Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waelezea waliyoyaona ndani ya miaka 60 ya Uhuru

Muktasari:

  • Mbali na sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania kufanyika kitaifa jijini Dar es Salaam leo Desemba 9, watanzania wengine  walitumia sherehe hizo kufanya shughuli za kijamii na wengine kutoa kauli mbalimbali. 

Mikoani. Mbali na sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania kufanyika kitaifa jijini Dar es Salaam leo Desemba 9, watanzania wengine  walitumia sherehe hizo kufanya shughuli za kijamii na wengine kutoa kauli mbalimbali. 

Jijini Dodoma baadhi ya wakazi wameishauri Serikali kwa miaka ijayo, kujikita katika kupeleka maendeleo ya vijijini ili kuondoa tofauti kubwa ya huduma za kijamii iliyopo kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

“Waboreshe huduma za jamii na waweke usawa wa huduma kati ya mijini na vijijini. Kwasasa huduma nyingi zilizoko mjini kuzipata vijiji ni nadra sana,” amesema Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango, Zainabu Mtunguja.

Mkazi wa Chinangali, Fatuma Ali ameiomba Serikali kujikita katika huduma za jamii ikiwemo kuwekeza katika miradi ya maji ili kuongeza upatikanaji wake.

Aidha ameiomba Serikali kumulika shule zake ili kuondoa michango inayotolewa kwa wanafunzi ambayo wazazi wengi wanashindwa kuimudu kutokana na hali ya uchumi waliyonayo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisilie amesema ni jambo la kujivunia kuwa licha ya changamoto zilizopo , Tanzania inasherehekea miaka 60 ya uhuru ikiwa na amani, umoja pamoja na utulivu.

“Tunasherehekea uhuru tukikumbuka tulikotoka tumepiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi, elimu na miundombinu. Hata hivyo tuna hamasa pekee ya kuwa na Rais mwanamke wa kwanza tangu tupate uhuru,”alisema.

Mkoani Manyara Mkuu wa mkoa huo, Makongoro Nyerere amekabidhi  mkopo wa pikipiki 43 na bajaji tatu mjini Babati huku akiwataka watanzania kutunza tunu za taifa.

"Tunapotizana miaka 60 ya Uhuru tunapaswa kuendelea kuenzi na kutunza amani, umoja, upendo na mshikamano wa Taifa kama tulivyoachiwa na waasisi wetu hayati mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Karume,"

Mkoani Kilimanjaro Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Mawenzi imeadhimisha miaka 60 ya Uhuru kwa kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na matibabu bure kwa wananchi wa mkoa kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Katika maadhimisho hayo ambayo yalienda sambamba na maadhimisho ya miaka 99, tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Mwenzi, zaidi ya wananchi 4,000,walilengwa kupewa huduma hizo, kutoka kwa wataalamu wa afya pamoja na madaktari bingwa.

Akizungumza katika Viwanja vya Uhuru Park wakati wa utoaji wa huduma hizo, Mganga Mfawidhi wa Mawenzi, Dk Edna-Joy Munisi amesema miaka 60 ya uhuru na miaka 99 ya hospitali hiyo, yapo mambo mengi ya kujivunia ikiwamo hospitali kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya ikiwemo za kibingwa.

"Mawenzi ilianzishwa mwaka 1922, yaani kabla ya uhuru, yapo mambo mengi ya kujivunia, tumeweza kuboresha miundombinu ya hospitali, lakini pia tumeboresha utoaji wa huduma na sasa tunatoa huduma za kibingwa. Leo tuko na madaktari bingwa ambao watatoa huduma za uchunguzi, elimu na ushauri wa kiafya kwa wake watakaofika katika viwanja hivi,” alisema

Kwa upande wake mratibu wa huduma za tiba za hospitali hiyo ambaye pia ni daktari bingwa wa watoto, Dk Michael Irira amesema huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa awali wa magonjwa yasiyoambukiza na  uchunguzi wa homa ya inni ambapo chanjo itatolewa bure kwa wananchi 400 wa kwanza watakaofika na kukidhi vigezo baada ya uchunguzi na ushauri wa madaktari.

"Tunapima shinikizo la damu, kisukari, Homa ya Inni, Macho, na tunao madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, magonjwa ya upasuaji na madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama,  lengo ni kuhakikisha wote watakaofika hapa wanapata huduma bora" amesema Dk Irira.

Akizungumza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Credianus Mgimba, amesema katika Mkoa huo, yapo matatizo mengi yanayotokana na magonjwa yasiyoambukiza na kwamba wataitumia siku hiyo kufanya uchunguzi ili kuyafahamu matatizo yaliyopo katika jamii na kutoa ushsuri wa kiafya.

Pia Mganga mkuu huyo ametumia fursa hiyo kuwataka wakaazi wa Kilimanjaro kuwa makini na kuchukua tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, katika kipindi hiki ambacho kutakuwepo na wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, ambo watafika kwa ajili ya kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka mkoani humo.

"Kilimanjaro hatari iliyopo ni kwamba tuuna muingiliano mkubwa katika kipindi hiki cha Desemba ambapo watu wengi wanarudi nyumbani kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka, wapo watu wanatoka maeneo mbalimbali ikiwamo nje ya nchi, hivyo ni lazima kuchukua tahadhari zote za msingi dhidi ya ugonjwa huu"

"Kwa sasa watu wamejisahau makanisani, masokoni na maeneo mengine watu wamejiachia hakuna anayechukua tahadhari, jambo ambalo ni hatari kwani akiingia mtu mmoja mwenye maambukizi kwenye jumuiya yenye mkusanyiko wa namna hiyo, ugonjwa unasambaa kwa haraka sana"

Kutoka Wilaya ya Hai, Mwenyekiti wa halmashauri ya hiyo, Edmund Rutaraka ameishukuru Serikali kwa kutuma fedha nyingi za miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye halmshauri hiyo, ikiwamo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, barabara pamoja na fedha za ujenzi wa miradi ya maji.

"Nikiri kwamba serikali imeleta fedha nyingi kwetu. Kwa mfano tumepata kiasi cha Sh1.5 bilioni kwa ajili ya barabara, Sh400 milioni kwa ajili ya kituo cha Afya Longoi Kata ya Weruweru, Sh90 milioni kujenga nyumba ya watumishi Chekimaji, Sh 860 milion kwa ajili ya kutengeneza vyumba vya madarasa katika shule zetu za Sekondar. Tuna kila sababu ya kujivunia matunda haya tukiwa tunaadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania,"alisema Rutaraka

Kwa upande wa viongozi wa dini wamesema amani na utulivu uliopo nchini kwa sasa ni kutokana na namna Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyoweka watu pamoja.

Mchungaji  wa KKKT Usharika wa Kiwalaa Moshi ,Richard Njau amesema Tanzania ilipopata Uhuru Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifanya kazi kubwa sana ya kuwaweka  Watanzania pamoja na usawa kwa wananchi wote.

“Miaka 60 ya Uhuru yamefanyika mambo makubwa katika sekta mbalimbali zikiwamo za elimu,afya ,miundombinu ya barabara ,maji ,umeme na mambo mengi ya maendeleo. Nchi yetu imepata mafanikio makubwa, kama kiongozi wa dini napongeza uongozi wa awamu zote kwa kuhakikisha amani ipo .

  “Mwalimu Nyerere alikuwa na maono makubwa sana kutaka wananchi wake wawe kitu kimoja na ndio maana alikuwa hana ukabila wala udini na hii ndio ilimsaidia sana  wakati wake wa uongozi wake,”alisema Mchungaji Njau 

Naye, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shekhe  Shaaban Mlewa amesema viongozi wa dini wanafurahia Uhuru na amani iliyopo nchini na kusema ni kutokana na kuwepo kwa viongozi wenye hofu ya Mungu.

  “Tunafurahi nchi yetu tuko huru ,zipo nchi nyingine zina Uhuru lakini haziko huru ,sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu tuko huru na tunafanya mambo yetu kwa uhuru bila kuharibu sheria za nchi,”amesema Sheikh Mlewa

Imeandikwa na Joseph Lyimo, Sharon Sauwa, Florah Temba, Bahati Chume, Janeth Joseph,