Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahudumu wa afya 4,000 ngazi ya jamii Lindi kuchaguliwa

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa huo (hawapo pichani) katika semina elekezi kwa ajili ya watoa huduma wa afya ngazi jamii. Picha na Bahati Mwatesa.

Muktasari:

  • Baada ya Serikali kuzindua Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma ya afya ngazi ya jamii, Mkoa wa Lindi utachagua wahudumu wa afya

Lindi. Zaidi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii 4,856 watachaguliwa mkoani Lindi kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya kila sehemu.

 Akizungumza kwenye semina elekezi leo Juni 11, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema watoa huduma ya afya ngazi ya jamii watasaidia kuhakikisha huduma za afya zinafika kila mahali na kufanya huduma hizo kumfikia kila Mtanzania.

Ndemanga amesema mpango wa huduma za afya ngazi ya jamii unaolenga kuhakikisha afua za afya, ustawi wa jamii na lishe, unaimarishwa katika ngazi ya jamii, kwa kuwatumia watoa huduma hao.

“Nitoe wito kwa viongozi kuepuka rushwa, udanganyifu na dhuluma wakati wa mchakato wa kuwapata watoa hudumu wa afya ngazi ya jamii na shughuli hii itafanyika katika Halmashauri ya Mtama pamoja na Manispaa ya Lindi,” amesema Ndemanga.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Ngazi ya Jamii, Orsolina Tolage amesema utekelezaji huo unaoendelea unalenga kuhakikisha unaimarisha huduma za afya ngazi ya jamii ili kufikia malengo ya Serikali ya afya kwa wote

“Mikoa yote Tanzania Bara tutachukua watoa huduma 137,219 ili kusaidia Serikali katika kufikia malengo ya afya kwa wote,” amesema Orsolina.

Mkazi wa Manispaa ya Lindi, Awetu Malunda amesema wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanasaidia kuibua wagonjwa wanaoishi vijijini ambao  hawana uwezo wa kufika hospitali, yaweza kuwa kwa kipato au hofu ya kwenda kupatiwa matibabu.

“Kuna wagonjwa wengi wapo majumbani ambao hawana uwezo wa kufika hospitali aidha kifedha au hofu, hawa watoa huduma ngazi ya jamii wanakwenda kuwaibua na kuwafikisha hospitali au kuwatibu wao wenyewe,” amesema Malunda.

Bushiri Ulaya ambaye ni mkazi wa Lindi amesema Serikali walichokifanya ni jambo jema kwa kuwa baadhi ya watu walio vijijini wamekuwa wazito kwenda hospitali licha ya kuwa vituo vya afya vipo karibu.

“Utakuta bibi anaumwa, ukimwambia twende hospitali, hataki, lakini hawa watoa huduma watakwenda kuwaibua wagonjwa ambao hawataki kwenda hosptali, watapatiwa matibabu kupitia kwa watoa huduma hao kwa kuwa wamepata mafunzo, wataweza kuongea na mgonjwa na akamuelewa tofauti na yule asiyepata mafunzo,” amesema Bushiri.