Wafanyabiashra waomba ulinzi kuongezeka vichaa sokoni
Mwenyekiti wa soko la Majengo Jijini Dodoma, Godson Rugazama akizungumza katika mkutano Mkuu wa mwaka wa wafanyabiashara wa soko hilo leo Aprili 26, 2023 jijini Dodoma.
Muktasari:
- Amesema mwaka jana kuna mfanyabiashara wa nyama aliuwawa na chizi lakini hakuna jitihada zilizochukuliwa kuongeza idadi ya walinzi.
Dodoma. Wafanyabiashara wa soko Kuu la Majengo jijini hapa wameliomba Jiji la Dodoma kuongeza idadi ya mgambo mida ya mchana kutokana na machizi kutishia maisha yao.
Akizungumza leo Jumatano, Aprili 26, 2023 jijini hapa, katika mkutano Mkuu wa mwaka, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Godson Rugazama amesema kumekuwa na changamoto ya kuongezeka kwa machizi katika soko hilo (bila kutaja idadi).
Amesema machizi hao baadhi wamekuwa wakiwadhuru kwa kuwapiga wafanyabiashara na wateja katika soko hilo.
Amesema mwaka jana kuna mfanyabiashara wa nyama aliuwawa na chizi lakini hakuna jitihada zilizochukuliwa kuongeza idadi ya walinzi.
Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti huyo ameliomba Jiji kuongeza idadi ya walinzi katika mida ya mchana.
"Mfanyabiashara yupo bize kufanyabiashara, mteja yupo bize kutafuta bidhaa nzuri na tunajua machizi wengi wanapenda kuwepo masokoni, tunaomba ulinzi angalau wa migambo wawili ili kusaidia suala la ulinzi, kwani tunaona machizi, wanaongezeka," amesema mwenyekiti huyo.
Akijibu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru, Diwani wa Kata ya Majengo, Shufaa Ibrahim amesema suala hilo atalipeleka katika mamlaka husika ili liweze kushughulikiwa.