Wahariri wa vyombo vya habari wanolewa kubaini bidhaa ‘feki’

Muktasari:
- Wahariri wa vyombo vya habari wamepewa elimu ya kukabiliana na bidhaa bandia ili habari zinazoandikwa zitoe ujumbe sahihi kwa walaji.
Dar es Salaam. Katika mkakati wa kukabiliana na bidhaa bandia nchini Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imekutana na wahariri wa vyombo vya habari kuwapa elimu ili kuandika habari zitakazotoa elimu sahihi kwa watumiaji.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Aprili 13, 2023, katika semina hiyo iliyokuwa na mada ‘Kumlinda mlaji na wajibu wa wahariri’, Mkurugenzi Mtendaji wa FCC, William Erio amesema semina hizo ni endelevu Kwa makundi mbalimbali na wanajua wahariri wakipata elimu hiyo itakuwa rahisi kuandika habari zitakazotoa ujumbe mzuri.
"Tunataka umma ujue na kama mnavyojua suala la mapambano ya bidhaa bandia ni vita ya dunia nzima, tumekutana na wahariri wa habari ikiwa ni mwendelezo wa kuendelea kutoa elimu, wapate uelewa ili waandike habari zinazotoa ujumbe sahihi kwa wananchi kujikinga na bidhaa bandia," amesema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kupata semina hizo zina umuhimu kwao kwa kuwa ni fursa ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayoleta utata.
"Watanzania wanahitaji uelewa kuhusiana na bidhaa bandia na kuwafikishia taarifa sahihi na ni haki yao kukataa bidhaa bandia," amesema.
Amesema Watanzania wakipata elimu itakuwa rahisi pale wanapenda kununua bidhaa kuchukua risiti na ikibainika ni bandia warudishe walikokinunua.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu amesema wanafanya biashara wanapotekeleza shughuli zao wanapaswa kuzingatia misingi ya kisheria ili kuhakikisha wanashindana kwa ubora wa bidhaa sokoni na mlaji wa mwisho anufaike.
"FCC jukumu lake ni kuchochea ushindani sokoni lakini kukabiliana na bidhaa bandia ili mlaji akienda kununua apate bidhaa bora ili kulinda afya zao," amesema Machumu.