Wahamiaji haramu wakamatwa wakisafirishwa uvunguni mwa gari

Baadhi ya wahamiaji haramu watano kutoka nchini Ethiopia wakiwa wamekamatwa mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye gari ya kubeba gesi katika eneo la Mji mdogo wa Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Raia hao wa Ethiopia wamekutwa wakiwa chini ndani ya gari hilo, sehemu ambayo siyo salama na gari hilo ni maalumu kwa ajili ya kusafirisha gesi.
Rombo. Siku chache baada ya wahamiaji haramu saba kutoka Ethiopia kukamatwa wakisafirishwa kwa gari la kifahari ‘shangingi’ mkoani Kilimanjaro, wahamiaji haramu wengine watano kutoa nchi hiyo wamekamatwa katika mji mdogo wa Tarakea, Wilaya ya Rombo wakisafirishwa wakiwa chini ya lori la kubebea gesi.
Wahamiaji haramu hao wamekatwa jana mchana Juni 19, 2024 katika kituo cha Tarakea wakitokea upande wa nchi jirani ya Kenya wakiwa katika gari hilo la gesi, mazingira ambayo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa raia hao, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga amesema wamekamatwa jana saa 7 mchana kupitia vituo cha forodha cha Tarakea wakitokea nchini Kenya na kuingia Tanzania wakiwa chini ya gari hilo la gesi.
“Tuko hapa Wilaya ya Rombo, kituo cha kutoka na kuingia nchini cha Tarakea, tumewakamata raia watano kutoka nchi ya Ethiopia ambao wamekamatwa wakiwa katika gari la kusafirishia gesi,” amesema.
Ameongeza kuwa raia hao wamekutwa wakiwa chini ndani ya hilo gari sehemu ambayo siyo salama na gari hilo halitumiki kusafirisha abiria, ni la gesi, hawasafiri kwa kutumia vyombo ambavyo vinaruhusu wao kutumia kwa mfano mabasi, gari hili walilopanda haliruhusiwi kusafirisha abiria.
Amesema mbali ya kuwa katika gari hilo katika mazingira hatarishi kwa afya yao, walipita bila kuwa na vibali wala hati za kusafiria.
“Tumewakamata hawa na hili gari si la Tanzania tutaendelea na taratibu za uchunguzi na hatimaye kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Ametoa wito kwa wafanyakazi vituo vya mpakani upande wa Tanzania na Kenya kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri vinavyopita kwenye eneo la mpakani ili kuhakikisha vitu vinavyopita havihatarishi usalama wa nchi.
“Wito wetu hapa mpakani, tunaomba wafanyakazi upande wa Kenya na Tanzania kwa maana ya forodha, uhamiaji na taasisi nyingine wajitahidi kadri wanavyoweza kufanya ukaguzi wa vyombo vinavyopita kwenye eneo la mpaka ili kuhakikisha vitu vinavyopita ni vitu ambavyo havihatarishi usalama wa nchi yetu ama nchi ya jirani.
“Lakini pia nitoe wito kwa wananchi, madereva wa malori na magari mengine, kuhakikisha wanapakia vitu vinavyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria tofauti na hivyo ni kwamba wanahatarisha usalama wa nchi yetu,” amesema.
Amesema Uhamiaji wanaendelea na programu ya “Mjue jirani yako” ikiwa na lengo la kuwabaini wale ambao wanakiuka taratibu za Uhamiaji na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Tunaomba tuendelee kushirikiana na wananchi, viongozi wa mitaa, vijiji, pamoja na wasafirishaji, tuhakikishe tunatoa taarifa pale tunapoona kuna mtu au watu ambao hawaeleweki tutoe taarifa kwenye vyombo na mamlaka husika ili waweze kushughulikiwa maana wanasafiri katika mazingira magumu,” amesema.