Waitwa kuutambua mwili uliookotwa kwenye kiroba Dodoma

Muktasari:

Mwili huo uliokotwa Jumatatu Desemba 5, 2022 jirani na shule ya Sekondari Jamhuri jijini Dodoma ukiwa umefungwa kwenye kiroba na kutupwa ndani ya mtaro.

Dodoma. Ikiwa zimepita siku nne tangu mwili wa mtu mmoja ambaye hajafahamika uokotwe ukiwa katika kiroba jijini Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma imewaomba wananchi kufika mochwari kwa ajili ya kuutambua.

Mtu huyo ambaye ni mwanaume anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25-30, mwili wake uliokotwa Jumatatu jirani na shule ya sekondari Jamhuri ukiwa umefungwa kwenye kiroba na kutupwa ndani ya mtaro.

Mwili huo uligunduliwa na wapita njia huku sehemu ya kichwa kikiwa kinaonekana hali iliyozua taharuki.

Jeshi la Polisi lilifika katika eneo hilo na kuuchukua mwili huo na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambapo upo mpaka sasa.

Hata hivyo mwili huo tayari umeanza kuharibika kutokana na kukaa kwa zaidi ya siku 4 ndani ya maji.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 8, 2022 Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mwahija Amrani amesema mwili huo bado upo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

"Tunawaomba wananchi waje kuutambua mwili huu kwani mpaka sasa bado ndugu zake hawajapatikana," amesema Ofisa huyo.

Mhudumu wa mochwari katika hospitali hiyo, Anwary Selemani amesema mwili huo ulifika katika Hospitali hiyo ukiwa umeharibika na ngozi ikianza kutoka kutokana na kukaa muda mrefu ndani ya maji.

Amesema mwili huo ulikuwa ukitoa harufu kali hali ambayo iliwalazimu kufungua kwa muda madirisha ya sehemu ya kuhifadhia maiti.

Mhudumu huyo amesema baada ya kuufanyia uchunguzi ulionekana hauna majeraha wala mvunjiko wa aina yoyote.