Wafungwa 1,369 wasamehewa
Rais Samia Suluhu Hassan. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha huo kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(a) hadi (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 1,369 kote nchini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Aprili 26, 1964.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumapili, Aprili 26, 2026, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Paschal Katambi, msamaha huo umetolewa na Rais kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba chini ya Ibara ya 45(1)(a) hadi (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika idadi ya wafungwa walioachiwa huru, 436 wameachiwa huru moja kwa moja, huku 933 wakipunguziwa adhabu zao.
“Serikali inatarajia walioachiwa watarejea katika jamii wakiwa na nidhamu na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa, huku wakijiepusha na kurejea tena katika uhalifu,” amesema Katambi.
Kulingana na taarifa hiyo, msamaha huo umejumuisha kupunguziwa moja ya sita ya adhabu kwa wafungwa waliotumikia robo ya vifungo vyao na walioingia gerezani kabla ya Januari 25, 2026.
“Aidha, umejumuisha wafungwa wagonjwa wa magonjwa sugu yaliyofikia hatua ya mwisho, wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, wanawake wajawazito au wenye watoto, pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili waliothibitishwa na wataalamu wa afya,” amesema Katambi.
Pia wanufaika wengine ni waliokuwa chini ya adhabu waliotumikia miaka 10 na zaidi, pamoja na waliodumu gerezani kwa miaka 25 na kuendelea.
Katika hatua ya kipekee, baadhi ya wafungwa wa kunyongwa waliokaa gerezani kwa miaka 15 na kuendelea, adhabu zao zimebadilishwa kuwa kifungo cha maisha kutokana na taratibu za rufaa kutokamilika.
Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje kama Parole na huduma kwa jamii, pamoja na waliokiuka masharti ya mifumo hiyo.
“Makosa mazito kama uhujumu uchumi, rushwa, utakatishaji fedha, dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu, makosa ya kijinsia, ugaidi, uharamia pamoja na makosa ya mauaji na unyang’anyi hayakujumuishwa kwenye msamaha huo.
“Wengine ni wafungwa wa kurudia makosa, waliowahi kupata msamaha wa Rais awali, pamoja na wafungwa wa madeni na maisha (isipokuwa waliobadilishiwa adhabu),” amesema Katambi.