Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wagonjwa 90 wapandikizwa figo nchini

Muktasari:

  • Licha ya changamoto za ugonjwa wa figo kuongezeka, Tanzania inazidi kupiga hatua za kukabiliana na magonjwa hayo baada ya kufanikiwa kupandikiza kiungo hicho wagonjwa 90.

Unguja. Licha ya changamoto za ugonjwa wa figo kuongezeka, Tanzania inazidi kupiga hatua za kukabiliana na magonjwa hayo baada ya kufanikiwa kupandikiza kiungo hicho wagonjwa 90.

Wagonjwa hao wamepandikizwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili na Benjamin Mkapa tangu huduma hiyo ianze kutolewa nchini Novemba 2017. Kuna madakatri wa figo 38.

Akifungua mkutano wa nane wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo (Nesot), Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema katika kipindi cha nyuma jambo hilo lisingewezekana na wagonjwa walikuwa wakisafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Haya ni mafanikio makubwa, nchi yetu inazidi kupiga hatua. Sasa ipo haja ya chama kuwajengea uwezo wataalamu wengine katika hospitali za rufaa na ngazi ya jamii ili kuwa na wataalamu wengi zaidi kukabiliana na tatizo hili,” alisema.

Hata hivyo, alisema lazima kuwapo na mipango madhubuti ya kukabiliana na ugonjwa huo na kwamba Serikali zote mbili zinatambua changamoto zinazowakabili wataalumu hao na zipo tayari kutoa msaada kukabiliana nazo.

Alisema takwimu za Tanzania zinaonyesha watu saba hadi 10 kati ya watu 100 wana tatizo la figo, hivyo kutoa picha kwamba tatizo hilo bado ni kubwa.

Awali, Mwenyekiti wa Nesot, Dk Onesmo Kisanga alisema utafiti uliofanyika dunia nzima unaonyesha asilimia 10 ya wagonjwa wanakabiliwa na magonjwa ya figo.

Utafiti wa Tanzania ngazi ya jamii unaonyesha asilimia 6.7 wana magonjwa ya figo na kiasi kikubwa yanachangiwa na uelewa mdogo wa ugonjwa huo.

Alisema wamejiwekea utaratibu wa kuadhimisha kila mwaka siku ya ugonjwa huo kujenga uwezo wa kitaaluma ili kuboresha utoaji huduma za afya ya figo nchini na mwaka huu wamealikwa wataalamu kutoka Ujerumani, Afrika Kusini, Kenya na UK.

“Tulipitisha azimio la mafunzo ya wauguzi wa figo na kwa sasa tayari wauguzi 10 wamehitimu na wengine 15 wanaendelea,” alisema.

Alisema tatizo la figo linakuwa kubwa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza kuongezeka, ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika ugonjwa huo, hivyo akaomba ushirikiano wa utoa elimu kwa jamii.

Pia alisema ugonjwa huo unaathiri watoto, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas).

Utafiti huo unaonyesha miongoni mwa watoto wachanga 378 waliokuwa wanaumwa na kuhudumiwa Muhimbuli kati ya Oktoba 2017 hadi Machi 2018, asilimi 31. 5 walipata ugonjwa wa figo na asilimia 80 ya hao walipoteza maisha.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa figo na mkuu wa kitengo cha usafishaji damu Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Maria Hamad alisema kwa sasa kuna mashine 10 za kusafisha damu na wagonjwa 45 wanapatiwa huduma hiyo kila wiki.