Mwili uliookotwa kwenye kiroba Dodoma haujatambuliwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno

Muktasari:

Mwili wa mtu uliookotwa ukiwa katika kiroba eneo la jirani na Shule ya Sekondari Jamhuri jijini hapa, bado haujatambuliwa.

Dodoma. Mwili wa mtu uliookotwa ukiwa katika kiroba eneo la jirani na Shule ya Sekondari Jamhuri jijini Dodoma, bado haujatambuliwa.

Mwili huo ambao ni wa mwanaume na umekutwa ukiwa umeanza kuharibika, bado upo katika chumba cha kuhifadhia maiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi mkoani hapa, kujua kinachoendelea kuhusu mwili huo alijibu kuwa yupo katika msafara wa viongozi, hivyo hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza.

Mwili huo uligunduliwa na wapita njia juzi asubuhi katika eneo ambalo lina msongamano wa watu, ambapo upande mmoja kuna shule za Msingi Uhuru, Sekondari ya Jamhuri, wakati upande wa pili kuna kituo cha mafuta, waponda kokoto na mchanga, soko la machinga na mita chache kuna kituo kidogo cha polisi Kata ya Majengo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Wahija Amrani alisema waliupokea mwili huo juzi mchana kutoka kwa polisi.

Wahija alisema licha ya watu wengi kufika katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya utambuzi, hakuna aliyetoa taarifa ya kuutambua au kuhisi kama ni mtu wanayemfahamu.

“Watu wengi wamekuja na kuulizia na tumekuwa tukiwaonyesha, ila bado wahusika hawajapatikana,” alisema Ofisa Uhusiano huyo.

Mwili waharibika

Kwa upande wa mhudumu wa mochwari katika hospitali hiyo, Anwary Selemani alisema mwili huo ni wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30.

Selemani alisema mwili huo ulifika ukiwa umeharibika na ngozi ikianza kutoka kutokana na kukaa muda mrefu katika maji.

Kwa mujibu wa Selemani, mwili huo ulikuwa hauna viatu, shati wala kitambulisho chochote, hivyo imekuwa ngumu kumtambua anakotokea na jina lake. “Uchunguzi ulionyesha hauna majeraha wala mvunjiko wa aina yoyote ila taarifa zaidi anazo daktari.”

Matukio ya kuokotwa kwa miili ya watu ikiwa kwenye viroba yaliripotiwa mwishoni mwa mwaka 2016 na mwanzoni mwa 2017, kabla ya kukoma kwa matukio hayo na hili ni tukio la kwanza kwa Mkoa wa Dodoma katika miongo kadhaa.