Saratani ya macho tishio kwa watoto

Daktari Bingwa wa Macho kwa watoto, Evalista Mgaya kutoka Hospital ya Rufaa Kanda Bugando (BMC) akifanya vipimo vya macho kwa mtoto alipokuwa akitoa huduma za macho kwa watoto mkoani Simiyu . Picha na Samirah Yusuph.

Bariadi. Uhaba wa elimu juu ya ugonjwa wa saratani ya macho (Retinoblastoma) umetajwa kuwa ni sababu ya vifo vingi vya watoto kutokana na kucheleweshwa kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza Mei 23, 2023 wakati wa ufunguzi wa kambi ya afya ya macho kwa watoto mkoani Simiyu, Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Dk Bernadeta Shilio amesema ugonjwa huo unawapata watoto kuanzia 0 hadi mitano na wachache wa umri zaidi ya huo.

“Uoni mzuri unachangia ustawi wa watoto kwani unapunguza vifo vya watoto, huwa wanafika katika hospital za rufaa za kanda na taifa wakiwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa hali hiyo inasababisha watoto wengi kupoteza maisha kwa saratani hhiyo” amesema Dk Shilio

Amesema Wizara ya Afya iliandaa miongozo kwa ajili ya kutoa maelezo ya kitaalamu kwa wataalamu wa Afya kwa ngazi zote, kati yake ni miongozo wa Taifa wa matibabu kwa watoto wenye saratani ya macho.

Amesema hadi sasa watumishi wa afya katika mikoa ya Singida, Morogoro, Kilimanjaro na Pwani wamefikiwa na elimu ya ugonjwa huo ili kuifikisha kwa wananchi.

“Wagonjwa walioonwa wakiwa na saratani ya macho hapa nchini kwa mwaka 2022 walikuwa 214, hii ni ongezeko ikilinganishwa na watoto 136 walioonwa mwaka 2021,”amesema

Mtaalamu wa Macho kutoka Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Evalista Mgaya amesema watoto wana muda mrefu wa kuishi wakiwa hawaoni iwapo tahadhari haitachukuliwa tofauti na ilivyo kwa watu wazima.

"Watoto wanapona  kwenye hospital ngazi za chini na mikoa hawafiki ngazi ya rufaa wanapungua kwa sababu wengi huanza kwenda kupata huduma za afya ya macho ugonjwa ukiwa umekomaa,"amesema Dk Mgaya

Akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Juma Topela amesema sababu kubwa ya wananchi kupeleka watoto wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa ni kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya magonjwa ya macho.