Wahadhiri waanzishiwa tuzo ya mamilioni

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Muktasari:

  • Katika kuwezesha kufanyika nchini zinoakisi ubora, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuanza kutoa tuzo ya Sh50 milioni kwa kila mhadhiri Mtanzania ambaye matokeo ya utafiti wake utachapishwa kwenye majarida ya juu yanayokubalika kimataifa.

Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amezindua tuzo kwa wahadhiri wa elimu ya juu ambao tafiti zao zitachapishwa katika majarida ya juu yanayokubaika kimataifa.

Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Jumapili Machi 26, 2023 wakati akizindua programu hiyo iliyotengewa Sh3 bilioni kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023.

Amesema wahadhiri watakaohusika na tuzo hiyo ni wale waliofanya utafiti kwenye maeneo ya sayansi asilia, hisabati na tiba na matokeo ya tafiti zao kuchapishwa katika majarida ya juu ya kimataifa.

Amesema kwa kawaida matokeo ya mtafiti yatachapishwa katika majarida hayo kama dunia itayatambua na kuona kuwa mtafiti amesogeza uelewa wa binadamu katika maeneo ya sayansi na tiba.

“Sasa dirisha la wale walioweza matokeo ya utafiti wao katika majarida makubwa sana duniani yanayoheshimika ambao wanasayansi wakubwa wanapenda kuchapisha huko,”amesema.

Amesema uamuzi huo hauna lengo la kudharau majarida ya nchini bali ni kuwawezesha wanasayansi wengi kuchapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida hayo na kuheshimika duniani.

Amesema tuzo za mwaka 2022/2023, zitaanza kutolewa kwa wahadhiri ambao tafiti zao zimechapishwa katika majarida hayo kuanzia Julai 2022 hadi Mei 31, 2023.

Aidha, Profesa Mkenda amesema watoto waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kwenye mitihani yao ya kidato cha sita na kukidhi vigezo vya kunufaika na tuzo ya Samia Scholarship watapatiwa vyeti ili waweze kuutumia kwenye wasifu wao.