Watu 10 kuondolewa uvimbe wa ubongo Bugando


Jopo la madaktari bingwa bobezi wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Vanderbilt Medical center Nashville nchini Marekani wakifanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo wa mwakamke mwenye umri wa miaka 24 kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Watu 10 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye ubongo ndani ya kipindi cha wiki moja ijayo.

Mwanza. Watu 10 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye ubongo ndani ya kipindi cha wiki moja ijayo.

Operesheni hiyo itakayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando inashirikisha wataalam bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Vanderbilt ya nchini Marekani na wenzao wa Bugando.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Fabian Massaga amesema kazi hiyo iliyoanza Julai 31, 2023 itakamilika Agosti 6, 2023 na kwamba hadi kufikia jana Agosti 2, 2023, wagonjwa wanne tayari wamefanyiwa upasuaji.

“Upasuaji huu unafanyika baada ya matokeo ya uchunguzi wa mfumo wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kwa watu 100 ambao pia ulifanywa na jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu Bugando wakishirikiana na wenzao wa Taasisi ya Tiba ya Vanderbilt ya nchini Marekani,’’ amesema Dk Massaga

Amesema kwa kufanya upasuaji huo, siyo tu madaktari hao bingwa wataokoa maisha ya wagonjwa, bali pia mamilioni ya fedha ambazo zingetumika kuwasafirisha wagonjwa hao kwa matibabu nje ya nchi.

‘’Gharama ya upasuaji unaofanyika Bugando haizidi Sh2.5 milioni; hiki ni kiwango kidogo kulinganisha na zaidi ya Sh15 milioni inayotozwa kwa upasuaji wa aina hiyo nje ya nchi,’’ amesema Dk Massaga

Kiongozi wa jopo la madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Vanderbilt ya nchini Marekani, Profesa Thompson Reid amesema pamoja na upasuaji, ushirikiano kati yao na wenzao wa Bugando unalenga kuwajengea uwezo wataalam wa ndani ili waendelee kutoa huduma bila kuwategemea wataam kutoka nje ya nchi.

Profesa Reid amesema anaamini upasuaji wa wagonjwa hao utasaidia kuwaongezea uzoefu madaktari wazawa ili kuwawezesha kufanya upasuaji mgumu unaohusisha maeneo nyeti na hatari katika ubongo wa binadamu.

"Pamoja na kuokoa maisha, ushirikiano wetu na madaktari bingwa wa Bugando pia unalenga kuwaandaa kumudu kufanya operesheni kubwa na hivyo kuwawezesha kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi, hasa wa vijijini wenye vipato vya chini wasiomuda gharama kubwa za huduma nje ya nchi," amesema Profesa Reid, Daktari Bingwa mbobezi wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu.

Johari Issa, mkazi wa Mtaa wa Iseni jijini Mwanza ambaye ni miongoni mwa waliofanyiwa upasuaji na mabingwa hao ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa kuanzisha ushirikiano na madakatari bingwa kutoka nchi ya nje na hivyo kuwawezesha wagonjwa wenye vipato vidogo kupata huduma za kibingwa.