Wagonjwa wa ukoma Tanzania wapungua
Muktasari:
- Jumapili Januari 31, 2021 Tanzania itaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya ukoma duniani huku idadi ya wagonjwa huo ikipungua kutoka zaidi ya watu 35,000 mwaka 1979 hadi chini ya wagonjwa 1,600 mwaka 2019.
Dodoma. Idadi ya wagonjwa wa ukoma nchini Tanzania imepungua nchini kutoka zaidi ya wagonjwa 35,000 mwaka 1979 hadi chini ya wagonjwa 1,600 mwaka 2019.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Januari 29, 2020 na mkurugenzi wa huduma za kinga ya Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi kwa niaba wa waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima.
Dk Subi alikuwa akizungumzia maadhimisho ya siku ya ukoma duniani yanayofanyika kila Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari.
“Idadi ya wagonjwa wa ukoma imeendelea kupungua kila mwaka kutoka wagonjwa zaidi ya 35,000 mwaka 1979 hadi chini ya wagonjwa 1,600 kwa mwaka 2019,”amesema.
Amesema Tanzania tayari imefikia kiwango cha kimataifa cha utokomezaji wa ukoma tangu mwaka 2016 ambacho ni kuwa na chini ya mgonjwa mmoja kati ya watu 10,000.
Amesema pia kiwango cha kutokomeza ugonjwa huo kimeendelea kuimarika tangu mwaka 2016 hadi kufikia chini ya wagonjwa 30 chini ya watu milioni moja.
“Tanzania tayari inayo sifa za kuweza kutokomeza ugonjwa wa ukoma katika jamii yetu. Viashiria vyote muhimu vinaonekana wazi hiyo ni pamoja na dawa za kuponyesha ukoma ambazo tunazo za kutosha,” amesema.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa dawa hizo bila malipo kwa wagonjwa wote.
Amesema kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kimeshuka chini ya asilimia tano na takwimu zinaonyesha.
Pia amesema asilimia 94 ya wagonjwa wapya wanaogundulika kila mwaka ni wagonjwa walioambukizwa miaka mingi iliyopita.
Amesema vimelea vya ugonjwa huo hupatikana na kustawi ndani ya mwili wa binadamu tu na kwamba haviendi sehemu nyingine.