Wahitimu mafunzo ya mgambo Hanang' kulinda mradi bomba la mafuta
Muktasari:
- Wahitimu 83 wa mafunzo ya mgambo Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara wameahidiwa ajira ya ulinzi katika mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda linalopita katika eneo hilo.
Hanang'. Wahitimu 83 wa mafunzo ya mgambo Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara wameahidiwa ajira ya ulinzi katika mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda linalopita katika eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Hanang', Janeth Mayanja akizungumza kwenye hitimisho ya mafunzo hayo yaliyofanyika Kata ya Nangwa, amesema wahitimu watapewa kipaumbele cha ajira katika mradi huo wa bomba la mafuta.
"Pamoja na ajira ya bomba pia wahitimu watapewa kipaumbele kwenye nafasi za ajira katika jeshi la kujenga Taifa (JKT) pindi zikitoka," amesema Mayanja.
Amewakaribisha viongozi wa SUMA JKT waliohudhuria hitimisho la mafunzo kutoa kipaumbele kwa wahitimu hao kwa ajili ya kazi za ulinzi na udereva.
Mmoja kati ya wahitimu wa mafunzo hayo, Gilbert John amesema wanatarajia mradi wa bomba la mafuta utakapoanza nao watanufaika.
"Pamoja na sisi hata dada zetu na mama zetu watanufaika kwa kuuza vyakula kwa watu watakaokuwa wanafanya kazi katika huu mradi," amesema.
Vijiji vinne vya wilaya ya Hanang' vitapitiwa na mradi huo unaotokea Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga, ambapo mkoani Manyara, litapita kwenye wilaya mbili pamoja na Kiteto.