Wafanyabiashara Kariakoo Mnadani wavunja ukimya

Muktasari:
- Wafanyabiashara wa Kariakoo Mnadani waomba msaada kwa Rais na CCM baada ya ukimya wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutoa ripoti ya uchunguzi wa moto uliotokea Oktoba Mosi mwaka huu, Brela wathibitisha uhalali wao.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kariakoo Mnadani wamuomba Rais Samia Suluhu Hassa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingilia kati sakata lao, wakipinga mapendekezo ya ripoti ya kamati.
Ripoti ya kamati ilitolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ikieleza wazi kuwa chanzo cha moto ni hujuma ambayo imetokana na mgogoro uliopo baina yao.
Pia, katika ripoti hiyo kamati ilipendekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kufanya mapitio ya kampuni ya Kariakoo Auction mart ili kupata uhalali wa umiliki wa namna ya uendeshaji wake.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 7,2023 mfanyabiashara wa eneo hilo, Mohamed Siasa amesema wanaendesha biashara kwa mujibu wa sheria na walionyesha barua kutoa kwa msajili wa Brela ya Julai 12, 2022 ikisema, “Napenda kuwafahamisha kuwa kampuni yenu haimo katika orodha ya makampuni mfu yaliyotangazwa kwa jaili ya kuyaondoa katika daftari la makampuni hata kama ingekuwepo mngepata taarifa ya maandishi kutoka kwa msajili.”
Amesema barua hiyo walipewa na msajili baada ya kuwepo kwa mgogoro baina yao na viongozi wao na uwepo wa tetesi wa kampuni yao kutotambuliki kwa msajili wa kampuni.
Siasa amesema walihitaji majibu ya madeni kutoka kwa viongozi ambapo walielezwa wanachodaiwa ni kodi ya ardhi ya mwaka mmoja ya 2022/23.
Ili kufahamu kilichoelezwa na kamati Mwananchi wamefuatilia usajili huo na kukuta ni kweli imesajili na Brela na kwa sasa wanaendelea kuhuisha usajili wao.
Kondo Mtitu amesema ukimya wa mkuu wa Mkoa kuhusu maamuzi yaliyochukuliwa baada ya ripoti ya kamati yanawaweka njia panda maana ripoti imetaja wazi kuhusu chanzo cha moto kuwa ni hujuma na kamera za Cctv zimeonyesha.
“Sioni sababu ya kukaa kimya wakati kila kitu kinajieleza maana ni wazi huyo mtu ni muhujumu uchumi, ametufanya tuishi maisha magumu watu tunadaiwa kodi, tunasomesha na Serikali imekaa kimya inatuumiza,” amesema Mtitu.
Amesema kuna watu wamesababisha waonekane hawana thamani kwa Serikali na hata kuwekewa zuio la kuweka maturubai ya kujikinga na jua kwa madai kuwa wanajenga sehemu ambayo hawaruhusiwi.
Mtitu amesema imefikia hatua wamepelekewa mgambo wa jiji kulinda eneo hilo ili kuzuia kutoendelezwa kwa shughuli zozote hadi pale Serikali itakapoamua cha nini kifanyike kwenye eneo hilo.
“Tuliunda kamati ambayo ilipeleka uthibitisho wote kwa Mkuu wa Mkoa lakini hawajapewa majibu hadi leo taarifa za ripoti ya moto tunasikia kwenye vyombo vya habari tumekuwa kama wakimbizi sasa,”amesema Kondo.
Moshi Mahita, mfanyabiashara wa eneo hilo zaidi ya miaka 30 amesema wameshafika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa lakini kuna majibu na hivyo ameomba viongozi wa juu waweze kuwasaidia.
“Sisi ni wapiga kura wao wanapokaa kimya kwenye jambo kama ili wanajenga nini kwetu tunamuomba Rais, Waziri Mkuu na Paul makonda kulitazama ili kuna mtu anatuhujumu kwenye hili. Hatuwezi kuishi kama wageni katika nchi yetu, mfanyahujuma akiwa huru,”amesema Mahita.