Wahamasishwa kulima mazao kuongeza mapato ya halmashauri

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma.

Ruangwa. Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma amewataka wakuu wa wilaya zote zinazounda ushirika wa Chama Kikuu cha Runali kusimamia kwa umakini na kuwekeza jitihada kubwa katika zao la korosho na ufuta katika halmashauri zao ili yaweze kuongeza mapato ya halmashauri hizo.

Ngoma ameyazungumza hayo katika mkutano mkuu wa 6 wa Chama Kikuu cha Runali wakati alipofungua mkutano mkuu   ambao umefanyika leo Aprili 20 2023 huku  akiwasisitiza wakurugenzi wa Halmashauri za Ruangwa, Nachingwea na Liwale kuwasimamia na kutetea masilahi ya wakulima  ili kudumisha uhai wa halmashauri zao.

‘’ Nje ya mapato ya ufuta na korosho hakuna Halmashauri ya Liwale, Ruangwa wala Nachingwea mazao hayo ndio Maisha kwenye halmashauri zetu hivyo Ma DC tunapaswa kuwatizama na kuwasimamia wakulima vizuri kwani wakishindwa kuzalisha halimashauri zitayumba,’’amesema DC Ngoma.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Goodluck MLinga amewataka viongozi wa vyama vya msingi kuwa waaminifu katika malipo ya wakulima kwakuwa atatumia vyombo vya dola pale itakapobainika viongozi hao “kupiga” fedha za wakulima.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo amewataka viongozi wa AMCOS kuunda SACCOS zitakazosaidia kuweka akiba na kukopa.

Lengo kubwa ni kuweza kusaidia kuwavutia wakulima wengi kujiunga katika vyama vya msingi kukwepa biashara ya kangomba inayowaumza wakulima wengi.

 Pia kuwahimiza viongozi wa ushirika kujali masilahi ya mkulima ili kilimo mazao ya korosho, ufuta, alizeti na mbaazi kiwainue wakulima kwani Ushirika ni biashara.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri Wilaya ya Ruangwa, Maisha Mtipa amesema ushirikiano wa vyama vya msingi ni  na chama kikuu cha ushirika runali ni jambo la msingi linalo imarisha na kustaeisha halimashauri hizo hivyo amehimiza ushirikiano ili kuwahudumia wananchi kwa tija huku Ded Wilaya ya Nachingwea, Chihonda Kawawa amesema Runali inashiriki maendeleo katika jamii jambo ambalo linakuza uchumi wa Taifa la Tanzania.