Wafanyabiashara waandamana Dar

Wafanyabiashara wa soko la Karume lililoungua wakiwa wameandamana kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Picha na Tatu Mohamed

Muktasari:

  • Wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga wa soko la Karume (Mchikichini) wameandamana hadi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kushinikiza kiongozi huyo atoe tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga wa soko la Karume (Mchikichini) wameandamana hadi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kushinikiza kiongozi huyo atoe tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo.

Wafanyabiashara hao wameandamana leo Jumatatu Januari 17, 2022 ambapo walikuwa wanaimba "Tunataka soko letu" wakiwa wamezingira geti la ofisi hiyo, ikiwa ni siku moja imepita tangu soko hilo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.

Mabomu ya machozi yarindima Dar

Wakizungumza katika tukio hilo, baadhi ya  wafanyabishara hao wamesema wanafanya hivyo baada ya kukosa imani na maamuzi yaliyochukuliwa na viongozi hao huku wakionyesha kusikitishwa kwao na kitendo cha wenzao kuvunjiwa mabanda yao waliyojenga usiku wa kuamkia leo na jeshi la polisi.

Silvanus Mwakipesile amesema Mkuu wa Mkoa aliwaahidi leo saa 2:00 asubuhi angefika kwenye soko hilo kuwaona na kuwapa muongozo lakini wanashangaa kabla ya kiongozi huyo kwenda kuna watu wamevunjiwa mabanda yao na sehemu hiyo kuwekwa chini ya ulinzi mkali ukisimamiwa na Jeshi la Polisi.

"Tumekosa imani na viongozi jana alisema anakuja lakini hadi sasa hatujamuona na chakushangaza waliojenga vibanda vyao wamebomolewa, sisi hatuwezi kuwasubiri wao maisha yetu magumu watuache tujenge wenyewe ili tuendelee kufanya kazi zetu," amesema

"Siku zilizotolewa kwa ajili ya kufanya uchunguzi ni nyingi tunataka tuachwe tujenge mabanda wakati uchunguzi ukiendelea na si kubaki hivihivi tutakula Nini na tunawatoto wanatakiwa kwenda shule,"amesema Saida Mohamed

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija amewaomba wafanyabishara hao kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliotangazwa na Serikali kwamba waiachie kamati ifanye kazi kwa siku saba na kutoa ripoti badala ya kuandamana kutaka kushindana na Serikali.

"Mnatakiwa kujiongeza pamoja na kwamba mnadai haki lakini lazima mfuate utaratibu, jana Waziri aliagiza kamati ifanye uchunguzi hivyo tuiachie Kamati ifanye kazi na ilete ripoti," amesema Ludigija.

Jana baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla aliwataka wafanyabiasha wa soko hilo kuwa watulivu huku akiahidi kuundwa kamati ambayo itachunguza chanzo cha moto huo kwa siku 14 akipiga marufuku shughuli zozote kuendelea wakati wa uchunguzi huo.

Muda mfupi baada ya RC Makalla kutoa tamko hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa aliagiza kamati hiyo kufanya uchunguzi kwa siku saba badala ya 14.