Prime
Wadau watoa mitazamo tofauti kuhusu ugaidi, uanaharakati
Rais Samia Suluhu Hassan. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kauli ya Rais Samia kuhusu wanaharakati wanaotumia njia za kuvuruga amani imeibua mjadala, huku wachambuzi wakitofautiana kuhusu mipaka ya uanaharakati na ugaidi.
Dar es Salaam. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaonya watu wanaojiita wanaharakati ambao kutumia mbinu za kigaidi zinazovuruga amani, imeibua mjadala miongoni mwa wachambuzi, huku baadhi wakisisitiza umuhimu wa kulinda usalama wa Taifa na wengine wakihofia kuchanganya uanaharakati halali na vitendo vya kihalifu.
Rais Samia alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika hafla ya kusaini tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa Zanzibar kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, akisema wapo watu wanaojificha nyuma ya jina la uanaharakati lakini matendo yao yanafanana na ugaidi.
“Nataka nitumie pia fursa hii kuwaonya wale wote wanaojiita wanaharakati kwa jina, ili wapate kutambulika duniani, lakini kiuhalisia matendo yao ni ya kigaidi,” alisema Rais Samia.
Alifafanua kuwa ugaidi unahusisha vitendo vya kuvuruga amani, uharibifu wa mali na miundombinu kwa lengo la kuitisha jamii au kuishurutisha Serikali kukubaliana na matakwa ya kundi fulani.
“Watu au kundi hilo linakuwa na kauli zinazovaa sura ya kizalendo, lakini kwa undani ni masilahi binafsi. Mtu anayeipenda nchi yake kiukweli huijenga na sio kuibomoa,” alisema Rais Samia.
Kauli hiyo imezua mitazamo tofauti kutoka kwa wachambuzi, wanazuoni na wataalamu wa sheria kuhusu tafsiri ya uanaharakati, nafasi yake katika jamii na mipaka inayotenganisha harakati za kijamii na vitendo vya ugaidi.
Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa siasa, Profesa Benson Bana, amesema uanaharakati si kosa kwa sababu ni sehemu muhimu ya jamii inayosaidia kutoa sauti kwa makundi mbalimbali.
Profesa Bana amesema yapo makundi mawili makubwa ya wanaharakati, makundi shinikizi na makundi yenye masilahi maalumu.
Amefafanua kuwa makundi shinikizi huwa na jukumu la kuishinikiza jamii au viongozi kuchukua hatua katika masuala mbalimbali, lakini makundi yenye masilahi maalumu hukitetea haki na masuala maalumu yanayowahusu wananchi.
Ametaja kuwa wapo wanaharakati wanaopigania haki za wavuvi, wakulima, wafanyakazi na makundi mengine ya kijamii, huku wengine wakijikita katika masuala kama haki za wanawake, watoto, mazingira na kupinga ukeketaji.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, makundi hayo yana mchango mkubwa kwa sababu huwakumbusha waliopo madarakani kuwajibika na kuhakikisha masuala ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, amesema uanaharakati unaweza kuwa na changamoto endapo mtu atatumia mbinu zinazokiuka sheria, maadili au misingi ya utamaduni wa jamii.
Hivyo, amesema Rais ana haki ya kutoa tahadhari kwa watu wanaovuka mipaka na kugeuka wahalifu, akisisitiza kuwa tatizo si uanaharakati wenyewe, bali ni mikakati inayotumiwa na baadhi ya watu katika kutekeleza malengo yao.
“Uanaharakati si kosa, kosa ni mkakati unaotumika ambao unaweza kuleta tatizo la kisheria,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mwandishi mkongwe wa habari nchini, Jenerali Ulimwengu, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, amezungumzia tofauti iliyopo kati ya mwanasiasa na mwanaharakati.
Ulimwengu ameandika kuwa mwanasiasa asiye mwanaharakati ni mtu anayefuata masilahi binafsi kwa kutumia kaulimbiu na majina ya vyama, huku mwanaharakati akiwa mtu anayesimamia misimamo yake na kubaki imara kwenye anachokiamini.
Ameandika, mwanaharakati hujitolea kusimamia jambo analoliona ni sahihi hata pale linapokuwa na gharama kwake.
“Ukiniuliza mimi, nawadharau wanasiasa lakini ninawaheshimu wanaharakati,” ameeleza Ulimwengu.
Kwa upande wa wataalamu wa sheria, Wakili Fulgence Massawe amesema si sahihi kuwachukulia wanaharakati wote kama magaidi kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kuzima sauti za watetezi wa haki za binadamu na makundi mbalimbali ya kijamii.
Massawe amesema historia inaonyesha kuwa katika baadhi ya nchi zimewahi kuwaita wapigania haki kuwa magaidi ili kuzima madai yao au kuwanyamazisha.
Ametoa mfano wa wapigania uhuru barani Afrika akiwemo Nelson Mandela wa Afrika Kusini, ambaye kwa kipindi fulani aliwahi kutajwa kama gaidi na serikali ya wakati huo kabla ya baadaye kuwa Rais wa nchi hiyo.
Amefafanua kuwa tofauti kubwa kati ya gaidi na mwanaharakati ni njia wanazotumia kufikisha ujumbe wao.
Akifafanua, amesema gaidi hutumia vitendo vya kihalifu, vurugu na hofu kwa siri au kwa njia zinazolenga kuathiri jamii, wakati mwanaharakati huweka wazi madai yake na kutafuta uwajibikaji kupitia njia zinazotambuliwa kisheria.
“Gaidi anatumia mbinu za kihalifu, lakini mwanaharakati ana jambo analotaka litimizwe na analieleza wazi,” amesema.
Naye Wakili Onesmo Kyauke amesema kauli ya Rais Samia ililenga zaidi watu wanaojifanya wanaharakati huku wakishiriki vitendo vingine vya uovu.
Amesema uanaharakati ni sehemu ya maisha ya jamii kwa sababu kila mtu anaweza kuwa mwanaharakati katika eneo fulani, iwe ni haki za binadamu, mazingira au masuala mengine ya kijamii.
Amesema mwanaharakati anayefanya kazi kwa njia halali si gaidi kwa sababu ana madai anayoyasimamia, tofauti na mtu anayefanya vitendo vya kihalifu kwa kutumia nguvu au hofu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alizozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Ijumaa Julai 10, 2026, alisema si sahihi kuwaona wanaharakati kama magaidi.
Alisema kuingiza neno ugaidi katika masuala ya kiraia ni jambo baya linaloweza kutumika kuwabambikia kesi za ugaidi wanasiasa wa upinzani.
“Hii tabia ya kuingiza ugaidi katika masuala ya kiraia imekuwa endelevu hapa nchini. Hii inaweza ikawa vita dhidi ya wanaharakati na zaidi vita dhidi ya viongozi wa Chadema,” alisema akigusia namna aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alivyoshitakiwa kwa ugaidi miaka michache iliyopita.
Mjadala huo unaonyesha mvutano uliopo kati ya wajibu wa Serikali kulinda amani na usalama wa nchi pamoja na umuhimu wa kulinda nafasi ya wananchi na makundi ya kijamii kutoa maoni na kudai uwajibikaji Dk Benson Bagonza, askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe.
Alizungumzia hilo katika mjadala wa wadau visiwani Zanzibar na kufafanua kuwa ni kosa kuharamisha uanaharakati.
"Unaharamishaje uanaharakati wakati Taifa letu limeasisiwa na wanaharakati," alihoji Bagonza akitolea mfano wa waasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume, ambao alisema walikuwa wanaharakati wakati wakipigania mageuzi ya nchi dhidi ya utawala wa kikoloni.