Wagonjwa 35 warekebishwa sura Bugando

Muktasari:
Wagonjwa 35 wamerekebishwa sura na madaktari bingwa 22 kutoka nchini Marekani wakishirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Kanda ya Bugando (BMC).
Mwanza. Wagonjwa 35 wamefanyiwa upasuaji wa kurekebisha sura (plastic surgery) na madaktari bingwa kutoka nchini Marekani wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Kanda Bugando (BMC).
Akizungumzia upasuaji huo Daktari Bingwa wa Upasuaji Sanifu kutoka BMC, Francis Tegete amesema wagonjwa hao ni kati ya 55 waliofanyiwa vipimo.
Upasuaji huo uliofanyika Agosti 21 hadi 25 mwaka huu katika hospitali ya Bugado chini ya madaktari bingwa wa upasuaji sanifu wa uso, pua, koo, na masikio kwa kushirikiana na wataalamu, manesi na madaktari pia ulihusisha madaktari bingwa 22 kutoka Shirika la Healing the Children North East lililopo nchini Marekani.
“Hatuna takwimu kamili za kwamba tunapokea wagonjwa wangapi kwa wiki au kwa siku lakini tunawagonjwa wengi sana ambao wengine ni tatizo la kuzaliwa nalo, ama ukubwani au wengine kutokana na saratani kwahiyo huwa tunaona ni wengi wanatatizo la magonjwa ya shingoni, masikioni, puani na usoni,” amesema Dk Tegete
Mkuu wa Chumba cha Upasuaji katika hospitali hiyo, Dk Stephen Swetala ametaja sababu zingine zinazopelekea tatizo hilo kuwa ni watu kuungua moto, kumwagiwa kitu cha moto usoni, kukatwa na ajali.
“Matatizo ya sura yanaweza kutokea kwa sababu ya ajali mfano za moto, kumwagiwa kitu cha moto usoni, kukatwa pua au sikio ni matatizo ambayo tumekuwa tukiona na kuyasikia mara nyingi,” amesema Dk Swetala
Grace Lwichungula, mkazi wa Bukoba mkoani Kagera ambaye alipata ajali na kupoteza sikio na mkono wa kushoto, ameishukuru hospitali hiyo kwa kumsaidia kumfanyia upasuaji wa sikio huku akiomba huduma hiyo kuzidi kuendelea kutolewa.
“Kiukweli huduma yao ni nzuri sana na tuna tamani wangeendelea kukaa wamalize hata mwezi kwa sababu mfano katika ajali tulipata wengi lakini mimi ndiye niliyefanikiwa kufika na sidhani kama kuna mwengine amepata taarifa,” amesema Lwichungula
Naye Justina Rubango, mnufaika mwingine wa upasuaji huo ameomba huduma hiyo kusambaa zaidi katika maeneo mengine ili wananchi wengi kufikiwa na matibabu hayo.
“Ushauri wangu hii huduma isambae zaidi kwa sababu huko vijijini kuna wagonjwa wengi zaidi lakini huduma hizi hazipo na ; hata mimi ndugu zangu waliposikia nimefanyiwa upasuaji wakawa wanasema na wao wangejua wangekuja,”amesema Rubango