kila siku mahakamani.

“Maprofesa waliobobea katika nadharia wasipelekwe kuwafundisha wanafunzi pale LST kwa sababu kufanya hivyo ni kukiuka lengo la msingi la kuanzishwa kwa chuo hicho,” alisema.

Kabla ya taasisi hiyo, alisema mawakili walipata maarifa kwa miezi tisa kutoka kwa mawakili na mahakimu waliopo kazini.

“Taifa lilipata wanasheria na mawakili nguli, nikiwemo mimi, Jaji mkuu mstaafu, Othman Chande na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda mwaka 1974. Wahadhiri wa LST wajitafakari kwa matokeo haya,” alisema.


“Tunaletewa kisichoiva”

Wakati wasomi hao wa sheria wakisema hayo, LST imeendelea kushikilia msimamo wake ikisema inapelekewa wanafunzi wasiokuwa na uwezo.

“Kwa maneno machache tuseme tu, tunaletewa chakula kisichoiva, hii inawafanya wanapokuja huku wasiweze kuendana na utaratibu,” alisema Profesa Lukumay katika mahojiano na Mwananchi.


Sifa ya udahili

Katikati ya mjadala Wakili Bashir Yakub alitoa andiko mitandaoni kuhusu suala hilo akisema “tatizo ni vyuo vya sheria na linaanza na sifa za udahili wa wanafunzi wanaostahili kusoma kozi hiyo.

“Kuna vyuo hadi mwenye D flat (zote), yaani D English (Kiingereza), D Kiswahili na D ya historia anapata na nafasi ya kusoma sheria.”

Wakili huyo alisema hivi sasa karibia hakuna chuo kisichotoa shahada ya sheria. Chuo hata kikiwa kipya moja ya kozi ambazo wanaanza nazo na ya sheria lazima iwemo, mchanganyiko ambao alisema hauwezi kuwa salama ukifika LST.