Waendesha Bodaboda wanne wauawa Butiama

Pikipiki

Muktasari:

Huu ni mlolongo wa matukio ya mauaji yanayoripotiwa wilayani Butiama mwezi huu baada ya watu wasiojulikana wanaoaminika kuwa ni majambazi kumvamia na kumuua kwa kumpiga risasi mfanyabiashara Nixon Nixon Gisiri katika tukio lililotokea Mei 21, 2023.

Butiama. Watu wanne wanaofanya kazi ya kuendesha pikipiki za abiria maarufu kama Bodaboda wameuawa kwa kupigwa na vitu vizito kichwani katika tukio lililotokea Kijiji cha Nyakiswa Wilata ya Butiama usiku wa kuamkia leo Mei 28, 2023.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Mei 28, 2023, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambayo chanzo chake hakijajulikana.

"Ninachoweza kwa sasa ni kuthibitisha kuwa ni kweli vijana wanne wanaoendesha Bodaboda wamefariki dunia kwa kupigwa na vitu vizito kichwani; hadi pole sasa hatujajua chanzo cha mauaji haya. Nipe muda niuatilie nitakupatia taarifa iliyokamilika baadaye,’’ amesema Kaegele

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Butiama kwa taratibu zingine za kitabibu, kisheria na kijamii.

Huu ni mlolongo wa matukio ya mauaji yanayoripotiwa wilayani Butiama mwezi huu ikitanguliwa na lile la Mei 21, 2023, ambapo watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walimvamia na kumuua kwa kumpiga risasi mfanyabiashara Nixon Nixon Gisiri.

Mariam Jumanne, mke wa Nixon Gisiri ambaye wakati wa uhai wake alijihusisha na biashara ya madini ya ujenzi alijirehiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali katika tukio hilo.

Watu hao waliokuwa na silaha za jadi na za moto walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara huyo kwa kuvunja mlango wakimshinikiza awape Sh15 milioni walizoamini alikuwa nazo, ndipo wakaamua kumpiga risasi baada ya kuzikosa.