Wafanyabiashara vyuma chakavu watakiwa kujisajili

Muktasari:

  •  Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa mwezi mmoja kwa wafanyabishara wa vyuma chakavu, vifaa vya kieletroniki kujisajili na kupewa vibali kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.


Mbeya. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa mwezi mmoja kwa wafanyabishara wa vyuma chakavu, vifaa vya kieletroniki kujisajili na kupewa vibali kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Mkurugenzi uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria Nemc Makao Makuu, Mhandisi Redempta Samweli amesema leo Alhamisi June 30,2022 kwenye kikao na wadau kilicholenga kuwajengea uelewa wa kanuni za  uendeshaji, utunzaji wa taka hatarishi.

Amesema utandawazi wa teknolojia za kisasa umechochea ongezeko la taka hatarishi hususan utupaji holela wa makopo.

''Tumewaita leo hapa kuwaeleza kanuni na sheria za mazingira katika uendeshaji wa biashara za vyuma chakavu, taka hatarishi na vifaa vya kieletroniki kutokana na kushamili kwa biashara bila kuwa na vibali hivyo ndani ya mwezi mmoja hakikisheni mmejisajili''amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka Nemc kutengeneza mifumo ya kudhibiti taka hatarishi ili kuwakinga wananchi na magonjwa ya milipuko.

Amesema kumekuwepo na changamoto ya utupaji holela wa taka hivyo amewataka Nemc kutunga sheria ndogo za kuwabana watakaobainika ili kuliweka Jiji katika hali ya usafi.

Wakala wa Forodha katika Mpaka wa Kasumulu baina ya nchi ya Tanzania na Malawi, Ramadhani Masangula ameomba Nemc kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kutokana na kuwepo kwa changamoto ya biashara holela ya vyuma chakavu ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira.