Wahafidhina wanavyoiweka kwenye wakati mgumu ccm 2025

Thursday November 25 2021
wahifadhinapic

Historia inatuonyesha na kusomeka kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni miongoni mwa vyama vikongwe hapa barani Afrika vilivyobaki madarakani hadi sasa baada ya wimbi la kudai uhuru wa bendera, uhuru wa watu na rasilimali za nchi kumalizika kwa ufanisi wa hali ya juu sana.

Makala ya wiki hii itaangazia kwa undani zaidi dhana ya uhafidhina na athari zake ndani ya chama katika kutimiza wajibu wake ikiwa sambamba na kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, CCM ndicho chama dola na chama tawala cha muda mrefu barani Afrika kwa takribani miaka 44 hadi sasa.

Kisiasa huu ni ukongwe uliotukuka, tunamulika na kuchokonoa yaliyomo ndani ya chama ili kujenga ufanisi wa uongozi bora na utawala wa demokrasia na haki kwa sababu moja tu, CCM ndicho chama dola hivyo kina dhamana pana kwa maisha ya kila siku ya Mtanzania, sharti wapokee na wakubali kukosolewa kimantiki.

Ipo wazi kuwa CCM ni chama chenye historia ya pekee katika falsafa za ukombozi barani Afrika, heshima yake ndani ya mipaka ya Afrika ni ya dhahabu na fedha, CCM ni jabali la siasa za ushawishi na mafanikio katika ukombozi wa mtu mweusi.

Historia inatuonyesha hayo kupitia vitabu na tafiti za machapisho mbalimbali ya kisiasa kulingana na jitihada zake za wazi za kuyakomboa mataifa mengi ya bara hili la Afrika wakati wa kudai uhuru wa mataifa yao.

Hata hivyo, siasa za kizazi cha sasa ni tofauti na siasa za kizazi cha enzi za Mwalimu Julius Nyerere, zama hizi tuna kizazi cha wanasiasa wanafiki, wakora, wanasiasa bendera na wachumia tumbo na si wanasiasa wazalendo wala wenye uchungu wa kufia taifa lao.

Advertisement

Tuna wanasiasa vishoka walio na fikra za kuhujumu zaidi ya kujenga nchi. Si wana siasa wote ni wakora, la asha! Tunao wema na wenye fikra za ukombozi wa taifa kiuchumi, kisiasa na kisayansi.

Hata hivyo, wapo wanasiasa wanaojitambua, wazalendo na wanaojua nini walifanyalo kwa mustakabali wa taifa lao. Tunao wanasiasa wenye utumishi chanya waliolenga kuacha alama.

Ili tujenge ustawi wa mifumo yetu ya siasa kwa kizazi cha sasa ni lazima ‘tufundane kisiasa’, hivyo tusihesabiane siku ili kuumizana, bali tuhesabu siku kujirekebisha na kujenga taifa letu kwa umoja wetu.

Ni dhahiri sasa kuwa upo mstari unaoitenganisha CCM ya Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete, Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan, watangulizi wa Rais Samia chini ya kofia ya uenyekiti wa chama tawala walipambana na uhafidhina ndani ya chama kadri walivyoweza, lakini zama hizi chama hicho kina wahafidhina hatari zaidi pengine kuliko nyakati zilizopita.

Picha ya uhafidhina uliopo ndani ya chama hicho kwa sasa inaweza isitofautiane sana na wahafidhina wa tawala zilizopita.


Uhafidhina ni nini hasa?

Andiko hili linatambua bayana kuwa kumekuwepo na upotoshaji wa wazi juu ya dhana hii ya “Uhafidhina”, msingi wa itikadi ya kihafidhina ni utamaduni unaopingana na zama zilizopo kulingana na historia ya zama zilizopita.

Wahafidhina kwa lugha ya Kiingereza wanaitwa “conservatives” na uhafidhina unaitwa “conservatism”. Uhafidhina ni ile hali ya uasili ya kutokubali mabadiliko ndani ya mifumo fulani, hivyo kuendelea kuishi na kuamini katika misimamo ya kale.

Uhafidhina hutumika zaidi katika masuala ya siasa, kisiasa hizi zinaweza kuwa ndio sifa kuu za uhafidhina Mosi; Kuwa na uasili wa jambo fulani na kutotaka mabadiliko, Pili; kuenzi historia na mifumo ya kiutawala bila kutaka mabadiliko chanya. Tatu; kuwa na mtazamo wa tahadhari unaojikita katika ukosoaji.

Katika siasa za kimataifa unapozungumzia uhafidhina unakuwa unalinganisha na mifumo ya falsafa za kiliberali, kwa mantiki kuwa uliberali ni falsafa, mtazamo au msimamo wa kupenda usawa katika jamii. Kwa nukta ya muhtasari juu ya dhana ya uhafidhina, sasa tujikite kwenye hoja yetu ya wahafidhina ndani ya CCM.

Ni dhahiri shahiri kuwa CCM kwa sasa kinao wahafidhina wengi ambao fikra zao ni kupinga mabadiliko ndani ya chama na Serikali, upingaji huu unaweza kuwa wa heri au wenye hujuma ndani yake kwa utawala wa Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Uhafidhina si dhambi wala jinai ndani ya chama endapo kuna ukinzani wa hoja yenye mantiki na mashiko ya kustawisha mipango na mifumo yenye falsafa ya mageuzi bora, kero hujitokeza pale uhafidhina unapochukua mkondo wa hujuma.

Mathalani, uhafidhina unaojitokeza CCM katikati ya kipindi hiki cha mpito baada ya kifo cha Rais John Magufuli inaweza kutafsiriwa kama hujuma na fujo za makusudi ndani ya chama na ndivyo ilivyo kabisa, aidha kundi hili dogo la wahafidhina ni matokeo ya kukosa tonge la ulaji na pengine kupoteza nafasi za uongozi walizokuwa nazo ndani au nje ya chama.

Sasa wamevimba na kufura unaweza kuwafananisha na volcano iliyolala “dormant volcano”, ambayo siku ikilipuka madhara yake huwa ni makubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

Kundi hili kwa sasa halitaki kuamini katika mabadiliko ya uongozi, sera na falsafa za kutawala na kuongoza nchi, bado wanaamini katika ukale na utawala wa awamu ya tano, hivyo kuona kinachofanyika awamu ya sita si sahihi.

Kundi hili linaweweseka na hivyo kuanza propaganda za kukwamisha juhudi za Mwenyekiti wa chama tawala, Wahafidhina hawa wanatumia dhana ya “ujinsia na “ukabila” kujenga hoja ya kuonewa ndani ya chama na Serikali.

Kutumia ukabila kutafuta huruma ya kisiasa ni sumu kali inayoweza kuwagawa wananchi na hatimaye kuwafarakanisha na kuchafua hali ya hewa, Baba wa Taifa, Julius Nyerere alionya juu ya dhambi ya ukabila.

Ukabila usitumike kujenga hoja za kisiasa, mwanasiasa anayetumia ukabila kuhalalisha hoja zake ni mpuuzi kisiasa na jamii nzima inastahili kumpuuza kabisa.

Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema kila zama na kitabu chake, huu ni utawala mpya, sharti mabadiliko yafanyike kadri ya maono, falsafa na mitizamo ya utawala uliopo madarakani, hivyo ni ngumu kwa utawala mpya kwenda na falsafa za tawala zilizopita.

Je, wahafidhina wanaopinga mabadiliko ya sera za utawala wa awamu ya sita hawajui kanuni na taratibu za mamlaka mpya inapochukua dola?

Kwa jicho la tatu na kwa kutumia dhana ya habari za uchunguzi ni wazi kuwa agenda ya wahafidhina ndani ya CCM si ya heri, bali yenye nia mbaya ya kukwamisha ufanisi wa Serikali ya awamu ya sita na hatimaye chama kushindwa kushika dola ifikapo 2025.

Wahafidhina waliopo ndani ya CCM wanao mtandao mrefu unaopenya hadi serikalini na taasisi zake ili kuhakikisha wanahujumu na kufarakanisha utawala wa sasa na wananchi wake.

Taarifa za kiintelijensia zilizopo zinaonyesha kundi hili la wahafidhina wameanza kuhujumu utawala wa Rais Samia kwa kuhakikisha wanapinga chini kwa chini sera na mipango na baadhi ya shughuli za kimaendeleo ili ifikapo 2025 Rais Samia asiwe na ushawishi wa kuchagulika ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kundi hili la wahafidhina kwa sasa wanatumia hoja za kuwaondoa wamachinga pembezoni mwa barabara kwenda sehemu rasmi kama hoja ya uchonganishi, aidha agenda ya fedha ya Uviko-19 inapotoshwa hili kuchonganisha watu na kiongozi wao.

Ajenda yao nyingine wanayoitumia kuleta nongwa ni pamoja na kuhoji ni kwa jinsi gani Rais anafungua nchi, kwani ilikuwa imefungwa? Ukiwasikiliza kwa makini utagundua ni wahafidhina wenye nongwa na utawala uliopo.

Endapo Mwenyekiti wa CCM atashindwa kuonyesha ukali zaidi dhidi ya wahafidhina waliomo ndani ya chama au kuwazuia mapema, huenda uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ukawa mgumu kwa chama hicho tawala.

Je, wahafidhina hawa wataipeleka CCM nje ya dola na hivyo kuwa chama cha upinzani baada ya uchaguzi mkuu ifikapo 2025?

Imeandikwa na Deogratias Mutingi

[email protected]

0717718619

Advertisement